Serikali imeuagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuandaa na kutekeleza programu maalum ya mafunzo ya Usalama na Afya kwa wachimbaji wadogo katika mikoa yote nchini yenye shughuli za uchimbaji madini ili kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi katika sekta hiyo muhimu katika uchumi wa nchi.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, alipotembelea banda la OSHA katika maonesho ya Tatu ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita.

Waziri Biteko ameeleza kuridhishwa kwake na mafunzo ya usalama na afya kazini ambayo yamekuwa yakitolewa na OSHA kwa baadhi ya makundi ya wachimbaji wadogo na kuahidi kuwapa ushirikiano OSHA kupitia Wizara yake.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, amewataka wadau wa sekta ya madini na sekta nyingine za kiuchumi katika mkoa wake kuzingatia misingi ya usalama na afya katika shughuli zao za uzalishaji.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema baada ya maonesho hayo taasisi yake itaandaa mpango mahsusi wa kutoa mafunzo hayo ya usalama na afya kwa wachimbaji wadogo katika mikoa yote yenye shughuli za uchimbaji madini.

Baadhi ya wadau waliotembelea maonesho wameeleza kufurahishwa kwao na mafunzo ambayo wameyapata kutoka OSHA wakati wa maonesho hayo ya Tatu ya Teknolojia ya Madini.

OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu yenye wajibu wa kulinda nguvukazi ya nchi kupitia kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Waziri wa Madini Dotto Biteko akipata maelezo kwenye banda la OSHA kuhusu shughuli za OSHA mara baada ya kutembelea banda la OSHA kwenye Viwanja vya Bombambili mjini Geita, wakati wa maonesho ya tatu ya Teknolojia na uwekezaji kwenye sekta ya madini.
Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel  akipata maelezo  juu ya OSHA mara baada ya Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi Khadija Mwenda  kumtembelea ofisi kwake, wakati wa Maonesho ya  tatu ya teknolojia na uwekezaji kwenye sekta ya madini yanayofanyika mjini Geita.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi Khadija Mwenda akipata maelezo kutoka kwa moja ya washiriki wa Maonesho, wachimbaji wadogo kwenye Maonesho yanayoendelea  ya tatu ya teknolojia ya uwekezaji kwenye Sekta ya madini Mjini Geita
Baadhi ya wananchi  wakitembelea banda la OSHAna kupata maelezo na elimu ya usalama na afya kwenye maonesho ya tatu ya Teknolijia na uwekezaji kwenye sekta ya Madini yanayoendelea kwenye viwanja vya Bombambili Mjini Geita.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...