Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa akisisitiza jambo wakati alipotembelea banda la TRA katika viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu. Wakwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka.
 Wazee wakipatiwa elimu kuhusu msamaha wa kodi ya majengo kwa wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60

Delina Lema, Afisa Msimamizi wa Kodi akimkabidhi mfanyabiashara cheti cha Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) baada ya kumsajili
 Anthony Faustin Afisa, Msimamizi wa Kodi, akitoa elimu wakati wa maonesho ya Naenane
 Afisa Msimamzi wa Kodi  wa TRA, Delina Lema (kulia) akimkabidhi mwananchi leseni ya udereva wakati wa maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nyakabidi Simiyu.
 Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka (kulia) wakimkisikiliza Afisa Msimamizi wa Kodi Lameck Ndinda akitoa maelezo kuusu huduma ambazo TRA inazitoa kwa wananchi wanaotembelea banda la TRA.





Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuendelea kukusanya mapato ya serikali kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Bashungwa ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la (TRA) kujionea shughuli na huduma ambazo TRA inazifanya katika Maonesho ya Nanenane ambayo yanafanyika Kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.

“Nawapongeza sana TRA mnafanya kazi nzuri sana ya kukusanya mapato na mnashirikiana vizuri na Wizara ya Viwanda na Biashara”, alisema Mhe. Bashungwa.
Pamoja na pongezi hizo, Waziri Bashungwa ameitaka TRA kuwasimamia vizuri wasambazaji wa mashine za kielektroni za kodi (EFD) kwa kuondoa kero ya kufutika kwa karatasi za mashine za hizo.

Aidha ameishauri TRA kuendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi kufanya biashara ili mapato ya nchi yaongezeke.
Mamlaka ya Mapato Tanzania ikiwa ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazoshiriki maonesho ya Nanene inatoa elimu na huduma mbalimbali katika viwanja vya maoenesho ambapo kati ya huduma zinazotolewa ni pamoja na kutoa leseni za udereva kwa waombaji wapya na wale ambao leseni zimeisha muda wake huduma ambayo imekuwa kivutio kwa washiriki wa maonesho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupokea leseni zao za udereva, baadhi ya wenye leseni wameipongeza TRA kwa uamuzi wa kutoa huduma hiyo ambayo inapatikana kwa urahisi na haraka.
“Sikutegemea kama nitapata leseni yangu haraka namna hii. Kwa kweli nawapongeza sana”, amesema Rayner Nicholause ambaye ni mkazi wa Dodoma.
Naye Andes Seiya mkazi wa Arusha amesema kwamba huduma ni nzuri kwani amepata leseni yake ndani ya siku moja baada ya kulipia. “Tunaomba huduma hii iboreshwe huko mikoani kwani kama imewezekana hapa katika maonyesho kwanini cihukue muda mrefu kupata leseni ya udereva katika ofisi za TRA?” alisema Seiya.
Kwa upande wake Nelson Mnyanyi ambaye ni Mkazi wa Dar es Salaam amesifu utoaji wa huduma katika banda la TRA na kusema kwamba ni huduma bora na zinatolewa  haraka na hivyo kuokoa muda. “Baada ya kupata taarifa kwamba leseni yangu ipo tayari nifike niichukue baada ya kulipia sikuamini. Nawashukuru na nawapongeza sana”, alisema Mnyanyi.
Mbali na kutoa leseni za udereva, huduma nyingine ambazo TRA inazitoa katika maonesho ya Nanenane ni pamoja na kutoa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa wafanyabiashara na watu binafsi, kutoa ankara za Kodi ya Majengo, kutoa elimu ya kodi katika shughuli za kilimo na elimu ya kodi kwa ujumla.
Aidha huduma nyingine ni kutoa maelezo ya fursa za masomo ambazo zinapatikana katika Chuo cha Kodi (ITA) ambacho kinamilikwa na TRA pamoja na namna ya kutuma maombi katika chuo hicho.
Maonesho ya Nanenane yenye kauli mbiu, ‘Kwa Maendeleo ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi Chagua Viongozi Bora’, yanafanyika katika viwanja vya Nyakabindi Wilaya ya Bariadi katika Mkoa wa Simiyu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...