Serikali  katika mwaka wa fedha 2019/20 imetumia Shilingi bilioni 2.3 kununua vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule za msingi 708 na sekondari 45 nchini.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa vifaa hivyo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu  amesema  vifaa hivyo vinalenga kuimarisha ujifunzaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum waliopo katika shule za Msingi na Sekondari nchini.

Dkt. Semakafu amesema pamoja na kugawa vifaa hivyo Wizara iliendesha mafunzo kwa walimu wa  lugha ya alama wanaofundisha  shule za sekondari ili waweze kutekeleza jukumu la ufundishaji ikiwa ni  pamoja na  kutengeneza Kamusi ya lugha za alama ya kufundishia shule za msingi na sekondari.

"Tunashukuru maono ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa baada ya kuingia madarakani imefungua fursa za  elimu kwa kuondoa vikwazo vilivyokuwa vinasababisha watoto kufaidika na fursa hizo.  Katika kuhakikisha tunatekeleza hilo Wizara ya Elimu  iliandaa mkakati wa kujibu ombwe hilo ambao ni kuwapatia vifaa wezeshi na vya kielimu watoto wenye mahitaji maalum," amesisitiza Dkt. Semakafu

Dkt. Semakafu amemtaka Mkurugenzi wa Elimu maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi naTeknolojia Dkt. Magreth Matonya kuwa na eneo la kipaumbele la kushughulikia  kila mwaka kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, na kwamba kwa mwaka wa fedha unaoanza 2020/21 kipaumbele kielekezwe kwa wanafunzi wenye usonji ili kuwezesha upatikanaji wa elimu bila changamoto.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Elimu Maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Magreth Matonya ametaja baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa kuwa ni mashine kubwa ya kuchapa maandishi ya wasioona, mashine 27 za kurudufisha maandishi ya nukta nundu, mashine 60 za kupima kiwango cha usikivu na vifaa 60 vya kufundishia matamshi kwa wanafunzi wenye changamoto ya matamshi.

Vingine ni miwani 5,167 za kuzuia mionzi ya jua, vioo 2,067 vya kukuzia maandishi kwa watoto wenye ualbino na uoni hafifu, vifani 5,720,  abakasi 9,909, pazo 2,260 za kufundishia stadi za kujimudu na hisabati kwa watoto wenye ulemavu wa akili na wenye usonji pamoja na vitimwendo kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo.

Naye Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam Maulid Maulid amemuhakikishia Naibu Katibu Mkuu Semakafu  kuwa vifaa hivyo vitafika shuleni kwa wakati na vitatumika ipasavyo badala ya kufungiwa stoo.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake mwanafunzi Selemani Joseph kutoka shule ya Sekondari Pugu ameishukuru Serikali kwa kuwapatia vifaa hivyo na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia kusoma bila changamoto yoyote.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akizungumza wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa shule za Msingi na Sekondari jijini Dar es Salaam.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa wenye mahitaji maalum walioshiriki tukio la uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu liliofanyika jijini Dar es Salaam
 Mwanafunzi Agustino Ilomo kutoka Shule ya Sekondari Tabata Kimanga akifurahi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu alipokabidhiwa  laptop wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu uliofanyika jijini Dar es Salaam
 Naibu Katibu Mkuu Dkt. Ave Maria Semakafu akimkabidhi kifaa saidizi mwanafunzi Godfrey Moris kutoka shule ya sekondari Pugu wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...