MJUMBE wa Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa Kondoa waendelee kuwamini viongozi
wanaoletwa na CCM ili walete maendeleo zaidi.
“Endeleeni
kuiamini Serikali hii ili iendelee kuongoza, endeleeni kuwaamini viongozi
wanaoletwa na CCM ili waendelee kuleta maendeleo zaidi. Ninaomba kura za
Mheshimiwa Rais, wabunge na madiwani watarajiwa sababu ndiyo wataleta maendeleo
katika maeneo yenu,” amesema.
Ametoa wito huo
leo (Jumapili, Septemba 13, 2020) wakati akizungumza na wananchi wa Kondoa
Mjini na Vijijini waliofika kusikiliza sera za wagombea kwenye uwanja wa
SabaSaba, wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.
Mheshimiwa
Majaliwa ambaye alifika wilayani humo kumuombea kura Rais Dkt. John Pombe
Magufuli na wagombea ubunge wa Kondoa Mjini, Ally Makoa na Dkt. Ashatu Kijaji
wa Kondoa Vijijini na wagombea udiwani wa CCM, amewataka wananchi hao watumie kipindi
hiki kutafakari kwa kina na kuchagua viongozi wanaowafaa.
“Wananchi
msiyumbe, tuna uchaguzi wa aina mbili. Uchaguzi wa kwanza ni kuchagua kiongozi
anayeweza kuleta maendeleo na mwenye uwezo wa kuleta maendeleo na uchaguzi
wa pili ni uchaguzi wa kishabiki wa kufuata upepo. Tutumie kipindi hiki
kichagua viongozi wanaoweza kutusemea masuala la maendeleo,” amesema.
Akielezea
miundombinu ya barabara, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya Tano
imefanikiwa kuunganisha makao makuu ya mikoa kwa barabara za lami na hata
katika baadhi ya wilaya huku akitolea mfano wa kutoka Babati hadi Kondoa, Kondoa
hadi Chemba na Chemba hadi Dodoma.
“Sasa
hivi tunataka kufungua barabara ya kutoka Babati hadi Orkesumet, na hii ya kutoka
Handeni - Kiberashi – Kondoa – Singida iko kwenye Ilani yetu ya sasa ukurasa wa
73. Barabara hii ikitoka Handeni itapita Kilindi – Kiteto – Kondoa hadi Singida.”
Katika
barabara za wilaya, Mheshimiwa Majaliwa amesema hizo zinashughulikiwa na Wakala
wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ambao wamepatiwa sh. bilioni 1.840
na sh. bilioni 6.4 nyingine zilitolewa kwa ajili ya barabara za Kondoa vijijini
kutoka makao makuu na kuunganisha kata hadi kata.
Kuhusu
mikakati ya Serikali ya awamu ya tano kukuza uchumi, Mheshimiwa Majaliwa
amesema kuna watu wanabeza ujenzi wa reli na ununuzi wa ndege lakini wanasahau
kuwa maendeleo hayaji bila maendeleo ya vitu. “Huwezi kupata maendeleo ya watu
bila kuwa na maendeleo ya vitu,” amesisitiza.
Kwenye
sekta ya kilimo, Mheshimiwa Majaliwa amesema wananchi wa Kondoa ni wakulima
wazuri wa mazao mbalimbali na akawakumbusha wakazi hao jinsi ambavyo Serikali imeboresha
upatikanaji wa mbolea na pembejeo za kilimo.
“Kilimo
ndiyo kinasheheneza mkakati wetu wa uchumi wa viwanda. Na mpaka sasa, tumeshaanzisha
viwanda 8,477 na hapa nasisitiza kuwa viwanda hivi na miradi ya kimkakati vimesaidia
kuongeza ajira hapa nchini.”
“Lazina
niwaeleze ukweli, mkikaa kusubiri ajira rasmi, nafasi ni chache mno. Ukitaka
kazi huko Halmashauri au kwingineko, itabidi usubiri hadi walioko wastaafu.
Ndiyo maana tumeanzisha miradi ya kimkakati ya reli ya Kisasa, mradi wa kufua
umeme wa Mwalimu Nyerere ili wananchi waweze kupata ajira huko.”
“Vijana
wanaojiajiri kwenye ususi, kuchomelea nondo, wafanyabiashara ndogondogo wote
hawa wana ajira. Ajira siyo siyo lazima iwe ile ya kushika kalamu ofisini,”
amesisitiza.
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwahutubia wananchi wa Kondoa, katika mkutano wa kampeni, Septemba 13,
2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi
nakala ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 mgombea ubunge wa CCM wa
jimbo la Kondoa Mjini, Makoa Ally Juma, katika mkutano wa kampeni,
Septemba 13, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi nakala ya Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya 2020-2025 mgombea ubunge wa CCM wa jimbo la Kondoa, Dkt.
Ashatu Kijaji, katika mkutano wa kampeni, Septemba 13, 2020. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...