Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila
imefungua mafunzo ya wiki moja kwa washiriki 25 wa kada mbalimbali yanayolenga
kuwapa ujuzi wa mbinu za utafiti ili kuboresha utoaji huduma za afya kwa
watanzania.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema kuwa uongozi wa hospitali ya
Muhimbili Upanga na Mloganzila unaunga mkono mafunzo ya wataalamu mahali pa
kazi kwani yatasaidia kuboresha utoaji huduma.
“Napenda kusisitiza kuwa bodi ya
wadhamini na uongozi wa MNH tunaunga mkono ufanyaji wa tafiti hizi kwa maslahi
mapana ya taifa letu na maboresho ya utoaji huduma za afya katika hospitali
yetu.” Amesema Dkt. Magandi.
Sambamba na hilo Dkt. Magandi ameeleza
kuwa ili kuweza kufikia mapinduzi makubwa katika sekta ya afya hatuna budi
kujikita katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali kama ilivyo katika nchi
zilizoendelea kama vile Marekani, Uingereza, China na Afrika ya Kusini ambazo
ni baadhi tu ya nchi zinazofanya tafiti nyingi na kuleta matokeo chanya katika
sekta ya afya.
Aidha Dkt. Magandi ametaja moja ya faida
za utafiti kuwa ni pamoja na kuwasaidia watafiti na wataalamu wa afya katika
kada zote kupata njia mpya na sahihi za kuelewa, kugundua, kudhibiti na kutibu
maradhi mbalimbali ya binadamu.
Mafunzo hayo yataendeshwa
na wataalamu bobezi katika tafiti za afya kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili- MUHAS kwa kusimamiwa na Kitengo cha Elimu, Utafiti na
Ushauri wa Kitaalamu MNH-Mloganzila
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akizungumza
wakati wa kufungua mafunzo ya wiki moja ya mbinu za utafiti kwa wataalamu wa
kada mbalimbali yaliyofanyika hospitalini hapa.
Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo
kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi SAhirikishi Muhimbili-MUHAS, Prof. Method
Kazaura akiwasilisha mada.
Wataalamu wakifuatilia kwa makini mada
katika mafunzo hayo.
Dkt. Magandi katika picha ya pamoja na
washiriki wa mafunzo hayo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...