Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WASULUHISHI wa migogoro ya kibiashara nchini na wahitimu wa mafunzo ya utatuzi wa migogoro ya kibiashara, wameonywa kuhusu rushwa na kutakiwa kuwa chachu ya usuluhishi wenye mafanikio, kwa faida ya biashara zao na uchumi wa taifa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakitoa mafunzo kuhusu mbinu bora za kutatua migogoro ya kibiashara kwa washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam waelimishaji wabobezi wa masuala ya usuluhishi, chini ya Mpango wa Mafunzo wa Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC) walisema, rushwa ni kikwazo katika suala zima la utekelezaji.

Waelimishaji hao waliotoa mafunzo hayo akiwemo Mhandisi Samwel Msita na Wakili Rosan Mbwambo walitoa elimu hiyo kwa siku tatu mfufulizo na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia maadili, miongozo, sheria,kanuni na miiko ya usuluhishi, huku wakilenga kuimaliza kwa amani ili biashara zisikwame.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayoMhandisi Msita alisema, "Ukiwa msuluhishi mpenda fedha utajikuta ukiuendeleza mgogoro badala ya kuumaliza, kwa sababu hutasimamia haki. Nawasihi wapenda hela kuwa makini na rushwa".

Alisema, ni vyema wanapohitajika kutatua migogoro ya kibiashara, hata kama ni kwenye biashara zao, wasimamie haki na kuangalia namna bora ya kuzifanya pande zilizoingia kwenye mgogoro kuelewana na kuendeleza biashara.

Alisema katika biashara kuna kodi ya nchi inayopaswa kulipwa, hivyo wasuluhishi lazima wame makini kuhakikisha kupenda kwao fedha hakuwapeleki kuithamini rushwa na kuitengenezea mazingira ya ushindi zaidi ya kutatua migogoro iliyombele yao.

"Ikiwa ni kwenye eneo la manunuzi, msuluhishi zingatia sheria za manunuzi na wala usilete zakwako au kuzipindisha zilizopo kwa faida yako. Tunachokitaka ni kuona unafikiwa muafaka wenye mafanikio," alisema.

Kwa upande wake, Wakili Mbwambo alisema, siku zote msuluhishi wa mgogoro wa kibiashara anapaswa kuepuka rushwa na sababu nyingine zinazoweza kumfanya abadili kanuni, sheria na miiko ya usuluhishi, kuepuka kuupendelea upande mmoja.

Kwa mujibu wa Mbwambo, migogoro ya kibiashara inaposhindwa kumalizwa inazuia wahusika kuendelea kufanya biashara, hivyo wasuluhishi wanapaswa kuhakikisha wanawapatanisha huku kila upande ukipata haki yake unaoidai na wala si kuendeleza mivutano inayopoteza muda.

Kutokana na maelezo yake, lengo la usuluhishi wa kibiashara ni kuwaacha walio kwenye mgogoro wa kibiashara wakiwa marafiki wenye uwezo wa kuendeleza biashara kwa amani na kuchangia kukuza uchumi wa nchi.Mafunzo hayo ni ya 14 kuandaliwa na NCC na yalihusisha washiriki kutoka katika fani mbalimbali ikiwemo biashara, sheria, ujenzi na nyinginezo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...