Na Said Mwishehe,Michuzi TV.
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) umeamua kuwanoa baadhi ya watendaji wake kwa kuwapatia mafunzo ya upangaji madaraja ya mbao na ukaguzi wa mazao ya misitu na kuwataka watendaji hao kujiepusha na aina yoyote ya vitendo vya rushwa katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa mujibu wa TFS watendaji waliopatiwa mafunzo hayo ni 10 na wanatoa katika mikoa mbalimbali ambao walikuwa wakipata mafunzo katika Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) kilichopo Moshi mkoani kilimanjaro na sasa wamehitimu na kukabidhiwa vyeti vyao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana kabla ya kukabidhi vyeti kwa wahitimu wa mafunzo hayo, Kamishna Mhifadhi Misitu kutoka Wakala wa Misitu Tanzania(TFS)Profesa Dos Santos Silayo ametumia nafasi hiyo kueleza sababu za kutolewa mafunzo hayo ni kutokana na kutambua umuhimu wa eneo hilo la ukaguzi na upangaji madaraja wa mazao ya misitu.
"Sasa hivi nchi yetu imepiga hatua kubwa kimaendeleo na kwenye sekta ya misitu ni eneo ambalo tunajivunia, katika miaka ya karibuni na hasa hii miaka mitano ya utawala wa Rais wetu mpendwa Dk.John Magufuli tumekuwa na ongozeko kubwa la viwanda vinavyochakata bidhaa zitokanazo na mazao ya misitu.
"Lakini tunajivunia zaidi sio wingi wa viwanda lakini teknolojia ambayo imeongeza tija katika uchakataji mazao.Kwa hvyo ubora wa mazao yetu sasa hivi umekuwa mkubwa , mzuri lakini kubwa zaidi kuna bidhaa nyingi tofauti kuliko tulivyozoea hapo awali, tunaviwanda vinachakata na kufanya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na misitu kuliko hapo awali lakini kwa ubora wa hali ya juu,"amesema Profesa Silayo.
Ameongeza kutokana na mabadiliko katika utendaji na uwekezaji, hivyo TFS wameona ni fursa kuwafundisha watendaji wao ili waweze kwenda na kasi hiyo ya mabadiliko ya uboreshaji wa viwanda vyenyewe , uboreshaji wa teknolojia na uboreshaji wa bidhaa zenyewe zitokanazo na mazao ya misitu.
"Ndio maana tukaona tuwapeleke kwenye mafunzo ili msije kuachwa nyuma na ile spidi ya uwekezaji,tulizoea kuwa na viwanda vinavyochakata vitu ambavyo tumevizoea zoea vya kupasua tu mbao,sasa nchi yetu inaviwanda vya kila aina vinavyojihusisha na utengenezaji bidhaa zinazotokana na mazao ya misitu.
"Tunaviwanda vya kutengeneza mbao, kuchakata nguzo na kutengeneza nguzo za umeme, tuna viwanda vinavyotengeneza nishati mbadala ya mkaa unaotoka kwenye misitu asili na huu unaotokana na mkandamizo wa taka ngumu.Kwa hiyo mtawanyiko ule wa bidhaa zinazozalishwa sasa hivi tunahitaji watu ambao wamepita mafunzo ya kuweza kutambua na kuangalia ubora wa bidhaa,"amesisitiza.
Amefafanua katika biashara ya mazao ya misitu kuna makubaliano mbalimbali ya kimkataba ambayo nchi yetu imeingia ikiwemo ya ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini na ubora wa bidhaa zinazoingia nchini, hivyo kwa kutumia watalaamu hao TFS inaamini bidhaa zitokanazo na mazao ya misitu zitakuwa bora na zenye viwango vinavyotakiwa.
"Katika biashara ya mazao ya misitu lazima tuwe na watu wanaoweza kuangalia bidhaa zinazotoka nje za mipaka ya nchi yetu lakini tuwe na watalaam wanaoweza kuhakikisha ubora wa bidhaa zinazoingia kwasababu jinsi nchi inavyoendelea kukua kiuchumi, uwezo wetu wa kuingiza bidhaa hapa ndani nao uaongezeka kwa maana ya uwekezaji unaofanyika.
"Hivyo lazima tuwe na watu wanaoweza kuwa na uwezo wa kuangalia ubora wa bidhaa tunazopokea ili tusiwe tunapokea bidhaa ambazo hazina ubora , ubora ambao unatakiwa kwa mujibu wa kimataifa, hivyo tukaona tuwafundishe watendaji wetu kwa ajili ya kazi hiyo,"amesema Prof.Silayo.
Amesema kupitia watalaam hao wa upangaji mdaraja ya mbao na ukaguzi wa mazao ya misitu watakuwa chachu ya kuhakikisha soko la Tanzania katika biashara hiyo linaendelea kuwa kubwa zaidi.
