MADINI ya makaa ya mawe yanayochimbwa mkoani Ruvuma yameingiza zaidi ya shilingi bilioni 400 na kutengeneza ajira za watanzania zaidi ya 700.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema kiasi hicho  cha fedha kimepatikana kutokana na mauzo ya madini ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni  3.3 ambayo yameuzwa kuanzia Agosti 2017 hadi Oktoba 2020.

Ameutaja uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe unafanyika katika wilaya za Songea ,Mbinga na Nyasa na kwamba Mkoa wa Ruvuma una hazina kubwa ya mashapo ya madini ya makaa ya mawe yaliyofanyiwa utafiti na kampuni tatu kubwa za uchimbaji.

“Kwa mujibu wa utafiti unaoendelea kufanyika,Mkoa wa Ruvuma una mashapo ya makaa ya mawe zaidi ya tani  milioni 457,mashapo hayo tulionayo,tunaweza kufanya uchimbaji kwa miaka 718 bila kumaliza hazina hii’’,amesisitiza Mndeme.

Hata hivyo Mndeme amesema katika kipindi cha mwaka 2019/2020  zaidi ya tani 636,000 za makaa ya mawe yaliyochimbwa mkoani Ruvuma ziliuzwa ndani na nje ya nchi.

Amesema Mkoa wa Ruvuma umebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali yakiwemo madini ya vito na dhahabu ambayo yanachimbwa kwa wingi katika wilaya za Tunduru,Songea ,Mbinga na Nyasa.

Mndeme amesema katika Mkoa wa Ruvuma kuanzia Mei 2019 yalifunguliwa masoko ya madini ya vito na dhahabu  katika wilaya za Songea na Tunduru ambapo hadi sasa kupitia masoko hayo zimeuzwa gramu zaidi ya milioni moja zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 7.7 na kwamba watanzania zaidi ya 1000 wamepata ajira za uchimbaji kwenye madini hayo mkoani Ruvuma.

Amesema tayari limejengwa jengo   kubwa la kituo cha umahiri cha madini la Mkoa ambalo litatumika kutoa elimu ya madini kwa wachimbaji wadogo,elimu ya upatikanaji wa masoko ya madini na elimu ya utambuzi wa madini.

Imeandikwa na Albano Midelo

Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...