Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
WAHAMIAJI haramu 36 kutoka nchini Ethiopia na Somalia wamehukumiwa kulipa faini ya sh. 600,000 ama kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuingia nchini bila ya kuwa na kibali.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya washtakiwa kufukishwa mahakamani hapo leo Novemba 18, 2020 na kusomewa mashtaka mawili ya kuishi nchini bila kibali na kukubali kutenda makosa hayo.
Kabla ya kusomewa adhabu hiyo Hakimu Shahidi aliwapa washtakiwa nafasi ya kujitetea ili wapunguziwe adhabu ndipo wote waliiomba mahakama iwaonee huruma kwa sababu wametoka nchi ambazo zinavurugu na wamekuwa Tanzania kutafuta amani na uhuru.
"Nimesikia lakini nyie bado ni wadogo na ni vijana ambao mnaweza kutafuta maisha huko huko kwenye nchi zenu mlizotoka ila mlichofanya nyie ni tamaa" amesema Shaidi.
"Mahakama inawahukumu kulipa faini ya sh.600,000 na mkishindwa mtatumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani na wakimaliza kutumikia adhabu hiyo warudishiwe nchini kwao", amesema Shaidi
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Godfrey Ngwijo imedai kuwa Novemba 16, 2020 huko katika eneo la Mbweni beach ndani ya wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa ni raia wa Ethiopia na Somalia waliingia katika Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania bila ya kuwa na kibali cha kuwaruhsu wao kufanya hivyo.
Katika shtaka la pili washtakiwa hao wanadaiwa siku na mahali hapo walikutwa wakiishi nchini Tanzania bila ya ama nyaraka zozote zinazowaruhusu kuishi nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...