Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara, kupitia CCM.
………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Babati 


WANACHAMA na wakereketwa wa CCM wa Mji wa Babati Mkoani Manyara, wameipongeza Kamati Kuu ya CCM kwa kukata mzizi wa fitina na kurudisha jina la Diwani wa Kata ya Maisaka, Abdulrahaman Kololi kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri baada ya uchaguzi wa nafasi hiyo kufanyika mara tatu na mshindi kukosekana. 


Kololi na diwani wa kata ya Mutuka, Yonah Wawo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo waligombea nafasi hiyo na kura zikarudiwa mara tatu na kila mmoja akapata kura sita hivyo suala hilo likafikishwa kwenye kamati kuu iliyomteua Kololi. 


Halmashauri ya mji wa Babati ina kata nane zenye madiwani wa CCM na watatu wa viti maalumu huku mbunge wake Pauline Gekul akiwa wa CCM hivyo kufikisha idadi ya wadiwani 12 hivyo madiwani hao kugawana kura mara tatu. 


Kada maarufu wa CCM mjini Babati Cosmas Masauda amesema anaipongeza Kamati kuu kwa kukata mzizi wa fitina na kuteua jina sahihi la Kololi ili awe Mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo.
Masauda amesema Kololi ni mtu makini ambaye atasimamia nafasi ya Mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo kwa kuhakikisha maendeleo yanapatikana na kuwasimamia watumishi. 


“Pia Kololi hawezi kuuza viwanja vilivyopo wazi hapa mjini Babati ndiyo sababu tunaipongeza Kamati kuu kwa kurudisha jina la kijana makini ambaye ataisimamia vyema halmashauri ya mji wetu,” amesema Masauda. 

Muuza biriani maarufu wa mjini Babati, Zulekha Ahmed amempongeza Kololi kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo kwani wananchi wa eneo hilo walikuwa na imani naye. Mbunge wa jimbo la Babati mjini, Pauline Gekul amempongeza Kololi kwa kuteuliwa kwenye nafasi hiyo na kuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha kwenye nafasi hiyo. 

“Mwenyekiti wa halmashauri sasa amepatikana tuchape kazi ndugu zangu, tutulie sasa madiwani wetu wakatekeleze ilani, pia mvua zimenyesha tukalime tujenge nchi yetu,” amesema Gekul.
Mchakato wa uchaguzi huo ulisababisha mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya hiyo, Hussein Yaburima kulazwa mahabusu na kufukuzwa kwenye nafasi hiyo akidaiwa kutoa nje siri za kikao kilichoazimia kukata jina la Kololi. 

Hata hivyo, mjumbe huyo Yaburima amesema hayupo tayari kuzungumza kwenye vyombo vya habari juu ya yeye kulazwa mahabusu na kufukuzwa katika nafasi hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...