Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuuya Tanzania, Dkt. Eliezer Feleshi akiwasili katika Mahakam Kuu kanda ya Mwanza na Kusalimiana na Watumishi siku ya kwanza ya ziara yake katika Kanda hiyo. Kulia ni Jani Mdfawidhi wa Kandda ya Mwanza, Sam Rumanyika.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuuya Tanzania, Dkt. Eliezer Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na Viongozi wa Mahakama alipotembelea Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza wakimsikiliza Jaji Kiongozi.


Na Lydia Churi- Mahakama, Mwanza

Jaji Kingozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Majaji wa Mahakama Kuu pamoja na Mahakimu wote kuhakikisha wanasikiliza mashauri yanayohusu Mirathi yaliyofunguliwa muda mrefu na kuyamaliza ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza katika siku ya kwanza ya ziara yake kwenye kanda hiyo, Jaji Kiongozi amesema   mashauri hayo ya mirathi yaliyofunguliwa muda uliopita hayapaswi kuvuka mwaka 2020 na amesisitiza kuwa ikiwezekana yasikilizwe hata siku ya Jumamosi ili kuhakikisha yanamaliza ndani ya mwaka huu.

“Mashauri ya Mirathi nyuma yake kuna wajane, wagane na Watoto yatima ambao wanahitaji matunzo ikiwemo kupata haki yao ya kusoma shule, ziko familia zinazovurugika na watoto kupata shida kutokana na mashauri ya aina hii kuchelewa kumalizika”, alisisitiza Jaji Kiongozi.

Jaji Kiongozi pia amewataka Majaji na Mahakimu waliopangiwa kusikiliza mashauri ya mirathi kujiwekea mikakati itakayowezesha mashauri hayo kumalizika ndani ya muda uliopangwa. Aliongeza kuwa viongozi hao hawatapaswa kuchukua likizo mpaka pale watakapokuwa wamemaliza kusikiliza mashauri waliopangiwa. 

Wakati huo huo, Jaji Kiongozi amewashauri watumishi wa Mahakama kujiendeleza kielimu ili kuendana na wakati. Akitolea mfano wa kada ya Mahakimu, Dkt. Feleshi amesema hivi sasa Mahakimu wanaoomba ajira, asilimia kubwa wanakuwa tayari wameshajiendeleza kielimu na kuwa na sifa nyingi za kitaaluma walizozipata kipindi walipokuwa wakisubiri kupata ajira.

Akiwa katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Ilemela alipoenda kumtembelea Kiongozi huyo, Jaji Kiongozi amewaomba Maafisa Tarafa nchini kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kurahisisha upatikanaji wa haki zao.

“Maafisa Tarafa kama walinzi wa amani mnao wajibu wa kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuwa Mahakama inaondokana na ulazima wa wananchi kufika mahakamani kufungua mashauri na badala yake watumie Tehama ili kurahisisha upatikanaji wa haki,” alisema.

Alisema faida za kutumia mfumo wa Tehama katika kurahisisha upatikanaji wa haki ni pamoja na kuondokana na matatizo ya rushwa na kupunguza muda wa wananchi kufika mahakamani ili muda huo wautumie kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali. 

Akizungumzia changamoto za huduma ya Posta Mlangoni ambayo pia hutumika kurahisisha upatikanaji wa nyaraka mbalimbali za kimahakama ikiwemo nakala za hukumu kwa wananchi waliokuwa na shauri mahakamani, Jaji Kiongozi  amewataka wananchi wanaobadilisha anuani zao kuijulisha Mahakama ili waweze kupelekewa nakala zao za hukumu kupitia huduma hiyo ya Posta Mlangoni.

Posta Mlangoni ni huduma iliyoanzishwa na Mahakama ya Tanzania baada ya kuingia mkataba na Shirika la Posta Tanzania uliowezesha shirika hilo kusambaza nyaraka mbalimbali za kimahakama katika maeneo yote nchini.

Katika hatua nyingine, Jaji Kiongozi amewataka Majaji na Mahakimu wa kanda ya Mwanza kuyamaliza mashauri yote ya kanda ya Musoma yaliyosajiliwa kwenye kanda ya Mwanza kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama kuu kanda ya Musoma ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.  

Jaji Kiongozi anaendelea na ziara katika kanda ya Mwanzo ambapo anatarajiwa kukagua shughuli za Mahakama katika wilaya za Ukerewe, Kwimba, Chato, Bukombe pamoja na Mkoa wa Geita.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...