Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ametengua nafasi ya Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Pwani na Lindi kutokana na kutoridhishwa na usimamizi na ufuatiliaji wa matumizi ya barabara ya Dar es Salaam - Kilwa - Lindi hadi Mingoyo yenye urefu takriban kilometa 450.

Aidha, ameagiza Mameneja wapya wa mikoa hiyo na mameneja wa mikoa mingine kuhakikisha wanaziba mashimo yote yaliyopo kwenye barabara zao ndani ya saa 48 kuanzia muda wa shimo hilo linapojitokeza.

 Mhandisi Kamwelwe, ametoa agizo hilo akiwa mkoani Lindi  ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, baada ya kutoridhishwa na hali ya miundombinu ya barabara kuanzia Nangurukuru hadi Mbwemkuru wakati alipoikagua barabara hiyo siku chache zilizopita ambapo pamoja na mambo mengine amesema kuwa hadi sasa bilioni 10 zimeshatengwa kwa ajili ya zoezi la kuziba mashimo yote kabla hayajaleta athari zingine.

 "Nimetengua nafasi za watendaji hawa wawili kwa makosa yaliyojitokeza katika barabara hizi zinazounganisha mkoa kwa mkoa na hadi kufikia mwishoni mwa mwezi  huu nahitaji wananchi wawe wanapita salama katika barabara hii", amesema Waziri Kamwelwe.

 Waziri huyo ameeleza kuwa sehemu kubwa ya barabara iliyoathirika ni kuanzia eneo la Muhoro mkoani Pwani hadi Mbwemkuru  mkoani Lindi yenye jumla ya urefu wa kilometa 190 na zote zipo katika utaratibu wa kuanza kukarabatiwa.

 Waziri Kamwelwe amebainisha kuwa ataendelea kusimamia muongozo wake alioutoa mwezi Juni mwaka huu kuwa barabara yoyote yenye mashimo katika barabara kuu na za mikoa basi huyo Mhandisi wa Mkoa ajiondoe mapema kwani hayuko tayari kufanya kazi na wataalamu wasio weledi na kushindwa kusimamia rasilimali fedha na watu vizuri.

 Ameongeza kuwa hadi sasa Serikali imeshatoa kiasi cha fedha bilioni 40 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zote nchini zilizoathriwa na maji ya mvua.

 "Fedha zipo sasa sitarajii kuona barabara yoyote hapa nchini ina mashimo, huyo Meneja ambaye barabara zake zina mashimo tutamalizana hapo hapo", amesisitiza Mhandisi Kamwelwe.

 

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akitoka kukagua mzani wa Nangurukuru uliopo mkoani Lindi wakati alipowasili mkoani humo kwa ajili ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli  baada ya kukagua barabara ya kutokea Lindi hadi Dar es Salaam na kutoridhishwa na hali ya miundombinu ya barabara hiyo.

 

Naibu waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa,  akitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi Arch. Elius Mwakalinga, kuhusu ukarabati wa sehemu iliyoharibiwa na malori ya mizigo ya mawe katika barabara ya Mtwara - Lindi - Dar es Salaam.

 

Viongozi na Wataalam kutoka wizara ya Ujenzi,uchukuzi na mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), wakisikiliza maelezo kutoka kwa wasafirishaji wa mawe katika eneo la Kilanjelanje mkoani Lindi tayari kwaajili ya kusafirishwa kuelekea jijini Dar es Salaam.

 

Muonekano wa sehemu ya barabara iliyoharibika kutokana usafirishaji wa mizigo kwa wingi baada ya ongezeko kubwa la magari ya mizigo yanayotumia barabara hiyo ya Lindi – Dar es Salaam na kupelekea kuharibu miundombinu ya barabara hiyo.

 

Lori la mizigo likipakia mawe katika eneo la Kilanjelanje mkoani Lindi tayari kwaajili ya kusafirishwa kuelekea jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...