* Baraza liandae Kanuni za kujiendesha na kuchangia mapato na ukuaji wa uchumi
* Asema waache kufanya kazi kwa mazoea, atawapima kwa matokeo na sio michakato
* Ameilekeza Tume ya TEHAMA kusajili wataalamu wenye ubunifu na sio vyeti tu
Na Prisca Ulomi, WMTH
Waziri
wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile
amelitaka Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC)
kushughulikia malalamiko ya wananchi na changamoto wanazozipata wakati
wanatumia huduma na bidhaa za mawasiliano nchini
Dkt.Ndugulile
ameyasema hayo wakati wa ziara yake alipotembelea TCRA – CCC akiwa
ameambatana na Naibu Waziri wake, Mhandisi Andrea Kundo Mathew kwa
malengo ya kukutana na bodi, menejimenti na wafanyakazi wa taasisi za
Wizara yake ili waweze kufahamiana, kutambua majukumu yao na kuweka
mwelekeo wa utendaji kazi wenye matokeo ili kufikia matarajio na ndoto
za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli ya kuunda Wizara hii mpya
Amesema kuwa wananchi wana
malalamiko kuhusu huduma wanazozipata hususani kwenye mitandao ya simu
kuhusiana na mabando yao kuisha, kubadilishiwa gharama za matumizi ya
mabando, kupunjwa mabando yao na fedha wanazotuma kwa njia ya mtandao na
haya yote yanahitaji majibu na kupatiwa matibabu
“Hatutaki
kufanya kazi kwa mazoea, nitawapima kwa matokeo na sio michakato,
tutakwenda kwa mwendo wa takwimu na kila baada ya miezi mitatu tupate
taarifa ya malalamiko mangapi yamepokelewa, mangapi yamefanyiwa kazi,
mangapi yameisha na kwa nini mengine hayajaisha kwa kuwa haya ni mambo
ya msingi ambayo tunatakiwa tuyaangalie na tuwe taasisi ya kutatua
changamoto za wananchi,” amesisitiza Dkt. Ndugulile
Ameongeza
kuwa ni vema tuweke mifumo ya kulinda watumiaji na walaji wa huduma za
mawasiliano na bidhaa za TEHAMA na taarifa na siri zao kwa kuwa sekta
hii inaendelea kukua na watu wanatumia biashara mtandao na hawaendi
madukani na tumieni lugha nyepesi kuelimisha wananchi namna ya kutumia
huduma na bidhaa za TEHAMA na muwe na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa
Baraza ili kutekeleza sheria ya TCRA iliyounda Baraza
Katika
hatua nyingine ameitaka Tume ya Taifa ya TEHAMA kuishauri vizuri Wizara
ili kufahamu mwenendo na mwelekeo wa wapi tunataka tupeleke TEHAMA ndani
ya nchi na tujue tuna wataalamu wangapi wa TEHAMA, tunahitaji wataalamu
wa namna gani na waje watibu changamoto za aina gani.
“Tumejiwekea
malengo ya kuhakikisha kuwa matumizi ya brodibandi yanafikia asilimia
80 ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 45 ya mwaka 2020 ili wananchi
wanufaike na huduma za mawasiliano”, amefafanua Dkt. Ndugulile
Naye
Naibu Waziri, Mhandisi Kundo Andrea Mathwe ameongeza kuwa TCRA na TCRA
CCC ni taasisi zilizo chini ya Wizara na moja inashughulika na watoa
huduma na nyingine watumiaji wa huduma ambapo ni rahisi kufanya nao kazi
na kuishauri Wizara kutatua malalamiko ya wananchi kwa kuwa mwananchi
anaweza kulalamika kuwa ameibiwa bando kumbe akielemishwa atafahamu
vizuri kwanini bando limeisha na hii itawafanya wananchi wavutiwe zaidi
kutumia huduma za mawasiliano na hatimaye tutachangia pato la taifa ili
kufikia malengo yaliyowekwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025
Katibu
Mtendaji wa TCRA CCC, Mary Shao Msuya amesema kuwa Baraza limejipanga
kushughulikia maelekezo yaliyotolewa kwa kuwa watumiaji wa huduma na
bidhaa za TEHAMA wameongezeka tofauti na mwaka 2003 wakati Baraza
linaanzishwa ambapo kulikuwa na huduma chache ya kupiga na kupokea simu
na za vifurushi tu wakati hivi sasa kuna huduma za kutuma na kupokea
pesa, tutaongeza kasi ya utendaji kazi ili twende na kasi ya ukuaji wa
TEHAMA nchini
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA amesema
kuwa watazingatia suala la usajili wa wataalamu wa TEHAMA pamoja na
maeneo yao ya ubobezi ikiwemo usalama wa mtandao; utengenezaji wa
programu; uchakataji na uhifadhi wa taarifa na data; na ubunifu ili nchi
iwe na wataalamu wa kutosha na kuendana na mahitaji kwa kuzingatia kasi
ya ukuaji wa TEHAMA duniani
Dkt. Ndugulile ataendelea na ziara
yake kwenye taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ikiwemo Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),
Shirika la Posta Tanzania (TPC) ambapo atazungumza na bodi, menejimenti
na wafanyakazi

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...