Mwezeshaji wa mafunzo akimuelekeza mmoja wa washiriki wa
mafunzo namna ya kuweka bidhaa katika soko mtandao.

Mwezeshaji nwa mafunzo, Faki Othman Faki, akiendelea kutoa mada
kwa washiriki katika mafunzo hayo ambapo amewataka kuwa wabunifu zaidi.

Washiriki wa mafunzo hayo wakiendelea na mafunzo.


Na Gaspary Charles - TAMWA Zanzibar.

WANAVIKUNDI vya ujasiriamali kisiwani Pemba wametakiwa kutumia fursa
ya uwepo wa mitandao ya katika kuongeza wigo wa kutangaza
na kuuza bidhaa zao kupitia soko mtandao.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuvijengea uwezo vikundi hivyo juu ya
matumizi ya soko mtandao yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Zanzibar mwezeshaji wa mafunzo hayo, Faki Othman Faki amesema ili mjasiriamali aweze kukua kiuchumi ni lazima ajue kutumia fursa ya mitandao ya kijamii.

Amesema uwepo wa mitandao hiyo imerahisisha uwezekano wa mjasiriamali
kuuza na kuwafikia wateja wengi zaidi kwa muda mfupi pasipo kutumia
nguvu kubwa kama ilivyo kwa njia nyingine za utaftaji wa masoko.

“Ni muhimu sana kuchangamkia fursa ya soko mtandao kwani ndiyo sehemu
pekee kwa sasa ambayo inaweza kukutanisha na wateja wengi zaidi na kwa
haraka duniani pasipo kutumia nguvu nyingi,” amesema.

Aidha mwezeshaji huyo alitahadharisha wajasiriamali hao kuachana na
dhana ya kuzalisha bidhaa kwa mazoea kwani kufanya hivyo kutapelekea
kuwakosesha wateja kutokana na bidhaa hizo kukosa mvuto na ubora wa
kushindana na bidhaa nyingine sokoni.

Pia amewasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia misingi ya
masoko ikiwa ni pamoja na kuimarisha mahusiano na mawasiliano chanya
kwa wateja ili kujenga uaminifu wa wateja kwa bidhaa zao.

Amesema, “Tuache taba ya kuzalisha bidhaa kwa mazoea na badala yake
tujenge misingi ya kuwa na mawasiliano ya karibu na wateja wetu ili
kujua mahitaji yao kwani hii itakusaidia kujua wapi pana hitaji
kuboreshwa ili kuendelea kuaminika zaidi sokoni.”

Mmoja wa washiriki hao, Fadhila Ali Juma ameshukuru kwa
mafunzo hayo kwani itawasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa soko
kwa bidhaa walizokuwa wanazalisha.

“Kiukweli leo nimefurahi sana kupata mafunzo haya kwani kuanzia leo
kikundi chetu tutaanza kutumia fursa hii tuliyooneshwa kwa ajili ya
kuuza bidhaa zetu ambazo ni, Sabuni asilia, Mafuta na majani ya chai
kwani changamoto kubwa inayotukabili ni upatikanaji wa masoko
tunazalisha sana lakini soko ni kikwazo,” amesema.

Mapema afisa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi Zanzibar - (WEZA
III) kutoka TAMWA ofisi ya Pemba, Asha Mussa Omar amesema lengo la
kutolewa mafunzo hayo ni kuwapatia mbinu za kuongeza wigo wa
upatikanaji wa soko la kuuza bidhaa zao wanazozalisha ili lengo la
kujikwamua kiuchumi lifanikiwe.

“TAMWA Zanzibar imeamua kutoa mafunzo haya ili yawawezeshe
wajasiriamali wetu kutambua na kuchangamkia fursa zilizopo katika soko
mtandao kwa lengo la kuendelea kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha
wanawake kiuchumi Zanzibar - (WEZA III) unaotekelezwa na TAMWA
Zanzibar kwa ufadhili wa Milele Zanzibar Foundation.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...