WAZIRI wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo ameipongeza menejimenti ya Benki ya Biashara ya DCB kwa uongozi wake mahiri na wenye tija uliowezesha kufanikisha tukio la utoaji wa gawio kwa wanahisa wake wakuu.

 

Pongezi hizo zilitolewa na Mheshimiwa Waziri Jafo katika tukio hilo lililofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibu ambapo DCB ilitoa gawio la kiasi cha shs milioni 500 kwa wanahisa wake wakiwa ni Jiji ja Dar es Salaam, Manispaa za Dar es salaam, Mfuko wa Uwekezaji (UTT) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

  “Naomba nichukue nafasi hii kuipongeza benki ya DCB kwa mafanikio makubwa iliyoyapata kwa kipindi cha miaka kumi na nane tangu kuanzishwa kwake. Natambua kuwa benki hii imeanzishwa kwa malengo ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wananchi wa kawaida ili wajikwamue kutoka kwenye umasikini.

“Benki ya DCB imeweza kujiendesha kwa faida kwa miaka takribani 12 kwa ujumla, huku ikitoa gawio kwa wanahisa wake kwa miaka kumi mfululizo, kiasi kinachofikia shilingi bilioni 12 na pia napenda kutambua juhudi za bodi ya wakurugenzi na uongozi wa benki kuhakikisha benki inapata mtaji kupitia zoezi la uuzwaji hisa lililokamilika kwa mafanikio makubwa mwaka jana.

 Waziri Jafo alisema serikali inaamini kuwa Sekta ya benki ni kati ya sekta muhimu katika kuendeleza uchumi wa Taifa na wananchi kwa ujumla hivyo mafanikio ya sekta za kifedha nchini ni moja ya nyenzo muhimu katika kufanikisha adhma ya serikali  ya kuwa na uchumi imara sambamba na mkakati wa maendeleo wa miaka mitano 2017-2021 ambao unasisitiza juu ya umuhimu na mchango wa sekta ya fedha katika kuchochea shughuli za uwekezaji na uzalishaji mali.

 Pamoja na hayo waziri alisema serikali inaipongeza jumuiya ya mabenki kupitia TBA na Benki kuu (BoT) kwa usimamizi thabiti na ushauri ambapo kwa pamoja imesaidia mabenki kuendelea kutoa huduma na kuvuka salama katika changamoto za Covid -19 mwanzoni mwa mwaka huu.

 “Napenda kuchukua nafasi hii pia kuwapongeza wanahisa wote wa benki, zikiwemo manispaa za Dar es Salaam, kwa kuiamini benki hii na kuwekeza mtaji tangu benki inaanzishwa, na kuendelea kuwekeza kila mara inapohitajika.

 Aidha alisema Manispaa zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha zinatoa ushirikiano kwenye benki yetu, na akachukua nafasi hiyo kuzipongeza kwa kufanikiwa kujiunga na mfumo wa malipo wa kielektroniki (GePG) wa benki hii ambao utachagiza ukuaji wa miamala na amana nafuu kwa benki na pia kurahisisha utendaji wa manispaa hizi.

 “Katika hafla ya leo nimeelezwa kuwa benki ya DCB imetoa gawio la shilingi milioni 500 kwa wanahisa wake wote. Natambua wanahisa watakaopokea gawio leo rasmi ni Halmashauri za Manispaa na Jiji shilingi milioni 138,603,889 Mfuko wa UTT shilingi 119,074,887 na Shirika la NHIF shilingi milioni 30,780,000.

 “Natoa pongezi zangu za dhati kwa Bodi ya Wakurugenzi na menejimenti ya Benki ya Biashara ya DCB kwa uongozi mahiri na hatua makini katika kuhakikisha benki yenu inaendelea kuwa na kimbilio la wananchi. Ni matumaini yetu kama serikali kuwa DCB itazidi kufanya vizuri mwaka hadi mwaka na kuzidi kuboresha huduma zake za kibenki ili ziendane na hali halisi ya watanzania wenye vipato vyote.

 Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Godfrey Ndalahwa alisema safari ya kimkakati iliyoanza mnamo mwaka 2018 ya kuhakikisha benki inarudi kwenye kupata faida na kujiimarisha ndani ya mwaka mmoja, na pia kujidhatiti katika kuwa benki thabiti katika mwaka wa pili, kabla ya kuanza ukuaji na upanuzi wa huduma zake katika mwaka wa tatu imekuwa na mafanikio makubwa.

