Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

BARAZA la Ujenzi la Taifa (NCC,) linatarajia kutoa mafunzo ya utatuzi wa migogoro ya kibiashara kwa siku tatu Jijini Dar es Salaam, mafunzo yatakayoanza Septemba 23 hadi 25, mwaka huu kwa kuhusisha makundi yote ya wahandisi na wataalamu wa sekta nyingine nchini waliothibitisha ushiriki wao ndani ya muda uliopangwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa Baraza hilo, Dkt. Matiko Samson Mturi, amesema, mafunzo hayo yataendeshwa na wataalamu wabobezi wa masuala ya sheria na utatuzi wa migogoro ya kibiashara katika hoteli Holiday Inn-Posta jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa  wadau wote wa sekta ya ujenzi,  wahandisi, wakadiriaji majengo, mameneja majengo na miradi, wasanifu majengo, wajenzi, wakaguzi wa viwango pamoja na wataalamu wa sekta nyingine mbalimbali wakiwemo wanasheria, maofisa bima na wanaotoka katika sekta ya usafirishaji majini watakuwa sehemu ya mafunzo hayo.

Amesema washiriki waliotaka kuhudhuria mafunzo hayo kwa kipengele cha kutahiniwa pekee, yaani kufanya mitihani, wameruhusiwa kufanya hivyo kulingana na masharti na vigezo vilivyotolewa na NCC, ambavyo ni kulipa kwa akaunti ya Baraza ya NMB, ada ya Sh. 350,000 kwa mshiriki, tofauti na iliyopaswa kulipwa kwenye akaunti hiyo na  wanaohudhuria mafunzo yote, ambayo ni Sh. 750,000. 

Kwa mujibu wa Dkt. Mturi, ameeleza lengo la mafunzo hayo ni kuandaa watatuzi bora wa migogoro ya kibiashara kwa njia mbalimbali zinazokubalika kisheria, ikiwemo usuluhishi, na kwa kuzingatia sheria na haki pindi watatuapo migogoro  kulingana  na misingi bora watakayofundishwa. 

 “Baraza linaendesha mafunzo haya kwa mara ya 14 sasa, na yamekuwa ya mafanikio wakati wote, kutokana na mrejesho tunaoupata kupitia watatuzi wa migogoro husika, wasuluhishwa na  utafiti tunaoufanya kutafuta mrejesho na njia nyingine za kupata taarifa ikiwemo kupokea maoni ya wadau.” amesema.

Akifafanua kuhusu ada, amesema fedha hizo zitatumika kulipia vifaa vitakavyotumika katia kozi hiyo, vyakula, vinywaji  pamoja na mambo yote muhimu yanayopaswa kugharamiwa katika kozi hiyo, nje ya usafiri ambao washiriki wanapaswa kujitegemea. 

Amesema ili kufahamu jinsi wahitimu walivyoelewa walichofundishwa kwa ajili ya kukitumia, watapewa mitihani itakayogusia mambo muhimu waliyofundishwa kulingana na miongozo ya kozi husika.

Dkt. Mturi amesema baadhi ya maeneo yatakayofundishwa ni pamoja na jinsi ya kuandaa utatuzi wa migogoro hiyo kwa njia mbalimbali, ikiwemo usuluhishi, sheria za kufuata, namna ya kuzitekeleza kufikia muafaka kusudiwa, vipengele muhimu katika utatuzi wa migogoro hiyo, gharama, jinsi ya kumpata msuluhishi, nguvu ya msuluhishi, namna ya kumaliza mgogoro ulio mahakamani na mengine.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...