Na
Veronica Kazimoto-Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert
Chalamila, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kufanya vizuri katika
ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha miaka mitano ambapo makusanyo yamekuwa
yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka shilingi trilioni 10.67 mwaka wa fedha
2014/15 hadi kufikia shilingi trilioni 17.87 mwaka wa fedha 2019/20.
Akizindua kikao kazi cha
tathmini ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani Mbeya,
Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa, Serikali hutumia mapato hayo kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
Amesema ufanisi huo unaipa
moyo ofisi yake na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na TRA katika kuhamasisha
wananchi kulipa kodi kwa hiari kwa manufaa mapana ya nchi. Pia, ametoa rai kwa
wakwepaji kodi na kusema kuwa, Serikali itashughulika nao kwani wanahatarisha
ustawi wa nchi.
Naye Kamishna Mkuu wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania Dk. Edwin Mhede, amesema makusanyo hayo ni ongezeko la kutoka
wastani wa sh. bilioni 850 zilizokuwa zinakusanywa kwa mwezi wakati Serikali ya
awamu ya tano inaingia madarakani hadi kufikia wastani wa sh. trilioni 1.5 kwa
mwezi sasa hivi ikiwa ni ongezeko la asilimia 76 kwa mwezi.
Ameeleza kuwa, ongezeko hilo
la makusanyo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na jitihada za serikali ya awamu ya
tano katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na kuzuia mianya ya ukwepaji kodi, kuhamasisha
matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti na kudhibiti nidhamu na
uadilifu kwa watumishi wa TRA.
“Pia miradi mikubwa ambayo
inatekelezwa na Serikali katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia mapato ya
ndani imekuwa ni chachu ya kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari kwa kuwa
walipakodi wanaona thamani ya kodi wanayolipa,” amesema Dkt. Mhede.
Dkt. Edwin Mhede amesema kwamba,
Mamlaka hiyo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha watumishi
wake wanafanya kazi kwa uadilifu na uwajibikaji. Katika kuhakikisha kuwa suala
la maadili linazingatiwa, TRA imeunda idara maalum inayosimamia maadili na
uadilifu wa watumishi hao.
Kikao kazi hicho cha tathmini
ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kimehudhuriwa na washiriki wapato
150 ambapo miongoni mwao ni Mameneja wa TRA wa mikoa na baadhi ya mameneja wa
wilaya kutoka nchini kote na kikao hiki kinategemea kumalizika tarehe 6
Septemba, 2020.
Lengo la kikao hicho ni kutathmini
utendaji kazi wa idara hiyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 na kujadili
mikakati mipya ya mwaka wa fedha 2020/21 kwa
ajili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Albert Chalamila akizungumza na
watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wa uzinduzi wa kikao kazi
cha tathmini ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani
hapa na kitahitimishwa tarehe 6 Septemba, 2020. Lengo la kikao hicho ni
kutathmini utendaji kazi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 na kujadili
mikakati mipya kwa ajili ya mwaka wa fedha 2020/21.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Dkt. Edwin Mhede akizungumzia mafanikio ya TRA katika kipindi cha miaka
mitano ya Serikali ya awamu ya tano wakati wa uzinduzi wa kikao kazi cha tathmini ya utendaji kazi wa
Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani Mbeya na kitahitimishwa tarehe 6
Septemba, 2020. Katika kipindi hiki cha miaka mitano, makusanyo yameongezeka
kutoka shilingi trilioni 10.67 mwaka wa fedha 2014/15 hadi kufikia shilingi
trilioni 17.87 mwaka wa fedha 2019/20.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede
akizungumzia mafanikio ya TRA katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya
awamu ya tano wakati wa uzinduzi wa kikao kazi cha tathmini ya utendaji
kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani Mbeya na kitahitimishwa
tarehe 6 Septemba, 2020. Katika kipindi hiki cha miaka mitano, makusanyo
yameongezeka kutoka shilingi trilioni 10.67 mwaka wa fedha 2014/15 hadi kufikia
shilingi trilioni 17.87 mwaka wa fedha 2019/20.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wakifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa kikao kazi cha tathmini ya
utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani Mbeya na
kitahitimishwa tarehe 6 Septemba, 2020. Lengo la kikao hicho ni kutathmini
utendaji kazi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 na kujadili mikakati mipya
kwa ajili ya mwaka wa fedha 2020/21.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wakifuatilia kwa makini hafla fupi ya uzinduzi wa kikao kazi cha tathmini ya
utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani Mbeya na
kitahitimishwa tarehe 6 Septemba, 2020. Lengo la kikao hicho ni kutathmini
utendaji kazi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 na kujadili mikakati mipya
kwa ajili ya mwaka wa fedha 2020/21.
Baadhi ya Mameneja na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya
Bw. Albert Chalamila (wa tatu kulia) mara baada ya uzinduzi wa kikao kazi
cha tathmini ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani hapa
na kitahitimishwa tarehe 6 Septemba, 2020. PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO -
MBEYA.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...