Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.GeralD Kusaya (kushoto) akizungumza na watumishi wa Bodi ya Korosho leo mjini Mtwara.Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Francis Alfred.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( kushoto) akizungumza na watumishi wa Bodi ya Korosho mjini Mtwara leo ambapo amewataka kufanya kazi kwa uadilifu na kujiepusha na ubadhirifu wa fedha za wakulima .
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Korosho Francis Alfred akitoa taarifa ya hali ya maandalizi ya msimu wa ununuzi wa korosho msimu wa 2020/21 utakaonza mwanzoni mwa mwezi Octoba ambapo tani 278,000 zinatarajiwa kuzalishwa . (Habari na picha na Wizara ya Kilimo ) 

*********************************** 

Wizara ya Kilimo imesema itachukua hatua kali za kisheria kwa watumishi wa Bodi ya Korosho Tanzania ambao wana tabia ya kujihusisha na ubadhirifu wa mali za umma na wanaodhulumu wakulima nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo (22.09.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipoongea na watumishi wa Bodi ya Korosho na wale wa Chama Kikuu cha Ushirika Masasi na Mtwara (MAMCU).

Katibu Mkuu Kusaya alisema lengo la serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt.John Pombe Magufuli ni kuhakikisha wakulima wanapata fedha zao kwa wakati na usahihi kupitia utendaji wa watumishi waaminifu wa Bodi ya Korosho na vyama vya ushirika.

“ Nitakuwa mkali sana kwa watumishi wa Bodi ya Korosho na vyama vya ushirika wanaoshirikiana na mabenki ya biashara kuwaibia wakulima wa korosho nchini kwa sasa. Watumishi nawataka mridhike na vipato vyenu na kuwa waadilifu “ alisema Kusaya

Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa watumishi watambue kuwa wanalo jukumu la kuhudumia umma kwa uaminifu na kuacha mara moja vitendo vya kuwaibia wakulima wa korosho nchini. 

Aliongeza kusema wizara ya Kilimo itaendelea kuchukua hatua kali kwa watumishi wake watakaokwenda kinyume na taratibu na kutumia vibaya fedha za umma na kuwa mtumishi yeyote atakayejihusisha na ubadhirifu hatoachwa.

“ Nikigundua kuna wizi wa mali ya umma, nitakuja haraka na kuchukua hatua za kunusuru mali za wakulima .Tutumikie wananchi kwa uaminifu zaidi na endapo tukibaini hatua za kisheria zitachukuliwa bila kusita ikiwemo kuwafirisi” alisisitiza Kusaya

Katibu Mkuu Kusaya ameagiza Bodi hiyo kuhakikisha inaratibu kwa ukaribu suala la uatikanaji wa magunia ya kukusanyia korosho toka kwa wakulima mapema kabla ya msimu kuanza mwezi Octoba.
“ Sitaki ifike sehemu tatizo la upatikanaji magunia ya kukusanyia korosho za wakulima lijitokeze mwaka huu tena.Bodi ya korosho fuatilieni vyama vikuu vyenye dhamana ya kuagiza magunia vitekeleze wajibu wao haraka “ alionya Katibu Mkuu Kilimo

Akitoa taarifa ya maandalizi ya msimu wa ununuzi wa korosho msimu 2020/21 , Kaimu Mkurugezni Mkuu wa Bodi ya Korosho Francis Alfred alisema uzalishaji unategemewa kuwa tani 278,000 na kuwa yatahijika magunia takribani milioni 3.4

Alfred aliongeza kusema tayari vyama vya ushirika vina magunia 700,000 huku mengine milioni 2.3 yamewasili nchini tayari kuanza kusambazwa kabla ya kuanza msimu wa ununuzi tarehe 02 Octoba mwaka huu.

Kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na Bodi ya Korosho, Alfred alisema wamefanikiwa kusajili wakulima 280,680 kati ya lengo la kusajili wakulima wa korosho 318,000 katika mikoa 17 inayolima zao hilo.

Bodi ya korosho Tanzania imefanikiwa pia kuratibu upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora na miche bora ya korosho kilo 88,508 katika msimu wa 2019/20 pamoja na usambazaji wa viuatilifu tani 8,780 a salfa ya unga na lita 82,438 za viuatilifu vya maji hali iliyoongeza ubora wa korosho ya Tanzania kufika asilimia 90 ya lengo.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Masasi na Mtwara ( MAMCU) Potency Rwiza amesema katika msimu wa 2019/20 wamefanikiwa kukusanya jumla la Shilingi Bilioni 197.8 kutokana na mauzo ya korosho ghafi za wakulima katika minada 11 iliyofanyika chini ya mfumo wa stakabadhi ghalani.

“Wakulima wa korosho Mtwara na Masasi walilipwa Shilingi Bilioni 180.7 msimu uliopita na kukifanya chama chetu cha MAMCU kuongoza kwa uzalishaji misimu ya miaka miwili sasa.Fedha zote zimelipwa kwa wakulima.” alisema Rwiza. 

Kuhusu hali ya upatikanaji magunia Rwiza alisema tayari wamesha peleka magunia 300,000 na kufikia mwisho mwa mwezi huu watapeleka magunia 160,000 kwa wakulima ambapo makadirio yao ni kuwa na magunia milioni moja msimu huu 2020/21.

“Tunaishukuru Serikali yetu kwa kulipa sehemu ya madeni ya magunia jumla ya Shilingi bilioni 1.7 zimeingizwa kwenye akaunti yetu MAMCU kwa ajili ya misimu iliyopita” Rwiza alisema pia wamepokea Shilingi 86,395,500 kwa ajili ya kulipa wakulima 124 wenye jumla ya kilo 26,259 za korosho ikiwa ni deni la msimu wa 2018/2019.

Katibu Mkuu Kusaya yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara ya kukagua na kutembelea taasisi chini ya wizara na kuzungumza na watumishi ili kuongeza ari ya utendaji kazi ndani ya wizara ya kilimo tangu alipoteuliwa mwaka huu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...