Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangalla amezindua rasmi Mpango mpya wa kukuza utalii wa ndani unaojulikana kama Domestic Tourism Promotion Initiative (DTPI) huku akitoa wito kwa watanzania hususani vijana kushiriki zaidi kwenye sekta hiyo.
Mkakati huo wenye kauli mbiu ‘Utalii Mpya.Fursa Mpya’ unaratibiwa kwa pamoja  baina ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) , kampuni ya Real PR Solutions ya jijini Dar es Salaam, BRAJEC,  pamoja na kampuni ya Peak Performance iliyojikita kwenye masuala ya uendelezaji ustadi wa watu hususani katika sekta ya utalii
Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam mapema ulihusisha na viongozi wengine waandamizi kutoka serikalini na pamoja na wadau wa utalii hapa nchini wakiwemo Bodi ya Utalii  Tanzania (TTB), Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Chama cha watoa huduma za utalii wa ndani  (TLTO) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Wengine ni pamoja na Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS),Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA), Taasisi ya Sekta binafsi (TPSF), Viongozi waandamizi kutoka mashirika ya ndege la Tanzania (ATCL) na Shirika la ndege la Precision Air pamoja na wadau wengine.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Dk Kigwangalla alisema mpango huo umekuja wakati muafaka wakati ambapo serikali imejizatiti kuhakikisha sekta hiyo inamilikiwa kwa kiasi kikubwa na wadau kutoka ndani ya nchi wakiwemo wawekezaji wadogo ili kutoa fursa za ajira na kutoa nafasi kwa wadau hao kushiriki kukuza sekta hiyo.
“Katika kufanikisha ushiriki wa wawekezaji wazawa hususani wale wadogo wadogo kwenye sekta ya utalii serikali iliamua kushusha tozo mbalimbali  na mashariti ambayo yalikuwa kikwazo kwa wadau hao kushiriki kwenye sekta hii muhimu’’.
Akifafanua zaidi kuhusu hilo Dkt Kigwangalla alisema uamuzi huo wa serikali umewezesha ongezeko kubwa la wadau hao kushiriki kwenye sekta ya utalii ambapo kwa wa mwaka 2019 idadi ya wawekezaji kwenye sekta hiyo iliongezeka kutoka 1,100 hadi kufikia wawekezaji takribani 2000  ambapo 600 kati ya hao ni wawekezaji wapya wazawa.
Kwa upande wake Mshauri Mkuu wa Mpango huo, Dkt Fenella Mukangara alisema mpango huo unaohusisha juhudi mahsusi katika kusaidiana na  serikali  kukuza utalii wa ndani na kupunguza athari za janga la Corona kwenye sekta hiyo muhimu.
 Alitaja baadhi ya mambo muhimu kwenye kampeni hiyo ambayo yatatekelezwa kwa awamu kuwa ni pamoja na Mafunzo kwa vijana kote nchini ili waweze kunufaika na mnyororo wa thamani katika sekta ya utalii ikiwemo kuongoza watalii, mafunzo ya huduma kwa wateja katika hoteli na migahawa, vyombo vya usafiri na ujuzi wa kufungua kampuni za utalii.
"Tunatarajia mafunzo haya yatawanuisha vijana zaidi 100,000 hususani wale wasio na ajira ili waweze kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii na wazitumie vizuri.’’ Alisema Dkt Mukangara huku akiitaja mikoa itakayoanza kunufaika na mpango huo kuwa ni pamoja na mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, Geita, Kagera, Simiyu, Mara na Shinyanga.
Alisema katika kuupamba mkakati huo kutakuwa na uhusishwaji wa matukio mbalimbali ya kimichezo na burudani ili kuvutia walengwa zaidi wa mpango huo. Matukio hayo ni pamoja na mbio za Capital Mountain Run zitakazofanyika katika mikoa mbalimbali hapa nchini , Mdahalo wa Masuala ya Utalii na Uwekezaji Kanda ya Ziwa (Lake Zone Tourism and Investment Symposium utakaofanyika jijini Mwanza.
“Mengine ni pamoja na Tamasha la Mkeka na Mvinyo linalolenga kuhamasisha matumizi ya mvinyo unaozalishwa hapa nchini, Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Marafiki (Buddy Basketball), Tamasha la Muziki  wa dansi linalojulikana kama Bongofest, Mashindano ya Gofu Mufindi, Safari za Kutembelea Vivutio mbalimbali vya utalii kwa Mabalozi na Wakurugenzi wa Makampuni na safari za wanafunzi kwenye vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.’’ alitaja
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) Dkt Costantino Bushungwa alisema chuo hicho kimejipanga kuhakikisha kinawaandaa kitaalamu wadau wa utalii ili waweze kutambua fursa zitokanazo na sekta hiyo muhimu na waweze pia kunufaika.
Nao wadau waliohudhuria uzinduzi huo waliahidi kushirikiana na waratibu wa mpango kuhakikisha unafanyika kikamilifu ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake.
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangalla (Kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mshauri Mkuu wa Mpango mpya wa kukuza utalii wa ndani unaojulikana kama Domestic Tourism Promotion Initiative (DTPI) Dkt Fenella Mukangara wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya wiki. Anaeshuhudia ni  Muwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) Dkt Costantino Bushungwa ambapo chuo hicho ni moja ya wadau wakubwa wa utekelezaji wa mradi huo.
 Mshauri Mkuu wa Mpango mpya wa kukuza utalii wa ndani unaojulikana kama Domestic Tourism Promotion Initiative (DTPI) Dkt Fenella Mukangara akizungumza kwenye hafla hiyo.
 Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) Dkt Costantino Bushungwa akizungumza kuhusu utayari wa chuo hicho katika kutekeleza mpango huo
 Mratibu wa Mpango mpya wa kukuza utalii wa ndani unaojulikana kama Domestic Tourism Promotion Initiative (DTPI) kutoka kampuni ya Real Pr Solutions Bw Samwel Gisayi akizungumza kwenye hafla hiyo.
 Mwakilishi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Bw Hassan Mguluma akizungumza kwa niaba ya wadau mbalimbali wa mradi huo wakati wa hafla hiyo.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangalla (katikati alieketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na waandaaji pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria hafla fupi ya uzinduzi wa Mpango mpya wa kukuza utalii wa ndani unaojulikana kama Domestic Tourism Promotion Initiative (DTPI) iliyofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya wiki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...