Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, John Nchimbi akifungua mkutano mkuu wa 13 wa Mtandao wa vikundi vya wakulima (Mviwata) Mkoa wa Manyara, uliofanyika mjini Babati jana, kushoto ni Mwenyekiti wa Mviwata Mohamed Hussein na Mratibu wa Mviwata Martin Pius. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, John Nchimbi (kushoto) akikagua mazao ya wakulima kwenye mkutano mkuu wa 13 wa Mtandao wa vikundi vya wakulima (Mviwata) Mkoa wa Manyara, uliofanyika mjini Babati. 
Wadau wa kilimo wakiwa katika picha ya pamoja kwenye mkutano mkuu wa 13 wa Mtandao wa vikundi vya wakulima (Mviwata) Mkoa wa Manyara, uliofanyika mjini Babati 

Mwenyekiti wa Mviwata Manyara, Mohamed Hussein akisoma taarifa kwenye mkutano mkuu wa 13 wa Mtandao wa vikundi vya wakulima (Mviwata) Mkoa wa Manyara, uliofanyika mjini Babati. 

……………………………………………………….. 

Na Mwandishi wetu, Babati 

WAKULIMA wametakiwa kugomea vipimo visivyo rasmi vya magunia na madebe wakati wa kupima mazao yao kwani vinawanyonya hivyo watumie mizani ili kuepuka kudhulumiwa haki zao. 

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati, John Nchimbi aliyasema hayo kwenye mkutano wa 13 wa Mtandao wa vikundi vya wakulima (Mviwata) mkoani Manyara. 

Nchimbi alisema wakulima wanapaswa kutambua kuwa vipimo vya ubabaishaji na wizi vya magunia na madebe hayapaswi kutumika kwa sasa kwa hiyo wagomee hilo na kusisitiza kuwepo kwa vipimo kwa kilo. 

Alisema serikali itawaunga mkono kwenye hilo endapo wao wenyewe watakuwa na msimamizi mkali wa kuepuka kunyonywa mazao yao ili wakulima wapate tija na kuepuka kudhulumiwa. 


“Mviwata haiwezi kukulinda wala serikali haitaweza kukusaidia endapo mkulima mwenyewe hautagomea vipimo vya wizi na ubabaishaji dhidi ya mazao ya mkulima. 

Hata hivyo, alisema baadhi ya wakulima wanaweza kuwa vikwazo kwa wenzao kwa kukubali kutumia vipimo vya magunia na madebe kutokana na tamaa ya muda mfupi badala ya kuwa na msimamo. 

Mratibu wa Mviwata mkoani Manyara, Martin Pius alisema wamekuwa karibu na wakala wa vipimo Tanzania juu ya kutumika kwa mizani huku wakitoa elimu na mbinu mbalimbali za kubaini vipimo halisi. 

Pius alisema kupitia mitandao yao mkoani Manyara wamekuwa wakiwaelimisha wakulima namna ya kutumia mizani kwenye upimaji wa mazao na kuachana na mtindo wa kutumia magunia na madebe. 

“Pia wakulima wameendelea kujifunza mbinu mbalimbali za kutambua mizani zinazowaibia wakulima kwa lengo la kuhakikisha wananufaika na mazao yao pindi wakipima uzito wa mazao yao,” alisema Pius. 

Alisema walizungumza na wakala wa vipimo nchini ili kuziwezesha halmashauri kutunga na kupitisha sheria ndogo za kutumia mizani za kupima mazao hasa vijijini. 

Mmoja kati ya wakulima wa kijiji cha Galapo, Hamis Ibrahim aliipongeza Mviwata kwa namna wanavyoingilia kati suala zima la matumizi ya vipimo kwa wakulima wa eneo hilo. 

Alisema awali ilikuwa vigumu wakulima kutekeleza hilo ila Mviwata walizunguka kwa wakulima mbalimbali na kutoa elimu hadi wakatambua haki zao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...