
Sehemu ya jengo la Hospitali ya Rufaa ya Mikoa ya kusini inayoendelea na ujenzi.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Gelasius Byakanwa wakikagua ujenzi wa Hospitali mpya ya kanda ya kusini inayojengwa Mkoani Mtwara.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akisikiliza maelezo kutoka kwa msanifu majengo anayesimamia mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kusini wakati alipotembelea Hospitali hiyo kuona hali ya ujenzi.
***********************************
Na. WAJMW-Mtwara
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametembelea ujenzi wa Hospitali mpya ya Rufaa ya Mikoa ya kusini iliyopo mkoani Mtwara na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Hospitali hiyo.
Waziri Ummy ameonekana kuridhidhishwa na ujenzi wa Hospitali hiyo ambao umefikia asilimia 80 na inagharimu Shilingi Bilioni 15.8 mpaka kukamilika kwake.
“Kukamilika kwa Hospitali hii kutasaidia kupunguza rufaa kwa wananchi wa mikoa ya kusini kwenda kutafuta huduma za kibingwa Muhimbili, MOI au JKCI, huduma zote zitakua zinapatikana hapa”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema lengo la Wizara ya Afya ni kuona huduma zinaanza kutolewa katika Hospitali hiyo kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi mwaka huu kwani ilikua ni ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipopita mwaka 2015 kuomba kura na Hospitali hiyo ipo kwenye utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.
“Hatutaki watu wa Mtwara na mikoa ya kusini kwa ujumla muende Dar Es Salaam kwa ajili ya kufuata huduma za CT-Scan, huduma za madaktari bingwa ikiwemo upasuaji wa mifupa, mishipa ya fahamu, Madaktari wa watoto na uzazi. Huduma zote hizi zitapatikana hapa mara baada ya ujenzi wa Hospitali hii kukamilika”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kwa ujumla hali ya sekta ya Afya mkoani Mtwara ni nzuri ambapo katika kipindi cha miaka mitano Hospitali mpya za Wilaya tatu zimejengwa ambazo ni Nanguluwe, Nanyamba pamoja na Masasi. Aidha, vituo vya Afya vinane vimejengwa katika Mkoa huo katika kipindi hicho na kufanya idadi kufikia vituo 23 kutoka 15 wakati Rais Magufuli anaingia madarakani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...