Na Mwandishi wetu, Manyara
TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, imemtaka
mkurugenzi wa kampuni ya Namaingo Business Agency ya jijini Dar es
salaam, Biubwa Ibrahim kuwarudishia wajasiriamali 300 wa Wilayani
Hanang' shilingi milioni 42 walizozichukua mwaka 2017.
Mkuu
wa TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu ameyasema hayo Novemba 9
Mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Makungu
amesema TAKUKURU Mkoani Manyara imeanza kuchukua hatua baada ya Rais
John Magufuli kuagiza vitendo vya dhuluma na rushwa kukomeshwa.
"Octoba
25 akiwa kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati, Rais John Magufuli
alitoa ahadi mbalimbali ikiwemo kutokomea vitendo vya dhuluma na
rushwa," amesema Makungu.
Amesema
TAKUKURU inafanya uchunguzi juu ya kampuni ya Namaingo na mkurugenzi
huyo Biubwa na baadhi ya maofisa wa serikali wasiokuwa waaminifu
walichukua fedha za wajasiriamali hao tangu mwaka 2016 wakidai
kuwafanyia semina.
Amesema
katika semina hiyo wajasiriamali hao walitakiwa kujiunga katika vikundi
vya watu 50 na kila mwana kikundi alitakiwa kuandaa banda la kuweka
vifaranga vya kuku 1,000 na kuahidi kuwapatia vifaranga 1,000 kama
mtaji.
Amesema viongozi
wa kampuni hiyo waliwaahidi wajasiriamali hao kuwapatia chakula, dawa za
kuwakinga na ugonjwa vifaranga hao hadi kufikia hatua ya kufikishwa
sokoni na watawatafutia masoko.
"Baada
ya maelezo hayo ya kuvutia kutoka kwa viongozi wa Namaingo
wajasiriamali hao kila mmoja alitakiwa kulipa shilingi 140,000 kwa
mchanganuo mbalimbali," amesema Makungu.
Amesema
Kati ya fedha hizo shilingi elfu 50 ni ya kiingilio, shilingi elfu 46
ya usajili wa BRELA, shilingi elfu 20 kwa ajili ya ukaguzi wa maeneo ya
kufugia vifaranga, shilingi elfu 20 za gharama ya kuingia mkataba na
shilingi elfu 5 ya kufungulia faili.
Amesema
viongozi wa Namaingo baada ya kupokea fedha hizo walitoweka na
wajasiriamali hao walipofuatilia fedha zao hawakufanikiwa na kubaini
wamefanyiwa udanganyifu.
"Takukuru
Mkoani Manyara tunamtaka mkurugenzi wa kampuni ya Namaingo Biubwa
popote alipo ajisalimishe na kurudisha fedha za wajasiriamali hao kabla
ya Novemba 30 kwani baada ya hapo watawachukulia hatua," amesema
Makungu.
Amewataka
wajasiriamali hao waliochukuliwa fedha zao wafike na nyaraka
zinazoonyesha kwenye ofisi za TAKUKURU Wilayani Hanang' na aliyembali
atume nyaraka kwa barua pepe rbcmanyara@pccb.go.tz ili madai yao yaweze kufanyiwa kazi kwa pamoja.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...