Na. Ramadhani Kissimba na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali imepokea msaada wa Faranga za Uswisi milioni 15.75 sawa na shilingi bilioni 39.59 kwa ajili ya kugharamia mradi wa uboreshaji wa afya na uimarishaji wa mfumo wa afya pamoja na kugharamia program ya kutokomeza Malaria nchini.
Akipokea msaada huo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.Doto James alisema lengo kuu la msaada huo ni uanzishwaji wa huduma ya msaada wa kitaalam kwa Serikali chini ya utaratibu wa kituo cha kuimarisha mifumo ya afya kilichopo Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Aidha, Bw. James alisema msaada huo utatumika kuwezesha mpango wa kudhibiti Malaria Tanzania ili kuondoa kabisa vifo vinavyotokana na malaria na kupanua wigo wa maeneo yasiyokuwa na malaria (Malaria Free Zones).
Bw. James alisema kuwa hii ni mara ya pili katika kipindi cha siku 30 zilizopita kwa Serikali ya Uswisi kuipatia Tanzania msaada wa kuboresha masuala ya afya ambapo tarehe 6 Oktoba, 2020 nchi hiyo iliipatia Tanzania shilingi bilioni 44.10 na kufikisha kiwango cha msaada katika kipindi hicho kufikia sh. Bilioni 83.7
‘Nchi zetu mbili zina uhusiano mzuri unaoendelea kukua kama unavyothibitishwa na kuongezeka kwa idadi ya miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali za Uswisi’ alisema Bw. James
Bw. James alieleza kuwa Tanzania imekuwa ikinufaika na inatarajia kuendelea kunufaika na ufadhili wa Serikali ya Uswisi, hususan katika maeneo ya afya, ajira na kipato, utawala bora, utamaduni na elimu.
Aliongeza kuwa miradi au program zinazoendelea kutekelezwa nchini kupitia ufadhili wa Serikali ya Uswisi inagharimu zaidi ya Faranga za Uswisi milioni 65.3 sawa na shilingi bilioni 164.12 na miradi iliyokamilika inagharimu zaidi ya Faranga za Uswisi milioni 59.87 sawa na shilingi bilioni 150.87.
Kwa upande wake Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot amesema tangu mwaka 2001, Uswisi kwa kushirikiana na Tanzania imekuwa ikitekeleza mapambano dhidi ya malaria kupitia program mbalimbali zenye lengo la kuisaidia nchi kufikia malengo iliyojiwekea kupitia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Mhe. Chassot aliongeza kuwa kati ya mikataba miwili iliyosainiwa mmoja unalenga kuimarisha mfuko wa bima ya afya ya jamii, ambao unasimamiwa na TAMISEMI ujulikanao kama ‘’CHF iliyoboreshwa’’.
Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Mkurugenzi wa Kinga Wizara hiyo, Dkt. Leonard Subi, alisema msaada huo utasaidia kuendeleza mafanikio yaliyopatikana hasa upatikanaji wa dawa na kuimarisha mifumo ya takwimu katika sekta ya afya nchini.
Dkt. Subi alisema katika mapambano ya malaria, Tanzania imepunguza idadi ya vifo vinavyotokana na malaria kutoka aslimia 14.8 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017.
Aliongeza kuwa Wizara ya afya kwa kushirikiana na Tamisemi itahakisha msaada huo unatumika vizuri kwa kutekeleza ipasavyo malengo ya msaada huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia) na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot, wakisaini mikataba miwili ya msaada wa Faranga za Uswisi milioni 15.75 sawa na Sh. bilioni 39.59 kwa ajili ya Uboreshaji wa Afya na Uimarishaji wa Mfumo wa Afya na Programu ya Kutokomeza Malaria Tanzania, katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot, wakibadilishana mikataba miwili ya msaada wa Faranga za Uswisi milioni 15.75 sawa na Sh. bilioni 39.59 kwa ajili ya Uboreshaji wa Afya na Uimarishaji wa Mfumo wa Afya na utekelezaji wa Programu ya Kutokomeza Malaria Tanzania, katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot, wakiwaonesha wanahabari mikataba miwili yenye thamani ya shilingi bilioni 39.59 ikiwa ni msaada uliotolewa na Serikali ya Uswisi kwa ajili ya Uboreshaji wa Afya na Uimarishaji wa Mfumo wa Afya na Programu ya Kutokomeza Malaria Tanzania. Hafla ya utiaji Saini mikataba hiyo imefanyika Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot, wakiwaonesha wanahabari mikataba miwili yenye thamani ya shilingi bilioni 39.59 ikiwa ni msaada uliotolewa na Serikali ya Uswisi kwa ajili ya Uboreshaji wa Afya na Uimarishaji wa Mfumo wa Afya na Programu ya Kutokomeza Malaria Tanzania. Hafla ya utiaji Saini mikataba hiyo imefanyika Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shaaban.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot, wakipongezana baada ya kusaini mikataba miwili yenye thamani ya shilingi bilioni 39.59 ikiwa ni msaada uliotolewa na Serikali ya Uswisi kwa ajili ya Uboreshaji wa Afya na Uimarishaji wa Mfumo wa Afya na Programu ya Kutokomeza Malaria Tanzania. Hafla ya utiaji Saini mikataba hiyo imefanyika Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, akielezea umuhimu wa msaada wa Faranga za Uswisi milioni 15.75 sawa na Sh. bilioni 39.59 kwa ajili ya Uboreshaji wa Afya na Uimarishaji wa Mfumo wa Afya na Programu ya Kutokomeza Malaria Tanzania kuwa ni pamoja na kuimarisha nguvu kazi inayotumika kuimarisha uchumi wa nchi, baada ya kusainiwa mikataba hiyo, jijini Dar es Salaam.Meza Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa pili kulia) na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot, wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Amina Shaaban na Wajumbe kutoka Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, baada ya kusainiawa mikataba miwili ya msaada wa Sh. bilioni 39.59 kwa ajili ya kuboresha Sekta ya Afya.
Meza Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa pili kulia) na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Mhe. Didier Chassot, wakiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe kutoka Idara ya Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya kusainiawa mikataba miwili ya msaada wa Sh. bilioni 39.59 kwa ajili ya kuboresha Sekta ya Afya, jijini Dar es Salaam.(Picha na Wizara ya Fedha na Mipango-Dar es Salaam)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...