Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC Plc) imetoa vifaa saidizi zaidi ya 800 kwa watu wanaoishi na ulemavu katika mikoa tano tofauti ikiwa ni sehemu ya program yake maalumu ya huduma kwa jamii yenye kauli mbiu yake ya ‘Tunaleta Mabadiliko Pamoja.’

Tukio la hivi karibuni lilifanyika katka Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi ambapo TCC Plc ilitoa vifaa saidizi zaidi ya 170 kwa watu wanaoishi na ulemavu.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Albert Mwombeki, ambaye alishuhudia tukio hilo, aliishukuru TCC Plc kwa kutoa msaada huo na kutoa wito kwa mashirika mengine na makampuni kuiga mfano huo. 

 “Msaada huu utawawezesha watu wenye ulemavu katika wilaya yetu na maeneo mengine yaliyonufaika na msaada huu kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwani itakuwa rahisi kwao kusogea kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine bila kuhitaji msaada mkubwa, jambo ambalo litatoa ahueni kwa familia zao na wanaowategemea,” alisema na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono jitihada kama hizi za TCC Plc.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) Tawi la Ruangwa, Dorice kamilos, alisema TCC Plc imekuwa mkombozi kwao kwani sasa wanaweza  kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine bila shida. 

“Sasa tunaweza kufanya shughuli mbalimbali katika maeneo tofauti tunaishukuru sana TCC na tunawaomba wasiishie hapo kwani bado msaada wao unahitajika,” alisema. 

Akizungumzia program nzima, Meneja Mahusiano ya Serikali wa TCC Plc, Derick Stanley alisema hadi sasa wametoa vifaa saidizi zaidi ya 800 katika mikoa mitano, Lindi ikiwa moja wapo. 

“Hii inaendana na sera yetu ya huduma kwa jamii na pia tuliamua kuungana na watu wanaoishi na ulemavu nchini katika mwezi huu ambapo ndio Siku ya Kimataifa ya Watu wenye ulemavu huadhimishwa Disemba 2 kwa maana hiyo mwezi wote huu tumeshirikiana nao katika mikoa mitano na kugawa vifaa saidizi,’’ alisema. 

Alisema mikoa iliyonufaika na misaada hiyo ni pamoja na Tabora ambapo waligawa magongo pea 100, fimbo nyeupe 100 na baiskeli 10 za magurudumu matatu, Katavi-fimbo nyeupe 100, Rukwa –baiskeli za magurudumu matatu 23, magongo 100 na fimbo nyeupe 15, Lindi-magongo pea 100, fimbo nyeupe 100 na baiskeli za magurudumu matatu 28.  

 Alisema mwaka jana peke yake, TCC iliwafikia zaidi ya watu 1800 wanaoishi na ulemavu nchi nzima kupitia program hiyo.

 “Hakuna namna bora ya kumaliza mwaka kama hii ya kurudisha kwa jamii tunayoijali. Tunajivunia kwa sababu tunajua misaada hii itanufaisha familia zao pia na wategemezi wao kwani sasa wanufaika hawa wanaweza kushiriki katika shughuli za kujipatia kipato hivyo kwa pamoja tutaweza kupambana na umaskini,” alisema.

Katika hatua nyingine, TCC plc imetoa msaada wa vyerehani kwa vikundi viwili vya wanawake vijulikanavyo kama Mvumweni na Wanambono vilivyopo katika vijiji vya Tae na Mbono wilayani Same.

Hatua hiyo ilisababisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Same, Anastazia Tutuba kuvipandisha hadhi vikundi hivi na kusema sasa hivi ni viwanda vidogo ambavyo vinaendana na dira ya maendeleo ya 2025 (Tanzania Development Vision 2025) ya uchumi wa viwanda.

Shughuli ya makabidhiano ilifanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Same.


Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Albert Mwombeki (wa pili kulia waliosimama) akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka kampuni ya Sigara Tanzania (TCC Plc) na wanufaika wa vifaa saidizi vilivyotolewa na kampuni hiyo kwa watu wenye ulemavu Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi chini ya programu maalumu ya huduma kwa jamii yenye kauli mbiu ‘Tunaleta Mabadiliko Pamoja.’
Meneja Programu za Jamii wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC Plc) Oscar Lwoga (kushoto) akikabidhi vifaa saidizi kwa Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Katavi, John Kyame (kulia) ikiwa ni sehemu ya program ya TCC Plc ya huduma kwa jamii yenye kauli mbiu ‘Tunaleta Mabadiliko Pamoja’. Katikati ni Mwenyekiti wa Chama Cha Wasioona Tanzania (TLB) Isaac Mlela.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabella Chilumba (kulia) akishuhudia Meneja wa Programu za Kijamii wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC Plc) Oscar Lwoga (kushoto) akigawa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Nyasa chini ya programu maalumu ya huduma za kijamii ya kampuni hiyo yenye kauli mbiu ya ‘Tunaleta Mabadiliko Pamoja’ huku mbunge wa eneo hilo Mh. Stella Manyanya (katikati) na wadau wengine wakishuhudia pia.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...