Mfanyabiashara Abdul Nsembo anayekabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya ameieleza Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, kuwa havitambui vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo dhidi ya kesi yake.
Pia amekana kusaini fomu ya ukamataji wa vielelezo ambayo anadaiwa kusaini nyumbani kwake baada ya kufanyiwa upekuzi usiku wa kuanzia Mei Mosi, 2019.
Nsembo amekana vielelezo hivyo mbele ya Jaji Elinaza Luvanda wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kujitetea, Nsembo akisitiza ombi lake la kutaka Mahakama iruhusu picha za CCTV camera ya nyumbani kwake zilizorekodiwa siku ya tukio ziwasilishwe Mahakamani ili kuthibitisha madai yake.
Akiongozwa na wakili wake Juma Nassoro Nsembo alidai baadhi ya vikopo katika vielelezo namba 3 B mpaka E hajawahi kuviona kabla ila vile alivyowahi kuviona ni vya wakati wa kufunga vielelezo katika Tume ya Kupambana na Kudhibiti dawa za kulevya ambavyo vilikuwa na unga wa njano vyote badala ya ule wa kaki aliouona mahakamani hapo jana.
Aliongeza kuwa, hata hati ya ukamatwaji hakuisaini nyumbani kwake bali alisaini Mei 13, akiwa katika kituo kikuu cha polisi na haikuwa imekamilika kama ile iliyowasilishwa Mahakamani.
“Mimi nililetewa fomu tu ya uthibitisho kwamba tulifanyiwa upekuzi ambayo ilikuwa na majina mawili, langu na Shamim Mke wangu na hakukuwa na majina mengine yoyote tofauti na hii ninayoiona hapa ina majina mengine ya mashahidi na hati yenye orodha ya vielelezo vilivyokamatwa ambayo sikuwahi kuiona hapo mwanzo, hii karatasi yenye orodha ya vielelzo sikuwahi kuiona mahali popote zaidi ya hapa leo.
Aidha Nsembo amekana kumfahamu shahidi wa 7 wa upande wa Jamhuri, Nassoro Athumani ambaye alijitambulisha kuwa ni mlinzi wa ulinzi shirikishi katika mtaa wa upendo, Mbezi beach jijini Dar es Salaam anakoishi na kuongeza kuwa, mtaa anaoishi kila mmoja ana mlinzi wake hakuna ulinzi shirikishi.
"Mimi naishi pale miaka mingi na ninashiriki vikao vya maendeleo, simfahamu kabisa Nassoro na sijawahi kulipa ada ya ulinzi shirikishi, hiyo inamaanisha hakuna ulinzi shirikishi kwenye mtaa wetu," amedai.
Katika maelezo yake Nsembo alidai kesi hiyo imetengenezwa kwa kile alichodai ugomvi baina yake na Inspekta Msaidizi wa polisi Salmin Sherimo ambaye ndiye alikuwa msimamizi wa kazi ya upekuzi siku hiyo, kwa madai kuwa waliwahi kukwaruzana mwaka 2014.
“Hii kesi ilianzia kwenye ugomvi wangu na Salmin ambaye alinikamata mwaka 2014 wakati wa ukaguzi wa magari yaliyotoka Afrika Kusini, alikamata gari langu Mercedes Benz na kunipeleka Kituo Kikuu cha Polisi akitaka niwasilishe nyaraka halali za gari hilo, kulitokea kutoelewana tukafikia kujibizana vibaya lakini baadaye nilishinda na kurudishiwa gari na yeye hakuridhika akaahidi kuwa atanikomesha na ni yeye huyo aliyeongoza askari kupekua nyumbani kwangu hiyo Mei 1,” amedai Nsembo.
Amedai, askari walimkuta chumbani kwake ambapo wakati wanaingia alikuwa akiwaona kwenye CCTV tofauti na ilivyodaiwa mahakamani hapo kuwa alikutwa juu ya dari
Akieleza namna askari walivyokwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake Mei Mosi, 2019 Nsembo amedai, siku hiyo akiwa nyumbani kwake na familia majira ya usiku walisikia kelele nje za geti likigongwa, alitazama kwenye CCTV na kuona kundi la watu wapatao ishirini wakiwa nje ya geti huku wengine wakiwa wamepanda juu ya geti
"Nilihisi tumevamiwa na majambazi, nikamchukua mke wangu na watoto nikawaambia wande chumbani kwa dada wa kazi na mimi nikabaki chumbani nikiangalia picha za CCTV”,
"Niliwaona watu wale wakiongea na kijana wake wa kazi, kidogo alizunguka nyuma ya nyumba na kugonga dirisha la chumba cha dada ambako na mke wangu alikuwemo, baada ya muda mfupi mke wangu alikuja na kuniambia walikuwa ni askari wanamwita nikamruhusu aende,”
Amedai baada ya mke wake kutoka alimwona akiwafungulia mlango na wakaingia ndani ya uzio baadaye mkewe aliingia ndani hakujua alienda kufanya nini lakini alipotoka alimuona akitoa ishara kidole kuelekea mlango wa gereji ya kulaza magari na kijana wake wa kazi akafungua milango hiyo iliyokuwa imeegeshwa.
Aliendelea kudai kuwa baada ya kuingia gereji hakujua nini kiliendelea kwa kuwa Kamera ya CCTV haikuwepo katika eneo hilo lakini aliwaona wakitoka baada ya muda wakiwa hawana chochote.
Waliendelea na upekuzi katika maeneo mengine ikiwemo magari yaliyokuwa ndani ya uzio, vyumbani, jikoni na baadaye wakaingia chumbani kwake ambako walimkuta na kumfunga pingu kabla ya kuanza upekuzi ndani ya chumba hicho na baadaye wakawatoa nje kabisa ya uzio wa nyumba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...