Kaimu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.
Francis Michael akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa ofisi
yake (hawapo pichani) yenye lengo la kuwajengea uwezo kiutendaji ili
waweze kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi
na utawala bora.

Baadhi ya
watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora wakifurahia ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa uandishi wa
nyaraka za ofisi, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, mapambano dhidi ya
rushwa pamoja na namna bora ya kukabiliana na msongo wa mawazo mahala pa
kazi.

Mkurugenzi
Msaidizi, Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Mwanaheri
Cheyo akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi
kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa ofisi hiyo yaliyoanza
Septemba 2, 2020 katika Ukumbi wa UDOM na yatahitimishwa Septemba 4,
2020.
*************************************
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 02 Septemba, 2020.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora (OR-MUUUB) wapatiwa mafunzo yatakayowawezesha kufanya kazi
kwa kuzingatia weledi na ufanisi ili kuboresha utoaji huduma kwa umma na
wadau wengine wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua
mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa ofisi yake yatakayotoa fursa ya
kuwajengea uwezo kwenye eneo la uandishi wa nyaraka za ofisi, utunzaji
bora wa kumbukumbu na nyaraka, mapambano dhidi ya rushwa ikiwa ni pamoja
na namna bora ya kukabiliana na msongo wa mawazo mahala pa kazi.
Dkt. Michael amewaka watumishi hao kufuatilia kwa umakini
mafunzo hayo ili wapate elimu na weledi kuhusu namna bora ya uandishi wa
nyaraka, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, kuepuka vitendo vya rushwa
na msongo wa mawazo ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaweza kuathiri utendaji
kazi wao wa kila siku.
“Mafunzo haya ni muhimu katika kuiwezesha ofisi kupata watumishi
mahiri, waadilifu, wenye kuzingatia weledi na ufanisi kiutendaji”, Dkt.
Michael amesisitiza.
Dkt. Michael amefafanua kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama zilivyo taasisi nyingine nyeti,
inapaswa kuwa na watumishi bora na wenye ujuzi na maarifa
yatakayowaongezea ufanisi kiutendaji na ndio maana menejimenti imeamua
kuwapatia mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kutoa huduma bora kwa
wananchi na wadau wengine.
Mafunzo haya ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa
OR-MUUUB yanafanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kuanzia
tarehe 02 hadi 04/09/2020 na yatahudhuriwa na watumishi 218.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...