Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

BARAZA la Ujenzi la Taifa (NCC,) limefungua milango kwa wadau wa masuala ya ujenzi, wakiwemo wakandarasi, wasanifu majengo, wakadiriaji majenzi, mafundi ujenzi wa ngazi mbalimbali na wana vyuo wa taaluma ya ujenzi, kutumia maktaba ya taasisi hiyo kujisomea mambo ya kitaaluma, ili kujiongezea maarifa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Baraza hilo, Dk Matiko Samson Mturi, amesema kuwa maktaba ya NCC ina vitabu visivyopatikana katika maktaba nyingine nchini na hata nje, ndio maana imekuwa ikiazimwa baadhi ya vitabu na wataalamu wanaotoka nje ya Tanzania, pamoja na taasisi za ujenzi zilizoko nje ya nchi.

Dk. Mturi amesema maktaba hiyo yenye vitabu 424, imesheheni machapisho mengine mbalimbali yenye taarifa za ukuaji na maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini, tangu miaka ya 1980 huku akisisitiza umefika wakati wadau wa ujenzi nchini waitumie, badala ya kuachia fursa ya kupata maarifa kupitia vitabu kwa watu na taasisi za nje.

"Ni vyema ikafahamika kuwa NCC ina maktaba inayojitosheleza kwa vitabu muhimu vinavyohitajika kwenye sekta ya ujenzi kwa sasa. Ieleweke pia kuwa Baraza linaruhusu wadau mbalimbali wa masuala ya ujenzi waitumie maktaba yetu, kwa kuzingatia masharti rahisi ya muda wa kazi na kuwa na hitaji la kweli la kitabu.

Kutokana na maelezo ya Dk. Mturi, hakuna malipo yanayotozwa kwa sasa kwa yeyote anayefika kutumia maktaba hiyo. "Hata kama itabadilika baadaye, kwa sasa ni bure kutumia maktaba ya NCC,"amsema. 

Ameongeza lengo ni kuamsha ari ya wadau wa ujenzi kujisomea na kupata maarifa ya kiufundi zaidi ambayo vitabu vilivyopo vimeyagusa moja kwa moja."Maktaba yetu iko ghorofa ya tisa kwenye jengo la Samora (Samora Tower) lililopo katika Mtaa wa Mansfield jijini Dar es Salaam".

Aidha, pamoja na kuwepo kwa maktaba hiyo kwa muda sasa, ni watu wachache wamekuwa wakifika kupata huduma, jambo linalompa wasiwasi kwamba huenda utamaduni wa watu kutopenda kujisome umeendelea kuwa changamoto.

Dk.Mturi amesema watu na taasisi za nje ya Tanzania ndio wamekuwa wakivutiwa zaidi na vitabu vilivyopo katika maktaba hiyo kutokana na jinsi wanavyovichangamkia kwa kuviulizia, kuja kuvisoma na wengine kuviazima.

"Maktaba ya NCC ni kubwa na ina wafaa pia wataalamu wanaofanya utafiti wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya ujenzi. Ni vyema ikaeleweka kuwa NCC ina majukumu tofauti likiwemo la kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya ujenzi kupitia vitabu na machapisho mengine ya kitaaluma yaliyopo maktaba."

Majukumu mengine ya NCC aliyoyataja ni kutoa elimu ya usuluhishi wa migogoro inayotokea katika miradi ya ujenzi, kutoa ushauri wa kiufundi katika masuala yote yanayohusiana na sekta ya ujenzi na kufanya tafiti zinazohusu masuala ya ujenzi nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...