 “ Napenda niwataarifu kuwa leo hii, ikiwa ni miaka mitatu tangu kuanza safari hii, tumefanikiwa kurudi kwenye faida mwaka 2018 na tumekuwa tukijiendesha kwa faida hadi sasa. Vilevile, benki imefanikiwa kuongeza mtaji kupitia uuzwaji wa hisa mwaka 2019 na kuendelea kujiimarisha zaidi. Benki yetu ipo imara kimtaji, kupungua mikopo chechefu, kuongezeka kwa ukwasi na uendeshaji bora huku ikifuata taratibu na miongozo ya usimamizi wa Benki Kuu na Mamlaka nyingine za usimamizi za serikali.

  “Hivi sasa, tunajivunia kukamilisha hatua mbili muhimu katika safari yetu hii za mageuzi na kujiimarisha, na sasa tupo katika hatua ya tatu ya ukuaji na upanuzi wa huduma zetu tukijikita katika kuhakikisha tunaongeza idadi ya wateja kutoka 200,000 kufikia 300,000 mnamo mwaka 2022, kukuza idadi ya matawi yake kufikia 13, na vituo vya huduma kufikia 25 kutoka idadi ya sasa hivi ya matawi 8 na vituo sita”, alisema Bwana Ndalahwa.

 Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa DCB imedhamiria kupanua wigo kwa kufungua matawi mapya ikiwemo tawi la wateja wakubwa (DCB ROYAL FAMILY) pamoja na ufunguzi wa vituo vipya nchini huku huduma za kidigitali zikiwa msaada mkubwa wakiwa na wateja zaidi ya 131,556 kulinganisha na wateja 123,285 mwaka 2018.

 “Kipekee napenda kukushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kukubali wito wa kujumuika pamoja nasi katika hafla hii,  aidha wageni mliohudhuria tukio hili kwa kukubali kufika na kutupa ushirikiano kipindi chote cha safari ya mafanikio ya benki yetu, wakuu wa wilaya kwa kutupa miongozo mbalimbali ya kiutawala, wakurugenzi wa manispaa kwa kutupa ushirikiano kwenye mambo ya kibiashara, wanahisa wote kwa kutuamini na kuwekeza na sisi, wahazini wa manispaa kwa mambo ya kimchakato na miamala ya kibenki, wateja kwa kutuamini na kuwekeza amana”, akaongeza mkurugenzi huyo.

 Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro alisema benki hiyo iliyoanzishwa mnamo mwaka 2002 kwa maelekezo ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, hayati Mhe. Benjamin William Mkapa imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa mitaji midogo midogo kwa wananchi wa kipato cha chini, ambapo hadi mwishoni mwa mwezi wa Desemba 2019, imeweza kutoa mikopo kwa wanawake na vijana wanaofikia zaidi ya 50,000 yenye jumla ya shilingi billioni 160 kwa wafanyabiashara wadogo wa vikundi, ikiwemo shilingi billioni 16 zilizotolewa kwa mfuko wa wanawake na vijana wa halmashauri za Jiji la Dar es salaam kupitia njia ya ukopeshaji wa vikundi vidogo kwa kutumia mfumo wa asilimia 10 ya mapato yao.

 “Leo hii, najivunia kilele cha mafanikio haya ambapo baada ya kupata faida ya Tsh 2.1 bilioni, na kwa idhini ya Benki Kuu na azimio la Wanahisa, Bodi ya wakurugenzi imependekeza kutoa gawio la sh milioni 500 ambayo ni robo ya faida na kubakisha sehemu ya faida baada ya kuangalia mahitaji ya kuendelea kuimarisha mtaji wa benki na kuiwezesha benki kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kupata faida zaidi miaka ya mbeleni”, alisema Bi. Zawadia.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Selemani Jafo, akikabidhi mfano wa hundi yenye dhamani ya shilingi 138,603,889 ikiwa ni gawio la wanahisa kutoka Benki ya DCB kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe (wa pili kushoto), na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Sarah Msafiri, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Godfrey Ndalahwa, pamoja na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo Zawadia Nanyaro, hafla hiyo imefanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Godfrey Ndalahwa, akiwakaribisha Mkuu Wilaya ya Kigamboni Sarah Msafiri,na Mkurugenzi wa Jiji Bi Sipora Jonathan  wakati wa hafla ya Benki ya DCB ilipokuwa ikitoa Gawio kwa wanahisa wake wakuu jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Godfrey Ndalahwa (katikati), akimsikiliza  Mkurugenzi Mtendaji  wa Mfuko wa Uwekezaji (UTT) Simon Migangala wakati wa hafla ya benki ya DCB ya kutoa gawio kwa wanahisa wake wakuu jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Bodi wa benki hiyo Zawadia Nanyaro.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...