KATIKA mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2020, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) unatarajia kulipa fidia kiasi cha shilingi bilioni 8.5, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Masha Mshomba amesema.

Bw. Mshomba ameyasema hayo katika banda la WCF kwenye maonesho ya 44 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam yanayokwenda na kauli mbiu isemayo “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara endelevu”

“Ujio wa Mfuko wa Fidia umekuwa ni mkombozi, mfanyakazi anaweza kupata ulemavu na asiweze tena kurudi kazini kwahiyo yeye na familia yake wanakuwa ni tegemezi lakini kwa uwepo wa Mfuko, hiyo imekuwa ni historia kwasababu sasa Mfuko unamlipa fidia na hata kwa familia pia pale kwa bahati mbaya inapotokea mfanyakazi amefariki kutokana na kazi.” Alisema Bw. Mshomba.

“Na ieleweke kwamba jukumu kubwa la Mfuko ni kulipa fidia kwa Mfanyakazi aliyepata ulemavu utokanao na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kwa mujibu wa mikataba ya ajira na katika hili ulipaji wa Mafao ya fidia tumepiga hatua kubwa sana kwani katika mwaka wa kwanza tangu tuanze kulipa fidia Julai 1, 2016, tulilipa shilingi bilioni 1.5 na katika mwaka huu wa fedha ulioisha Juni 30, 2020 Mfuko unatarajia kulipa jumla ya shilingi bilioni 8.5.” Alibainisha Bw. Mshomba.

Alisema, sambamba na kulipa fidia Mfuko pia umeweka mkazo kwenye suala la elimu kwa wadau wa Mfuko wakiwemo waajiri, wafanyakazi lakini pia madaktari na watoa huduma wengine wa afya.

Akifafanua zaidi alisema, waajiri na wafanyakazi pamoja na mambo mengine wamekuwa wakifundishwa kuzingatia sheria ya Usalana na Afya Mahali pa kazi(OSH) ili hatimaye kupunguza ajali au magonjwa yatokanayo na kazi.

‘’Kundi lingine muhimu katika kuhakikisha Mfuko unatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa haki ni madaktari na watoa huduma ya afya.

Tumetoa mafunzo kwa madaktari na watoa huduma ya afya wapatao 1,064 nchi nzima kuhusu namna ya kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi (Assessment of occupational injuries and diseases) ili hatimaye mfuko uweze kutoa fidia stahiki na kwa wakati.” Alisema.

Bw. Mshomba alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutimiza ndoto yake ya kuona nchi inafika katika uchumi wa kati.

“Mlimsikia Mhe. Rais wakati akifunga bunge hivi karibuni, alitoa tathmini ya viwanda nchini na kusema kumekuwepo na ongezeko kubwa la viwanda na sisi kama Mfuko tunao wajibu mkubwa wa  kuhakikisha tunalinda nguvu kazi ya nchi kwa kuwahudumia wafanyakazi walioko viwandani ili waweze kurudi kazini haraka na hata wale waliopata ulemavu pengine warudi katika kazi zao au kazi zingine mbadala na kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetimiza lile jukumu la kusaidia kukuza uzalishaji viwandani na hivyo kupelekea uchumi kukua.” Alifafanua Bw. Mshomba.

Kuhusu maonesho hayo ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema, yametoa fursa ya kuendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya Fidia, kama kauli mbiu inavyosema, hapa ndio mahala pake hasa kwa Mfuko kukutana na wadau wake muhimu, yaani waajiri na wafanyakazi.

“Sabasaba imekuwa nzuri sana kwakweli tumepata wageni wengi katika banda letu na kama kawaida imekuwa ni sehemu nzuri sana ya kuelezea huduma zetu pia nafasi nzuri ya kuelezea mchango wetu katika serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt.John Pombe Joseph Magufuli.”Alisema.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Masha Mshomba (aliyesimama) akimsikiliza mwananchi huyu aliyefika kwenye banda la Mfuko huo katika viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba ili kupata huduma. Anayemuhudumia ni Afisa Matekelezo Mwandamizi wa Mfuko Bi. Melinda Matinyi.
 Muonekano wa banda la WCF Sabasaba
Bw. Mshomba (katikati) akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge (kushoto) wakimsikiliza kwa makini afisa huyu wa Mfuko.
 Bi. Melinda akimsikiliza mteja
 Afisa Mwandamizi wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSH), Bi. Tumaini Kyando (kushoto) akitoa elimu kuhusu OSH na shughuli za Mfuko kwa ujumla wake.
 Afisa msaidizi wa Madaina Tathmini WCF, Dkt. Brian (kushoto) akimsikiliza mwananchi huyu aliyefika katika banda la Mfuko kupata huduma. 
 Afisa Mwandamizi wa Madai, WCF, Bw. Silvanus Kulosha (kushoto) akimfafanulia kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo shughuli za Mfuko mwananchi aliyetembelea banda la WCF.
 Afisa Mwandamizi wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSH), Bi. Tumaini Kyando (kushoto) akitoa elimu kuhusu OSH na shughuli za Mfuko kwa ujumla wake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...