Meneja wa Mawasiliano wa Tigo Tanzania, Woinde Shisael akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani). kuhusu udhamini wao wa mawasiliano kwenye maonyesho ya biashara yanayoratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini Tanzania (TanTrade) kulia kwake ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa TanTrade, Theresa Chilambo Mapema leo Dar Es salaam. 

 Kampuni ya mawasiliano inayoongoza kwa kutoa huduma za kidigitali nchini, Tigo Tanzania, kwa mwaka wa tano mfululizo, inakuwa mdhamini mkuu wa mawasiliano kwenye maonyesho ya biashara yajulikanayo kama Dar es Salaam International Trade Fair (DITF) au ‘Maonyesho ya Sabasaba’ yanayoratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini Tanzania (TanTrade) ambayo hufanyika kila mwaka.

Maonesho ya mwaka huu, yanafanyika chini ya kauli mbiu isemayo Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu’. Katika kuunga mkono kauli mbiu hii, Tigo itaonyesha bidhaa pamoja na huduma ambazo zina mchango mkubwa katika kuhakikisha uchumi wa viwanda unafikiwa..

Akizungumza juu ya ubia huu, Meneja wa Mawasiliano wa Tigo Tanzania, Woinde Shisael, amesema Tigo imekuwa mbia mkubwa wa DITF katika kipengele cha mawasiliano kwa mwaka wa tano mfululizo. Amesema ushirikiano huu unaonyesha namna Tigo ilivyojizatiti katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua biashara pamoja na ukuaji wa viwanda vya ndani ili kuongeza pato na uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa TanTrade, Theresa Chilambo, ameipongeza na kuishukuru Tigo kwa udhamini huu. Chilambo amesema kuwa TanTrade inajivunia kuwa na mbia wa kuaminika katika kipengele cha mawasiliano na kwamba TanTrade iko tayari kushirikiana kikamilifu na Tigo kwenye maonyesho ya mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Tigo imeingia ubia na kampuni zinazo uza simu za mkononi ili kuweza kutoa ofa kabambe ikiwemo huduma za intaneti pamoja na promosheni za simu janja kwa maelfu ya wateja watakaoudhuria maonyesho ya Sabasaba yanayofanyika katika VIwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Tunapoingia kwenye msimu wa kusisimua wa maonyesho ya Sabasaba, tumeandaa huduma bora za intaneti pamoja na simu janja kwa ajili ya wateja wetu. Tumeingia ubia na makampuni ya Nokia, Samsung, TECNO Mobile na KaiOS ili kuwapa wateja wetu wigo mpana wa kuchagua ofa za intaneti pamoja na simu janja zinazofaa kwa mahitaji yao,” amesema Shisael.

“Wateja wataweza kupata ofa kabambe na maalum ambazo ni pamoja na simu janja za bei nafuu kama vile Kitochi 4G Smart, Tecno S3, Tecno R7, Samsung A2 core na Nokia C2 bila kusahau bando ya intaneti ya GB 78 bure kwa mwaka mzima yenye spidi ya mtandao wa Tigo 4G+. Kwa kuongezea, wateja watapata fursa ya kununua muda wa maongezi pamoja na vifurushi wavipendavyo kwa kutumia huduma yetu mpya iliyozinduliwa hivi karibuni ijulikanayo kama Tigo Rusha itakayokuwa inatolewa kwenye banda letu,” Shisael ameongeza.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwataarifu wateja wetu na wanaotarajia kuwa wateja wetu wa hapa Dar es Salaam pamoja na nchi nzima kuwa watembelee banda letu katika msimu huu wa maonyesho ya Sabasaba ili waweze kupata huduma za moja kwa moja kutoka kwa watoa huduma wetu makini bila kusahau ofa kabambe ambazo zinatolewa na kampuni yetu,” amesema Shisael.

Wateja wanakaribishwa kutembelea banda la Tigo ambalo litakuwa likitoa huduma kwa wateja, dawati la kitengo cha biashara pamoja na burudani kwa watoto. Banda la Tigo linatarajia kupokea watu zaidi ya 500 kwa siku katika msimu huu wa Sabasaba. Pia, wateja wanakumbushwa kuzingatia masharti ya afya wanapotembelea banda letu katika Viwanja vya Sabasaba ikiwa ni pamoja na kuachiana nafasi kati ya mtu na mtu, kunawa mikono kwa maji safi au kutumia vitakasa mikono pamoja na kupima jotoridi la mwili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...