Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainab Chaula (kushoto) akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Nne la Mwaka la TEHAMA jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainab Chaula (kushoto) akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonaz baada ya kufunga Kongamano la Nne la Mwaka la TEHAMA, jijini Dar es Salaam.


Na Faraja Mpina - WUUM, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainab Chaula ameiasa jamii ya kitanzania kutumia simu janja kutafutia fursa mbalimbali za kujitafutia kipato ili kuinua uchumi binafsi na  nchi kwa ujumla.


Dkt. Chaula alizungumza hayo alipokuwa akifunga Kongamano la Nne la Mwaka la TEHAMA lililofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 7 hadi Oktoba 9, 2020. 


“Tuzitumie simu janja vizuri kwa kutafuta fursa za kutuinua kiuchumi, tusitumie  simu hizo kuperuzi kwa ajili ya burudani pekee bali tufunguke, tutafute fursa za kiuchumi kwa kutumia simu janja zilizounganishwa na mtandao ili maendeleo yapatikane kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla”, alizungumza Dkt Chaula.


Dkt Chaula ametoa rai kwa  wadau kutoka taasisi za umma na binafsi walioshiriki katika Kongamano hilo kutekeleza yale yaliyo ndani ya uwezo wao, wasiiachie Serikali ifanye kila kitu kwasababu fursa nyingi zinapatikana kwa wadau hao ,na kuwaasa wasitoe fursa kwa kufahamiana bali kwa kila mtanzania anayekidhi vigezo kulingana na Katiba, sheria na taratibu za nchi.


Aidha, Dkt. Chaula aliliambia Kongamano hilo kuwa, Wizara imepokea maoni yote yaliyotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi kwa haraka, uaminifu na uadilifu mkubwa, ili fursa zilizobainishwa na masuala mengine yaliyojadiliwa ambayo yanahitaji  mkakati wa kidijitali, kwa kushirikiana na wadau mkakati huo utaandaliwa na kutekelezwa kwa wakati.


Naye Mhadhiri kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Dkt. Moses Mwasaga amesema kuwa  matumizi stahiki ya simu janja yatawezesha watu wengi zaidi kuingia na kushiriki kwenye uchumi wa kidijitali kwa kupata huduma mbalimbali na kutengeneza ajira kama ilivyo kupitia mfumo wa miamala ya fedha kupitia simu ya mkononi, ambapo watu wengi wameweza kujiajiri kama mawakala wa kutoa huduma hiyo muhimu, ambayo hapo awali ilikuwa ikitolewa na benki pekee.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...