Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Iringa
MGOMBEA urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli amehutubia maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Iringa huku akitumia mkutano huo kuelezea kwa kina mambo makubwa ya maendeleo yanayokwenda kufanyika nchini katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ametumia nafasi hiyo kufaanua hatua kwa hatua kuhusu Ilani ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 ya Chama hichoa ambapo amesoma kurasa kwa kurasa yale ambayo yanakwenda kufanyika iwapo yeye na Chama chake watapata ridhaa ya watanzania kwa kuwachagua tena kwa ajili ya kuendelea na yale ambayo wameyafanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza kuna mambo mengi ambayo yamefanyika licha ya kutowekupo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya 2015 hadi 2020.
Akizungumza leo Septemba 28 mwaka huu 2020 mbele ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Iringa Dk.Magufuli ameamua kujikita zaidi katika kueleza yatakayofanyika kwa kupitia kila kurasa ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu na kusisitiza kuwa huu ni wakati wa kujenga Tanzania mpya ambayo itajitegemea katika kuleta maendeleo yake.
"Ni matumaini yangu yale ambayo tutazungumza leo yatafanikiwa kwa maslahi ya vizazi na vizazi vya wana Iringa na Watanzania.Nawapongeza kwa kujitokeza kwa wingi, wakati naingia Iringa nimekutana na umati mkubwa, wapo ambao nimewasalimu, na wengine nimeshindwa, sikutegemea kukutana a watu wengi hapa Samora lakini nimefika hapa nimekuta mafuriko, hii inaonesha mwaka huu Iringa mna jambo lenu.
"Ndugu zangu mwaka 2015 nilikuja kuomba kura mkanianimini, mkanichagua kuwa Rais, nakishukuru Chama changu kwa kuniteua kupeperusha bendera na mwaka huu tena kupitia Mkutano Mkuu wameniteua nije kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi.Wamenikabidhi kitabu cha Ilani chenye kurasa 303 ili yaliyomo humu nikayatekeleze.
"Nieleze mafanikio machache kwa hapa Iringa kuna maendeleo makubwa tumefanya katika kipindi cha miaka mitano, tujenga hospitali tatu za Wilaya, vituo vya afya vitano, na zahanati 23.Kwa upande wa elimu tumetumia Sh.bilioni 33.74 kwa ajili ya elimu bila malipo.Pia tumefanya upanuzi wa Chuo Kikuu Mkwawa pamoja na vyuo vingine vya hapa Iringa tumevifanyia maboresho ya miundombinu yake.tumejenga shule, mabweni, nyumba za walimu,"amesema Dk.Magufuli.
Amewaambia wananchi hao kuwa ni mashahidi katika eneo la maji kwani wametekeleza miradi ya maji 43, ambayo imetumia Sh.bilioni 20.3.Pia kuna miradi mingine ya maji 70 ambayo utekelezaji wake uko hatua mbalimbali na kiasi cha fedha Sh.bilioni 22.94 zinatumika.
"Upatikanaji wa maji umefikia asilimia 72, kutoka asilimia 66.Kuhusu umeme vijiji 242 katika Mkoa wa Iringa vimewekwa umeme na vimebakia vijiji 37 tu na katika nchi nzima vijiji 9700 vimepatiwa umeme na vimebakia vimebaki 2,500.Tunawoamba wana Iringa mtupe tena miaka mitano, tutahakikisha ndani ya mwaka mmoja tutakuwa tumefunika vijiji vilivyobakia, ndio maana tumekuja tena kuomba ridhaa yenu tukamalizie kazi tuliyoanza.
Hata hivyo Dk.Magufuli wakati anafafanua zaidi kuhusu maendeleo ambayo yamefanyika katika kipindi cha miaka mitano, ameeleza yapo mengine ambayo hayakuwepo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015 lakini yamefanyika.
"Nilipokuja kuomba kura kuna mambo hayakuwepo lakini tumefanya , hakukua na ununuzi wa ndege 11 mpya lakini tumenunua. Hakukua na ujenzi w bwawa la umeme la Julius Nyerere leo ujenzi unaendelea.
"Hatukuwa na ujenzi wa reli ya kisasa leo ujenzi unaendelea.Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015 haijazungumzia unununuzi wa meli tano na kukatabati nyingine zilizopo lakini tumenunua na kukarabati meli.Nataka mtuamini tutafanya zaidi ya yale ambayo yamekuwepo kwenye Ilani.
"Kwa Iringa tutaendelea kuboreha miundombinu ya barabara na tutaupanua uwanja wa ndege wa Nduli ili ndege kubwa ziwe zinatua. Tunataka ndege kubwa ziwe zinatua, tunataka tuitangaze Hifadhi ya Taifa ya Ruaha liwe eneo la utalii.Tunataka kuufanya Mkoa wa Iringa kuwa eneo la utalii,"amesema Dk.Magufuli.
Pamoja na hayo Dk.Magufuli wakati akielezea ambayo yamefanyika kwa kipindi cha miaka mitano amesema atajikita zaidi kuelezea Ilani ya CCM."Najua mnanisikiliza , nataka mjue kwa kifupi ambayo tumepanga kufanya, sura ya kwanza ya Ilani hii ya Uchaguzi sura ya kwanza hadi ya nane inaelezea utangulizi na hasa misingi ya kulinda uhuru wa nchi, kudumisha amani, umoja na mshikamano, kulinda Muungano pamoja na kulinda Mapinduzi matakatifu ya Zanzibar.
