Veronica Simba – Kilimanjaro
Waziri
wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), kuanza kuwakatia umeme wateja wake wenye madeni sugu nchi
nzima, ifikapo Agosti 31, mwaka huu.
Alitoa maelekezo hayo akiwa
katika ziara ya kazi wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 17, 2020
kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme ambapo pia aliwasha umeme katika
taasisi za umma na makazi ya wananchi.
Alisema TANESCO inadai
zaidi ya shilingi bilioni 300 kutoka kwa Mashirika hasa ya Umma,
Halmashauri, Sekta ya Afya, Mambo ya Ndani, Maji, Ulinzi na nyingine
nyingi.
“Natoa siku 14 kuanzia sasa kwa Taasisi zote zinazodaiwa
zikiwemo za Umma, zilipe, zisipolipa tutakata umeme, tena bila huruma
wala taarifa nyingine yoyote. Taarifa ndiyo hii,” alisisitiza.
Akielezea
sababu za kufikia uamuzi huo, Waziri Kalemani alisema Shirika hilo
linajiendesha kibiashara pasipo kupata ruzuku serikalini, hivyo
malimbikizo ya madeni ya wateja yanahatarisha uhai wake.
Alieleza
baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa na Shirika hilo kwa kutumia
fedha za ndani kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kupeleka gridi
ya Taifa mkoani Kigoma pamoja na kusambaza miundombinu mingine katika
vijiji na mitaa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
“Kwahiyo
ni lazima tuwe na vyanzo vya uhakika vya ndani ambavyo pamoja na mambo
mengine, ni kwa wateja wetu kutulipa kwa wakati.”
Aidha, Dkt
Kalemani alitahadharisha kuwa wakati wa utekelezaji wa suala hilo,
asipigiwe simu na wadaiwa zenye mlengo wa kumsihi kusitisha kutokana na
sababu ambayo hutolewa na wengi kuwa taasisi zao ni muhimu hivyo
zisikatiwe umeme. Alisisitiza kuwa badala ya kupiga simu, wadaiwa walipe
ankara zao.
Katika hatua nyingine, akizungumza na Mkuu wa Mkoa
wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Waziri alimweleza kuwa Mkoa huo una umeme
mwingi ikilinganishwa na mahitaji yake.
Alisema kuwa Mkoa una
zaidi ya megawati 110 za umeme wakati matumizi yake ni megawati 45 hadi
48, hali inayoufanya kuwa na ziada kubwa kuliko mahitaji.
Aidha,
alieleza kuwa kwa sasa Serikali kupitia Wizara yake, inafuatilia
utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini inayoendelea, ambayo ni REA II
na REA III.
Alisema ameunda kikosi kazi maalumu kinachojumuisha
wataalamu kutoka wizarani, TANESCO Makao Makuu na REA Makao Makuu,
kitakachowajibika kuhakikisha Miradi hiyo ya umeme inakamilika ifikapo
Septemba 15, 2020.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa alipongeza kazi
kubwa inayofanywa na Wizara lakini akaomba kusimikwa kwa nguzo za umeme
zilizo imara zaidi, hususan katika maeneo ya milima ambako kuna upepo
mkali, ili ziweze kuhimili hali hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Siha, Onesmo Buswelu, alisema Wilaya yake ina deni kwa Rais John
Magufuli ambalo inawiwa kulilipa kutokana na kuwajali wananchi hao kwa
kuendelea kuwapigania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo
umeme.
Katika ziara hiyo, Waziri alifuatana na Kaimu Kamishna wa
Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji
wa TANESCO Dkt Tito Mwinuka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos
Maganga pamoja na Wataalamu wengine mbalimbali kutoka Wizarani na
katika Taasisi hizo.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akitoa hamasa kwa wananchi wa Kitongoji cha Lasawana, kijiji cha Lokili, Kata ya Kashashi, wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, waige mfano wa Mzee Abrahamu Kileo (mwenye kofia ya njano), kwa kulipia shilingi 27,000 tu ili waunganishiwe umeme. Waziri aliwasha rasmi umeme katika nyumba ya Mzee huyo akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 17, 2020.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...