Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya vya umma wametakiwa kuheshimu fedha za dawa kadri zilivyopangwa kwenye bajeti ya Serikali kuu na vyanzo vingine ili kuweza kuondoa kero ya upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya afya nchini.

Rai hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 21 wa kutathimini utekelezaji wa vipaumbele vya kisera katika sekta ya afya uliofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Gwajima amesema kuwa bado kuna maoni mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na ukosefu wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini,hivyo viongozi wa hospitali na vituo vya kutolea huduma vya umma wanapaswa kuanisha matumizi ya fedha za dawa walizopokea au kutoka kwenye makusanyo ya mapato ya hospitali hiyo Pamoja na matumizi yake.

“Ili kufikia azma ya Mhe. Rais, sisi kama sekta ya afya inabidi kuongeza kasi katika uwajibikaji wa Pamoja katika malengo tuliyoyaweka, ni lazima tufanye upekuzi wa matumizi ya fedha za dawa,vifaa na maabara lazima ziheshimike na kufika kwa mgonjwa ili wananchi watuamini na kuweza kutatua kero zao”. Alisema

Aidha, Dkt. Gwajima amesema katika kutekeleza hilo,Wizara itatoa maelekezo ya kuongeza ufanisi katika uwajibikaji kuanzia kwa watumishi wote wa sekta ya afya,ngazi mbalimbali za usimamizi na uendeshaji katika sekta na taasisi zilizo chini ya wizara Pamoja na wadau wote wanaotekeleza masuala mbalimbali katika sekta ya afya.

Hata hivyo Dkt. Gwajima amewahimiza wadau wote kuweka kipaumbele kwenye utekelezaji kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa na serikali kwa miaka mitano ijayo (2020-2025),kwa uwajibikaji wa Pamoja katika ngazi zote za kutolea huduma za afya nchini na hivyo kuboresha huduma zitakazotolewa ili kuwafikia wananchi wote na kuwapatia huduma kulingana na mahitaji ya kiafya yanayowakabili.

Aliongeza kuwa licha ya mafanikio ya sekta ya afya nchini ,sekta hiyo bado inaendelea kuwa na changamoto ambazo juhudi za Pamoja zinahitajika ili kukabiliana nazo ikiwepo ile ya wananchi wengi bado wako nje ya mfumo wa bima ya afya na hivyo kukosa huduma za afya kwa wakati kutokana na changamoto za kifedha ambapo hadi sasa ni asilimia 11 tu ndio wamejiunga.

Kwa upande wa tiba asili na tiba mbadala Dkt. Gwajima amesema zimekuwa zikisaidia katika kutibu magonjwa mbalimbali kwa wananchi na hivyo serikali inakusudia kuimarisha kitengo cha utafiti wa tiba mbadala.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Festo Dugange amesema ili kufikia lengo la kuwawezesha wananchi wote kuwa na bima ya afya kunahitajika kuimarisha kwa mifuko ya bima ya afya na ili kuwafikia wananchi wengi zaidi ni kuweza kukamilisha mpango mkakati wa sera ya ugharamiaji wa huduma za afya Pamoja na sheria ya bima kwa wote.

“Mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa kwa sasa unachangia asilimia 5 ya wanufaika wote waliojiunga katika mifuko ya bima za afya nchini na katika kipindi cha utekelezaji wa mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa kuanzia Julai 2018 tumefanikiwa kusajili kaya 557,882 sawa na wanufaika 3,347,112 kufikia Novemba 2020”. Alisema Dkt. Dugange.

Hata hivyo amesema jumla ya shilingi bilioni 16.2 zimekusanywa katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2020 ambapo zimewezesha kuimarisha huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuwawezesha wananchi yakiwemo makundi maalum kuzifikia huduma hizo bila vikwazo vya kifedha.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa afya Dkt. Godwin Mollel amesema upo uwezekano wa sekta ya afya kufanya vizuri endapo viongozi na wadau wa maendeleo wakijipanga na kushirikiana ili kufikia malengo ya kuwahakikishia watanzania wanapata huduma za afya bora na kwa uhakika.

Dkt. Mollel amesema matatizo na kero nyingi ambazo zipo kwa wananchi zinahitaji uelewa kwani wananchi wengi bado hawajafikiwa na hii ni kutokana na mfumo wa mawasiliano,hivyo amewata waganga wakuu wa Mkioa,Wilaya na waganga wafawidhi wa hospitali kutoa mawasiliano yao ili wananchi waweze kusaidiwa pale pasipohitaji msaada.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima akifungua mkutano wa 21 wa kutathimini vipaumbele vya utekelezaji wa kisera katika sekta ya afya uliofanyika jijini Dodoma

Katika mkutano huo watendaji wakuu wa sekta ya afya walisaini mkataba wa kisera ambao utatekelezwa na wadau wote nchini

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akiongea na washiriki wa mkutano huo(hawapo pichani) ambapo

 Waziri Dkt.Gwajima akimkabidhi tuzo ya shukrani Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Afya Edward Mbanga.
Wakurugenzi wa taasisi zilizo chini ya wizara ya afya wakifuatilia mkutano huo ambapo wametakiwa kushirikiana kwa pamoja na wadau wa afya ili kuimarisha huduma za afya nchini

Waziri wa Afya Dkt. Gwajima akimkabidhi tuzo ya shukrani Mwakilishi Mkazi wa  Shirika la Afya Duniani(WHO) nchini Tanzania Dkt. Tigest Mangestu kwa kuthamini mchango wao katika sekta ya afya nchini
Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Festo Dugange akiongea kwenye mkutano huo ambao umewakitanisha viongozi mbalimbali kutoka wizara ya afya,TAMISEMI,Wizara zinazojihusisha na masuala ya afya,sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo nchini
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...