Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, akimbidhi Sh.milioni 8,600,000, Esther Pununta (wa pili kushoto) mbele ya Wajumbe wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida, mkoani hapa juzi, akiwa ni mmoja wa waathirika waliopitiwa na wimbi  la  ‘Mikopo Umiza,’ ambazo ziliokolewa na Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Singida. Kushoto ni mtoto wake Naomy Geuza. Wa tatu kutoka kulia ni Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, Wengine ni Mstahiki Meya Yagi Kiaratu na Naibu Meya, Hassan Mkata.

Muathirika wa Mikopo Umiza  Mwalimu Mstaafu Seleman Haji, akimkabidhi shilingi milioni 46 mke wake Magdalena Gunda baada ya kukabidhiwa na  Mkuu wa Mkoa wa Singida  Dk .Rehema Nchimbi,

 Mkuu wa Mkoa wa Singida  Dk. Rehema Nchimbi, akizungumza na Wajumbe  wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida (hawapo pichani) baada ya kukabidhi fedha hizo.

Muathirika wa Mikopo Umiza  Loth Mwangu,  akiwa na fedha zake baada ya kukabidhiwa.

Wajumbe  wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida wakishuhudia waathirika wa Mikopo Umiza walivyo kuwa wakirudishiwa fedha zao.


Baadhi ya waathirika wa mikopo hiyo wakiwa na maafisa wa Takukuru wakati wa kurudishiwa fedha zao.
Wajumbe  wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida wakishuhudia waathirika wa Mikopo Umiza walivyo kuwa wakirudishiwa fedha zao.
Wajumbe  wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida wakishuhudia waathirika wa Mikopo Umiza walivyo kuwa wakirudishiwa fedha zao.

*NDANI YA MIEZI MITATU YAOKOA ZAIDI YA MILIONI 80

Na Godwin Myovela, Singida

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),  kwa kasi na mwendelezo ule ule imeendelea kuwafuta machozi wananchi wanyonge mkoani hapa, kwa kuokoa na hatimaye kuwakabidhi fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 80 walizokuwa wametapeliwa kupitia Kampuni za Mikopo zinazoendesha shughuli zake kinyume na utaratibu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, amewakabidhi kiasi hicho cha fedha waathirika wote waliopitiwa na wimbi hilo, maarufu ‘Mikopo Umiza,’ mbele ya Wajumbe wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida, mkoani hapa juzi.

“Ni Serikali hii ya Magufuli ndio iliyofanikisha kuwabana hawa wakopeshaji haramu na hatimaye leo mnakabidhiwa haki yenu iliyokuwa imeporwa, tuendelee kumshukuru Rais kwa mema haya anayoendelea kutufanyia,” alisema Nchimbi.

Zoezi la urejeshaji wa fedha hizo kwa waathirika limefanyika mbele ya madiwani hao ili kuhamasisha umuhimu wa ushirikiano na utendaji wa pamoja baina yake na Taasisi hiyo katika kupiga vita vitendo vyote vya rushwa, ikizingatiwa madiwani ni miongoni mwa viongozi wanaowajibika kwa karibu zaidi na wananchi.

 Akiwasilisha taarifa ya fedha zilizookolewa kutokana na Riba Umiza katika kipindi cha Oktoba na Disemba mwaka huu, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alisema takribani shilingi milioni 88.8 zimeokolewa na kurejeshwa kwa wahusika. 

Mathalani, mbele ya Mkuu wa Mkoa na Madiwani wa Baraza la Manispaa, Elinipenda alieleza kwamba miongoni mwa matukio yaliyodhibitiwa na Taasisi hiyo katika kipindi cha miezi 3 iliyopita ni pamoja na tukio la kusisimua la mkopeshaji mmoja asiye na vibali vya kufanya biashara hiyo ya ukopeshaji alimkopesha Mwalimu Mstaafu Seleman Haji shilingi milioni 6.5 na baada ya mwalimu huyo kupokea pensheni yake mkopeshaji alimtaka amlipe shilingi milioni 46.

“Takukuru iliingilia kati makubaliano hayo ya kikandamizaji kwa kumtaka mkopeshaji huyo arejeshe shilingi milioni 39.5 na amefanya hivyo. Tunaomba Mkuu wa Mkoa umkabidhi leo hii mstaafu huyu fedha yake iliyookolewa,” alisema Elinipenda.

Hata hivyo matokeo ya ufuatiliaji na udhibiti huo umebaini kuwa baadhi ya wakopeshaji binafsi wanafanya shughuli hiyo bila ya vibali halali, hali inayosababisha kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mapato na kujipatia fedha isivyo halali.

Aidha, udhibiti umebaini kuwepo kwa utozaji mkubwa wa riba zisizovumilika za zaidi ya asilimia 100 kinyume na viwango vilivyowekwa na kuainishwa na Benki Kuu. 

Aidha, kupitia ripoti hiyo iliyowasilishwa na Takukuru, imeelezwa baadhi ya wakopeshaji hawaandai mikataba ya ukopeshaji, hivyo wakopeshwaji hawana nakala za mikataba, na hata iliyopo kwa baadhi ya kampuni hizo haikidhi sifa na vigezo.

Imeelezwa, baadhi ya kampuni hizi za mikopo hazina hata wataalamu wa mahesabu hali inayowafanya kutoza riba zenye mkanganyiko, na hivyo kujikuta wakimbambikiza riba kubwa mkopeshwaji.

Pamoja na mambo mengine imebainika kuwa kuna uvujishaji mkubwa wa taarifa za watumishi wanaostaafu. Mathalani taratibu za malipo ya mafao ya mstaafu yanapokuwa yamekamilika wakopeshaji wanakuwa wa kwanza kupata taarifa kabla ya mhusika mwenyewe. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...