Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imesema ina mkakati wa kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2022 inakua na uwezo wa kutengeneza vitalu vyumba kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga na matunda na kuacha kuagiza nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Vijana, Anthony Mavunde kwenye mahafali ya Chuo cha Don Bosco jijini Dodoma ambapo vijana 980 wametunukiwa vyeti vyao vya kumaliza mafunzo hayo ya muda mfupi.
Akizungumza na wahatimu hao, Mavunde amesema mafunzo hayo ya muda mfupi kwa wanafunzi hao yamedhaminiwa na Serikali kwa kuwalipia ada pamoja na fedha ya nauli kiasi cha Sh Laki Moja kila mwezi.
Mavunde amesema mradi huo wa mafunzo ni muendelezo wa serikali ya awamu ya tano kuwapatia vijana wake mafunzo yatakayowafanya wapate ajira kwa haraka lakini pia yakiwajengea uwezo wa kujiajiri wenyewe.
" Rais Magufuli amejipambanua na Sera yake ya viwanda ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani imetuwezesha leo kufikia uchumi wa kati, hivyo akaona aanzishe programu hii ya kusomesha vijana wa kitanzania ambao wataweza kuajiriwa kwenye viwanda na miradi mbalimbali ya serikali kwani tunao mafundi bomba, mafundi umeme, wajenzi na wengine.
Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Vijana, Anthony Mavunde akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo mafupi katika Chuo cha Don Bosco jijini Dodoma mmoja wa wahitimu kati ya 980 waliohitimu.
Leo wahitimu zaidi ya 900 wametunukiwa vyeti na kati yao asilimia 45 tayari wameshapata kazi, hii ni kuonesha kwa muda mfupi waliosoma wameweza kujiimarisha kwenye fani zao lakini pia tuzipongeze Taasisi na makampuni ambayo yamewapa ajira hawa vijana wetu," Amesema Mavunde.
Naibu Waziri Mavunde amesema mradi huo umewahusisha wanafunzi kutoka mikoa 13 nchini huku akiwataka vijana hao ambao wamehitimu kuungana kwa pamoja na kuanzisha vikundi watakavyovisajili ili waweze kupatiwa mikopo na kuanzisha miradi yao.
" Nitoe rai kwenu wahitimu siyo lazima msubiri ajira, kwa wale ambao mmesoma fani moja na mnaishi karibu anzisheni vikundi mvisajili kisha muombe mikopo Halmashauri ili muanzishe miradi yenu, wapo vijana wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro tuliwasaidia kuanzisha mradi wa vitalu nyumba na leo wako mbali sana hivyo niwatie moyo hata nyie mnaweza," Amesema Mavunde.
Amewataka vijana hao pia kushiriki Uchaguzi mkuu Oktoba 28 kwa kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi sahihi watakaoweza kuwasaidia changamoto zao huku akiwasisitiza kuepuka kutumika na makundi ya kisiasa.
Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Vijana, Anthony Mavunde Akizungumza na wahitimu 980 wa mafunzo ya muda mfupi yaliyofadhiliwa kwa asilimia 100 na serikali.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Vijana, Anthony Mavunde (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chuo cha Don Bosco.
Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Vijana, Anthony Mavunde akiwasili katika mahafali ya Chuo Cha Don Bosco jijini Dodoma ambapo vijana 980 wamehitimu mafunzo ya muda mfupi yaliyodhaminiwa kwa asilimia 100 na Serikali.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya muda mfupi katika Chuo cha Don Bosco jijini Dodoma ambapo vijana takribani 980 wametunukiwa vyeti na Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Vijana, Anthony Mavunde.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...