Maofisa
kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi makao Makuu Dodoma
wakipeana maagizo namna ya kutekeleza zoezi la elimu ya mlipa kodi nje ya Ofisi
ya Halmashauri ya Manyoni, kabla ya kuanza utekelezaji wa zoezi hilo nyumba kwa
nyumba katika mtaa wa Majengo.

Na Eliafile Solla
WATENDAJI wa sekta ya Ardhi katika Halmashauri ya Manyoni mkoani Singida, wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao kwa urahisi zaidi, kauli hiyo imetolewa na Kaimu kamishna wa Ardhi msaidizi mkoa wa Singida Speratus Ruteganya, katika kampeni maalum iliyozinduliwa na Wizara ya siku ya elimu ya mlipa kodi ambayo hutekelezwa kila siku ya Ijumaa.
Akizungumza na kikosi kazi maalum kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kilichofika Wilayani Manyoni kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu kodi ya pango la Ardhi, Ruteganya amesema umoja na ushirikiano ndiyo nguzo pekee ya kufikia malengo katika sekta ya Ardhi. Aliongeza kwamba, wananchi wanachohitaji ni elimu tuu kwani wakielimika kodi itapatikana pamoja na taarifa muhimu za umiliki.
Kwa upande wake kiongozi wa kikosi kazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Adam Komba amesema, lengo la Wizara kuanzisha siku ya elimu kwa mlipa kodi ni kuhakikisha wananchi wanapewa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi pamoja na kuboresha taarifa zao za umiliki.
Alisisitiza kwamba, kutokana na mabadiliko ya teknolojia hasa kwenye utoaji wa huduma, Wizara ina mpango wa kuboresha mifumo yake ya utoaji huduma hivyo pamoja na kutoa elimu kuhusu kodi ya pango la Ardhi pia zoezi linalenga upatikanaji wa taarifa muhimu za kila mmiliki wa kipande cha Ardhi.
Kwa upande wake Afisa Ardhi mteule wa Wilaya ya Manyoni Bi. Zamzam Seif, ameishukuru Wizara ya Ardhi kwa hatua mathubuti iliyochukua ya kuboresha taarifa za wamiliki Ardhi na pia kampeni ya siku ya elimu ya mlipa kodi, amesema, kitendo cha Wizara kutuma kikosi kazi Wilayani hapo na kimewapa moyo sana na nguvu mpya ya kufanya kazi.
Siku ya elimu ya Mlipa kodi ni kampeni maalum iliyoanzishwa na Wizara ya Ardhi ambapo, kila siku ya Ijumaa kikosi kazi kitakuwa kinapita mitaani kutoa elimu nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha wamiliki wa Ardhi wanajua sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayoisimamia sekta ya Ardhi. Pamoja na hayo, pia lengo ni kuhakikisha Wizara inajenga ukaribu zaidi na wamiliki wa Ardhi na kuona namna bora ya kutatua changamoto mbalimbali za sekta ya Ardhi kwa ujumla.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...