Mgombea Ubunge Jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, Anthony Mavunde akizungumza na wananchi wa Kata ya Chamwino alipoenda kuomba kura kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 28.
Aliyekua Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Adam Kimbisa (kushoto) akimnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kupitia CCM, Anthony Mavunde leo kwenye kampeni zilizofanyika katika Kata ya Chamwino.
Wanachama na Wafuasi wa CCM Wilaya ya Dodoma waliojitokeza kwenye kampeni za Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, Anthony Mavunde katika kata ya Chamwino.

 Charles James, Michuzi TV

NDIO NAANZA KAZI! Hii ni kauli ya Mgombea Ubunge Jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, Anthony Mavunde ambaye amesema miaka mitano ya kwanza alikua anajifunza kuwatumikia wananchi na sasa ndio anaanza kazi rasmi.

Kauli hiyo ameitoa leo katika mkutano wa kampeni Kata ya Chamwino jijini Dodoma ambapo ametaja vipaumbele vyake ambavyo ataenda kuvitekeleza kwa miaka mitano yake mingine huku akiahidi kumaliza kero ya kudumu ya mtandao wa maji taka kwenye kata hiyo.

Mavunde amesema kwa muda mrefu wananchi wa kata ya Chamwino wamekua wakipata changamoto ya mtandao wa maji taka lakini kupitia jitahada zake kwenye kipindi cha uongozi wake aliwasiliana na Duwasa ambao wameshaanza kuchukua hatua na tayari fedha za mradi huo zimeshatengwa.

Amesema sekta ya elimu ni kipaumbele kingine ambacho anaenda kushughulika nacho kwa nguvu zake zote ndani ya jimbo hilo na kata ya Chamwino ikiwemo huku akiahidi kuhakikisha Shule ya Sekondari Chinangali iliyopo kwenye kata hiyo inapata kidato cha tano na sita.

" Ninaposimama kuomba kura hapa ninamuombea pia Dk John Magufuli ambaye ni mgombea wetu wa Urais, wote tunafahamu mambo makubwa aliyotufanyia ikiwemo kutoa elimu bila malipo, kuboresha miundombinu, kukusanya mapato kwa uadilifu na kukuza uchumi wa Nchi.

Hivyo kwenye sekta ya elimu nitaendelea kumuunga mkono kwa kujenga madarasa na matundu ya vyoo, pamoja na kuchochea matumizi ya teknolojia kwa kuwaletea Kompyuta wanafunzi wetu," Amesema Mavunde.

Amesema ataendelea kuchochea ukuaji wa sanaa na michezo ndani ya Jiji la Dodoma kama alivyowezesha Timu ya Dodoma Jiji FC kupanda daraja na sasa inacheza Ligi Kuu hivyo ataendelea kuwezesha kila mtaa kukua kimichezo na kisanaa ambapo kwenye sanaa tayari amejenga studio ya kisasa inayowahudumia wasanii wote wa Mkoa wa Dodoma.

Mavunde amewaomba wananchi wa Jimbo hilo kumchagua kwa Mara ya pili ili azidi kuwatumikia na kuwawezesha akina Mama, Vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo itakayowawezesha kujikomboa kimaendeleo.

Ameomba wananchi wa Jimbo la Dodoma kumchagua Dk Magufuli kwa mara nyingine kwa sababu chini ya uongozi wake amelifanya jiji hilo na mkoa huo kwa ujumla kupiga hatua za kijamii na kiuchumi.

" Chini ya miaka mitano ya Dk Magufuli Dodoma kama Jiji tunaongoza kwa mtandao wa barabara za lami kuliko sehemu yoyote na tunafuatia na Kinondoni, leo hii Dodoma tuna Soko na Stendi ya kisasa kuliko sehemu zingine na sasa Dk Magufuli anatuletea usafiri wa Treni za ndani, tuna kila sasa za kumchagua kwa wingi Oktoba 28," Amesema Mavunde.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Kuu Mstaafu, Adam Kimbisa ameomba wananchi wa Chamwino kumchagua Dk Magufuli kuwa Rais, Mavunde kuwa mbunge na Jumanne Ndede kuwa Diwani ili waharakishe maendeleo kwa pamoja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...