Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Kasulu


MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amewahidi maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kuwa jumla ya Sh.bilioni 402 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika mkoa huo ikiwemo kutoka eneo hilo hadi Afrika Kusini.


Pia Dk.Magufuli amesisitiza mkakati uliopo ni kuufungua Mkoa wa Kigoma kiuchumi kwa kuunganisha na nchi nyingine zaidi ya tano na lengo ni kuwawezesha wafanyabiashara wanakuwa na uwanja mpana wa kufanya shughuli zao za biashara kati ya Wilaya hiyo, mkoa na nchi nyingine.


Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi hao leo Septemba 17, 2020, Dk.Magufuli amefafanua kiasi hicho cha fedha Sh.bilioni ndizo zitatumika kujenga barabara itakayounganisha nchi za Sudani Kusini, Uganda kupitia Kagera, Nyakanazi hadi Kigoma kisha kuendelea hadi Tunduma kupitia Malawi, Zambia, Zimbabwe hadi Afrika Kusini.


Amesema barabara hiyo ambayo itakuwa ya kimataifa itakapokamilika kwa kiwango cha lami, magari makubwa ambayo yatakuwa yakitokea nchi ya Sudan Kusini yatakuwa yakipita katika Mkoa Kigoma huo.


Hivyo amesema amefika tena kwao kwa ajili ya kuwaomba ridhaa ya miaka mitano mingine ili aendelee kuleta maendeleo ya Mkoa huo kwani kupitia Ilani ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 imefafanua vizuri zaidi mambo makubwa yanayokwenda kufanyika katika Wilaya ya Kasulu na Mkoa huo kwa ujumla.


Amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Kasulu kwamba hatawaangusha. "Yote ambayo nimesema mbele yenu yote yapo kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu.Pia tutaendelea kutoa elimu  bure, kujenga vituo vya afya na kuleta dawa,"amesema Dk.Magufuli na kusisitiza katika nishati ya umeme vijiji wataendelea kuweka vijiji ambavyo vimebakia.


Ameongeza kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita wamefanikiwa kutekeleza yale waliyoahidi wananchi wa Kasulu na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla."Tuliahidi kusimamia hali ya ulinzi na usalama, tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.Najua kuna mengi yamefanyika na mengine bado, hivyo tupeni nafasi tukamalizie yote tuliyoanza kuyafanya.Mkinipa tena miaka mitano nifanya zaidi."


Akizungumza zaidi kuhusu barabara katika Wilaya ya Kasulu, Dk.Magufuli amesema barabara zinaendelea kujengwa ikiwemo ya barabara ya Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilometa 68 pamoa na barabara ya Buhigwe hadi Kasulu.


Wakati kwa Kasulu mjini amesema kilometa tano za barabara za lami zitajengwa na kuweka taa za barabarani huku akiahidi kuwa wanataka kuhakikisha wanamaliza matatizo yote yanayowakabili wananchi."Barabara ya Nyakanazi hadi Kakonko yenye urefu wa kilometa 50 tulianza nazo na tukaongeza nyingine kilometa 68.


"Nataka kuwahakikishia mipango tuliyoipanga kwa ajili ya Kasulu tunaifanya na tutaendelea kuifanya,"amesema Dk.Magufuli na kuahidi kuendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.


 Wakati huo huo Dk.Magufuli amewaambia wananchi hao mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kupitia majina ya wagombea walishaumaliza na ndio maana leo wako mbele ya wananchi wakiomba ridhaa. "Mchakato tulishaumaliza ndio mana mnawaona waliopata na waliokosa wapo hapa."



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...