"Tuwe chachu ya kuuhisha uchakataji wa mazao ya misitu yanayokidhi ubora wa soko la ndani na nje , tunatambua walioko sasa ni wachache lakini tutaendelea kufundisha wengine.Lengo letu ni kuwa na watalaam wengi zaidi katika eneo hilo na ambao mmepata mafunzo haya najua mmejifunza vitu vingi.
"Mmejifunza vitu vinavyohusiana na mahesabu , sababu ubora lazima ufahamu na hesabu, ili ujue kiwango lazima ufahamu hesabu, lakini tunatambua kwenye kufanya kazi hii ya ukaguzi mnakutana na wafanyabiashara wa aina mbalimbali , wapo waadilifu na wapo ambao sio waadilifu.
"Wanaoweza kutaka kuwarubuni ili kubadilisha madaraja ,sasa tumefanya jitihada za kuhakikisha mnakutana na watalaam wanaoweza kuwafundisha mbinu za kukwepa rushwa, mbinu za kubaini wanaoweza kuwarubuni katika rushwa ili mnapofanya kazi zenu na serikali mfanye kwa kutumia weledi lakini msimame imara katika kulinda maadili ya kazi,"amesema.
Mbali na mafunzo hayo, amesema kuwa tayari kuna nyaraka ambazo zimendaliwa na kupelekwa Shirika la Viwango Tanzania(TBS) kwa ajili ya kuandaa mcahakato wa kuwa na viwango vya ubora vya bidhaa zinaztokana na mazao ya misitu na hivyo baada ya hapo watatumia viwango vya TBS kulinda ubora wa bidhaa hizo.
"Tunataka tuwe na viwango vya ubora vya TBS ili tuwe na uwezo wa kuvigawa kwa madaraja ya ubora kulingana na viwango vya TBS,kwa hiyo tumepiga hatua ya namna hiyo lakini tumepiga hatua zaidi kuhakikisha tunakuwa na utambuzi wa ubora wa misitu yetu.
"Kwa watalaam hawa ambao wamehitimu mafunzo yao wamekuja wakati muafaka sana wakati ambacho nchi yetu ipo kwenye mabadiliko mengi, ongezeko la viwanda, uwekezaji na ukuaji wa teknolojia umeongezeka,"amesema Prof.Silayo na kuongeza Serikali kupitia TFS inayodhamana ya kuhakikisha misitu inasimamiwa vizuri , inatoa mazao ya kutosha na mazao bora na yanapochakatwa basi wachakataji wawe wanazingatia ubora na viwango vinavyotakiwa.
Awali akisoma risala ya watendaji hao , Dyaga Mkomwa ambaye ni mtumishi wa TFS -Temeke jijini Dar es Salaam amesema kupitia mafunzo hayo wamefanikiwa kutambua namna ya kukagua na kupanga kwa ufanisi madaraja ya mazao ya misitu mbalimbali kulingana na sifa na ubora wake."Tulipata nafasi yakujaribu kanuni mbalimbali za kutafuta ujazo wa mbao, ambapo washiriki tulipewa nafasi ya tuelekeze namna tunavyotafuta ujazo katika vituo vyetu vya kazi, hivyo kujua na kutambua umuhimu wa kutumia kanuni moja katika kutafuta ujazo."
Kamishna Mhifadhi wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) aliyesimama kushoto Profesa Silayo akikabidhi leseni ya mtumishi wa Wakala huo kutoka wilayani Korogwe mkoani Tanga Maria Karawa( kulia)baada ya kumalizika kwa mafunzo ya upangaji madaraja na ukaguzi wa mbao .
Profesa Dos Santos Silayo ambaye ni Kamishna Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( kushoto) akiwa ameshikana mkono na Mtumishi wa Wakala huo Dyaga Mkomwa (kulia) baada ya kuhitimu mafunzo ya upangaji madaraja ya mbao na ukaguzi wa mazao ya misitu ambayo yamefanyika Chuo cha Viwanda vya Misitu( FITI).Profesa Silayo ndio aliyekabidhi vyeti kwa wahitimu wa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Mratibu wa mafunzo kutoka Chuo cha Viwanda vya Misitu( FITI) Moshi Cathbert Naburu akizungumza wakati wa hitimisho la mafunzo ya upangaji madaraja ya mbao na ukaguzi wa mazao ya misitu kwa watumishi 10 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS) lililofanyika jijini Dar es Salaam ambapo Kamishna Uhifadhi Misitu kutoka TFS alikabidhi vyeti kwa wahitimu wa mafunzo hayo
Kamishna Uhifadhi Misitu kutoka TFS Profesa Dos Santos Silayo akifafanua jambo kwa wahitimu wa mafunzo hayo
Kamishna wa Uhifadhi Misitu kutoka TFS Profesa Dos Santos Silayo( wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maofisa wa TFS, Viongozi wa Chuo cha Viwanda vya Misitu( FITI) pamoja na wahitimu wa mafunzo hayo waliosimama nyuma baada ya kutunukiwa vyeti









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...