Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah(katikati) akiongea na Waandishi wa habari (hawapo pichani) alipotembelea na kukagua ukarabati wa kiwanda cha Alpha Tanganyika Flavour kilichopo Mkoani Rukwa mapema leo Agosti 13, 2020. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji, Alpha Tanganyika Flavour Ltd, Alpha Nondo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi(WMUV), Stephen Lukanga.
 Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi, Stephen Lukanga(katikati aliyenyoosha mkono) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji, Alpha Tanganyika Flavour Ltd, Alpha Nondo(hayupo pichani) katika Ziara ya Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya kukagua ukarabati wa Kiwanda cha Alpha  kilichopo Mkoani Rukwa leo Agosti 13, 2020. Kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah. Wengine kutoka kulia ni Afisa Uvuvi Mkuu, Idara ya Uvuvi(WMUV), Melkizedeck Koddu, wa pili kutoka kulia ni Afisa Uvuvi Mkuu Msaidizi, Kikosi cha Doria- Kanda ya Kusini-Tanganyika, Juma Makongoro, na wanne kutoka kulia ni Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Rukwa, Ocrani Chengula.
 Mkurugenzi Mtendaji, Alpha Tanganyika Flavour, Alpha Nondo(kulia aliyenyoosha Mkono) akimuonesha Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah(aliyekaa) namna kiwanda cha Alpha cha kuchakata Samaki kitavyokuwa kinaonekana baada ya kukamilika kwa ukarabati wake alipotembelea kukagua ukarabati unaoendelea wa kiwanda hicho kilichopo Mkoani  Rukwa mapema leo Agosti 13, 2020. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi(WMUV), Stephen Lukanga.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah(wa nne kutoka kushoto, aliyevaa koti jeusi), akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, Alpha Tanganyika Flavour, Alpha Nondo(aliyevaa T-shirt ya njano) alipotembelea kiwanda cha Alpha kilichopo Mkoani Rukwa kukagua ukarabati wake unaoendelea leo Agosti 13, 2020. Wengine pichani ni Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Maafisa wa Kampuni ya Alpha Tanganyika Flavour.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alipofanya ziara Mkoani Rukwa mwaka jana, moja ya maelekezo yake kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha kuwa katika Mkoa huo kunaanzishwa kiwanda cha kuchakata samaki ili kuwasaidia wavuvi wa maeneo hayo kupata soko la uhakika kwa samaki wao.

Kufuatia agizo hilo, Kampuni ya Alpha Tanganyika Flavour  kupitia ushirikiano mkubwa kutoka kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wameweza kufanya uwekezaji katika sekta hiyo ya uvuvi kwa kuanzisha kiwanda cha kuchakata samaki ambacho kwa sasa kinamalizia ukarabati wake kabla ya kuanza kazi mwishoni mwa mwezi wa tisa, mwaka huu.

Hayo yalifahamika, baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah alipofanya ziara ya kukagua ukarabati wa kiwanda hicho cha kuchakata samaki cha Alpha Tanganyika Flavour  kilichopo Wilayani Sumbawanga, Mkoani Rukwa Agosti 13, 2020.

Akiwa katika kiwanda hicho, Dkt. Tamatamah alisema kuwa Rais Magufuli alipofanya ziara yake mwaka jana katika mkoa huo moja ya maelekezo yake kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha kuwa katika Mkoa huo kunaanzishwa kiwanda cha kuchakata samaki ili kuwaondolea kadhia ya masoko wanayoipata wavuvi wa maeneo hayo na mikoa ya jirani.

"Leo nimekuja na wataalamu wangu kukagua ukarabati unaoendelea katika kiwanda hiki cha Alpha ambapo ukikamilika na kiwanda hiki kuanza kazi kitatoa ajira zaidi ya mia moja(100) kwa wananchi na vile vile kitachangia kuongeza mapato ya Serikali," Amesema Dkt. Tamatamah

Dkt. Tamatamah aliendelea kueleza kuwa kiwanda hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuchakata Tani 20 za samaki ambazo bidhaa zake zitauzwa ndani ya Tanzania na vile vile katika soko la Marekani, hivyo kitasaidia nchi kupata fedha za kigeni.

Aidha, Dkt. Tamatamah alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ya Alpha Tanganyika Flavour, Alpha Nondo kwa kuamua kufanya uwekezaji huo mkubwa ambao unatekeleza kwa vitendo agizo la Rais Magufuli huku akimuahidi kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kumpatia  ushirikiano utakaohitajika ili kumuwezesha kufikia adhma yake ya kuwekeza kiwanda hicho mkoani humo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji, Alpha Tanganyika Flavour, Alpha Nondo aliishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa wanaompatia huku akisema kiwanda hicho kitakuwa ni jibu kwa Rais Magufuli na Wavuvi waliokuwa wanahangaika na soko la kupeleka samaki wao.

"Kiwanda cha Alpha kinakuja kumkomboa mvuvi aliyekuwa hana uhakika na soko la samaki wake, hivyo nawaomba wavuvi na wananchi wote kutupa ushirikiano ili kiwanda hiki tunachoenda kukianzisha kiweze kuwahudumia vizuri." Amesema Nondo.

Naye, Katibu Tawala Msaidizi, Mkoani Rukwa, Ocrani Chengula alisema kuwa kwa muda mrefu Mkoa huo ulikuwa unahangaika kupata kiwanda cha kuchakata samaki ili kiweze kuwasaidia wavuvi kupata masoko ya uhakika na kuachana na kufanya biashara ya kutorosha samaki kiholela katika nchi za jirani.

"Tunaamini kuanzishwa kwa Kiwanda hiki kwanza kitatoa ajira kwa watu wetu hapa, lakini vile vile kitatuongezea mapato katika Halmashauri yetu na pia Wavuvi wetu wataachana na uuzaji holela wa samaki wao kwa sababu soko la uhakika litakuwa limepatikana kupitia Kiwanda hiki." Amesema Chengula

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...