"Ilani pia inaendelea kueleza juhudi za kujenga Taifa ambalo linajitegemea kiuchumi kwa kutegemea rasilimali zetu.Ni ukweli rasimali zilizopo zina uwezo wa kuleta maendeleo ya wananchi, kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.Ndio maana nimekuwa nikizungumza Tanzania ni tajiri, ukiachia mambo haya ambayo yameelezwa vizuri, llani imeeleza mipango ya yale ambayo yamepangwa kufanyika kwa miaka mitano.
"Tumeweka mipango na mikakati ya kuishughuli, ndio maana tunaeleza tutaleta mapinduzi ya maendeleo ya watu kwa maana ya wafanyakazi, wakulima , wavuvi, wajasiriamali na makundi mengine na katika hilo hilo katika sura ya pili inaeleza tutakuza uchumi kwa asilimia nane.
"Miaka mitano iliyipita tumetoka kwenye uchumi masikini hadi kuingia uchumi wa kati. Tumeingia uchumi wa kati wakati nchi nyingine zilikuwa kwenye lockdown.Tumeingia katika uchumi wa kati kipindi hicho licha ya kuwa na Corona, tunamshukuru Mungu wetu, tulikubali kumtanguliza mungu na ametusikia na ndio maana katika ilani hii inatuagiza kama tutachaguliwa , uchumi unakuwa kwa asilimia saba, lakini tunataka ukue kwa asilimia nane,"amesema Dk.Magufuli.
Amefafanua Ilani ndio mkataba kati ya Serikali na wananchi, na kwamba katika miaka mitano ijayo wanatarajia kutengeneza ajira milioni nane, kwani katika miaka mitano iliyopita wametengeneza ajira milioni sita."Kupitia miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ikifanyika ikiwemo ya ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa bwawa la umeme la Julius Nyerere.Tumenunua ndege mpya 11.Hivyo kupitia yote ambayo tumefanya ndio maana tunasema tumetengeneza ajira milioni sita."
Ameongeza kuwa wataendelea kufanya mageuzi ya kuboresha mazingira ya biashara na wataimarisha sekta ya usimamizi wa fedha.Wataanzisha programu maalum na kuhamasisha wanawake na vijana kujiunga katika makundi."Tunataka kuwa na mabilionea wa tanzania, tunataka wawekezaji wa tanzania wawe wengi.
"Tunataka tuwe na akina Asasi wengi, Tanzania itoke kwenye mambo ya kufikiria tutabebwa au kufukiria kuna watu watatueletea fedha. Tanzania ni tajiri na haya yamefafanuliwa vizuri kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu kuanzia ukurasa wa tisa hadi wa 24, kama mnavyofahamu serikali yetu imeanzisha mifuko karibu 24 ambayo ipo kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali.
"Mifuko hiyo yote kwa ajili ya kusaidia wananchi na ndio maana tulianzisha kitambulisho, tutahakikisha wananchi wanaifahamu mifuko hiyo ili waweze kunuifaika nayo.Tutaboresha kila sekta kuhakikisha tunapiga hatua ya maendeleo ya nchi yetu,"amesema Dk.Magufuli.
Amesisitiza kuwa katika miaka mitano ijayo wataendelea na ujenzi wa viwanda kwani ni miongoni mwa sekta muhimu katika kutengeneza uchumi wa nchi na kuinua pato la wananchi."Tunataka kuijenga nchi na haya ndio maagizo yaliyopo katika Ilani ya uchaguzi Mkuu. Tunataka kujenga kanda kwa ajili ya viwanda.
"Miaka mitano iliyopita tulikuwa na mkakati wa kuwa na umeme wa uhakika, umeme wa bei ya chini, tulizoea kuwa na umeme wa majenereta, ndio maana tukaamua kuanzisha mradi wa bwawa la Nyerere ambalo wakati kabla ya kuanza ujenzi tumepigwa vita sana na mabeberu.
"Umeme utakapokuja tutausambaza nchi nchima, tutaupunguza bei kwasababu wa maji ni gharama ya chini. bidhaa ambazo zitatengenezwa zitakuwa chini. Unit ya umeme inayouzwa Tanzania ni mara dufu ya ile ambayo inauzwa Marekani. tunataka kuijenga Tanzania yenye umeme wa uhakika.
"Huwezi kuzungumzia uchumi wa kati wakati hata kusafirisha bidhaa zao huwezi, ndio maana tumeendelea kuboresha miundombinu ya barabara, kufufua reli na kujenga reli ya kisasa itakayokuwa inabeba tani nyingi zaidi. Tunakwenda kwenye uchumi wa kisasa. tunataka Tanzania iwe zaidi ya Ulaya,
"Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 Afrika ambazo uchumi unakwenda kwa kasi, zamani tulikuwa wa mwisho, lakini sasa tunapasua.Ndio maana leo tunayo maduka ya dhahabu, zamani ukishikwa na madini unaambiwa mlanguzi, leo hii hadi akin Laiza wanapata madini.Hata hivyo tumeamua kufufua bandari zetu na Sh.trilioni 1.5 zinatumika,"amesema Dk.Magufuli.
Wakati Dk.Magufuli anazungumza na wananchi hao ameweka wazi jinsi ambavyo Ilani ya CCM imeeleza kwa kina kuhusu maono, mipango na mikakati iliyopo katika kuleta maendeleo ya Watanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...