Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MKURUGENZI Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania( TFCG) Emmanuel Lyimo amesema wao na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kupitia Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswiss (SDC) wamefanikiwa kuchochea mabadiliko makubwa ya kijamii, kiuchumi na maendeleo katika vijijini 35.

Amesisitiza kwamba sekta ya misitu imekuwa   na mchango mkubwa kwa jamii ambazo zinazingatia dhana ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya jamii( USMJ) lakini bado taarifa sahihi hazijafikia kundi kubwa hapa nchini, hivyo ameomba vyombo vya habari kuandika na kuchambua habari za uhifadhi wa misitu na faida za kiuchumi, kijamii.

Akifafanua zaidi wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini kuhusu umuhimu na faida ya USMJ kiuchumi, kijamii na maendeleo kwa ujumla amesema rasilimali misitu inaweza kuonekana umuhimu wake iwapo jamii inayozunguka itanufaika na waandishi wa habari ndio watu wa kuonesha matokeo chanya.

"Tunatoa mafunzo haya kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa kuandika kwa kina namna uhifadhi ulivyo na faida za kiuchumi, kijamii na maendeleo pale misingi muhimu inavyoguaswa," amesema Lyimo

Amefafanu kuwa ipo dhana kwamba ukataji misitu kwa ajili ya mkaa ndio sababu ya uharibifu lakini ukweli shughuli za kilimo ndio chanzo kikuu cha uharibifu na hilo linaweza kuoneshwa na waandishi wa habari kupitia kalamu zao huku akieleza TFCG na MJUMITA wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi kuhusu njia nzuri ya kutumia rasilimali misitu bila kuharibu mazingira.

"Baada ya miaka takribani nane ya kuwajengea uwezo vijiji takribani 35 kwa sasa wanajikita katika ngazi ya wilaya ili ziweze kusambaza dhana hiyo muhimu katika uhifadhi,"amesema Lyimo.

Wakati huo huo Ofisa Sera na Majadiliano wa MJUMITA, Elida Fundi ameongeza mafunzo hayo yanawajengea uwezo waandishi namna ya kubaini changamoto zilizopo katika vijiji vya mradi na kuja na mapendekezo.

"Uhifadhi wa misitu endelevu unahitaji kila mdau kushiriki hivyo imani yao ni kupitia kundi hilo la waandishi ujumbe utafika kwa usahihi.

Takwimu zinaonesha uharibifu wa misitu na mazingira unaendelea kwa kasi, hivyo elimu inapaswa kutolewa kwa wadau wote ili kuokoa rasilimali hiyo muhimu kwa viumbe hai,"
amesema.

Amefafanua takwimu zinaonesha kwa mwaka hekta 469,000 zinapotea na hiyo ni sawa na Kisiwa cha Unguja, hivyo sio jambo la kufumbia macho ili kunusuru misitu.

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa TFCG Bettie Luwuge amesema kwa sasa wanatekeleza Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu Tanzania (CoForEST) ambao utahusisha wilaya saba.

Hivyo mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yamejikita katika kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu namna bora ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira na misitu.

"Mradi huu wa CoForEST ni mwendelezo wa mradi wa TTCS, ila tofauti yake ni huu wa sasa unajikita kuendeleza USMJ kwa kushirikisha sekta zote kwa maslahi ya uhifadhi," amesema.

Alitaja wilaya ambazo zitanufaika na mradi huo mpya ni Kilolo, Liwale Nachingwea, Ruangwa, Morogoro, Kilosa na Mvomero.
 Ofisa Uhusiano wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania( TFCG) Bettie Luwuge akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo
 Ofisa Sera na Majadiliano wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania Elida Fundi akitoa mada kuhusu umuhimu wa usimamizi shirikishi wa misitu kwa waandishi wa habari
Waandishi wa habari wakiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Shirika la Kuhifadhi ya Misitu Asili Tanzania( TFSG)pamoja na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu yaTanzania(MJUMITA) wakati wa mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu usimamizi shirikishi wa misitu nchini
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...