Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Umoja
wa Ulaya (EU) kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), umeipatia
Tanzania msaada wa Euro milioni 30 sawa na shilingi za kitanzania
bilioni 84 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kujenga miundombinu ya
kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia.
Sehemu ya fedha
hizo, kiasi cha Euro milioni 26 sawa na shilingi bilioni 72, Mkataba
wake umeingiwa leo Jijini Dar es Salaam (15 Desemba, 2020) kati ya
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, Balozi wa
Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Frederic Clavier na Mkurugenzi Mkazi wa
Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bi. Stephanie Mouen Essombe.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto james, alisema kuwa fedha hizo
kiasi cha Euro milioni 26 kitatumika kujenga kituo cha kupooza umeme -
Tunduma, kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kv 330 yenye urefu wa
kilometa 4 kutoka Tunduma hadi mpakani mwa Tanzania na Zambia.
“Mradi
huu pia unahusisha ujenzi wa njia mpya ya kusafirisha umeme katika
maeneo ya vijijini, ambayo hayajafikiwa na Grid ya Taifa na kuongeza
uwezo wa njia zilizopo za kusafirisha umeme kupitia Iringa – Kisada –
Mbeya – Tunduma – Ushoroba wa Sumbawanga” alisema Bw. James
Alisema
hatua hiyo itaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea
uzalishaji katika maeneo ya vijiji husika na pia kuongeza upatikanaji wa
umeme katika maeneo yasiyofikiwa na yale ambayo umeme hautoshi hususan
maeneo ya Kusini Magharibi mwa nchi yetu, ambayo yamekithiri umaskini.
Bw.
James alisema kuwa msaada huo unaonesha kwamba Jamhuri ya Ufaransa na
Umoja wa Ulaya ni marafiki wazuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kinyume na dhana ya baadhi ya wapinzani wa nchi wanaodai kwamba uhusiano
wa Tanzania na wadau wake wa maendeleo unadorora.
“Kupitia
uhusiano wetu huu mzuri tunatambua kuwa kiwango cha uwekezaji cha AFD
kwa Serikali ya Tanzania kimefikia takriban Euro milioni 454.5, sawa na
shilingi trilioni 1.26 ambazo zinajumuisha mkataba uliosainiwa hivi
karibuni wa mkopo wa masharti nafuu wa Euro milioni 100 kwa ajili ya
mradi huu” Aliongeza Bw. James.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Maendeleo la Ufaransa Bi Stephanie Mouen Essombe alisema kuwa miezi
michache iliyopita Shirika lake lilisaini mkataba wa mkopo nafuu wenye
thamani ya Euro milioni 100 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa
kusafirisha umeme wa Tanzania na Zambia.
“Leo tumekutana tena kwa
ajili ya kusaini mkataba wa kiasi kingine cha nyongeza cha Euro milioni
26 sawa na shilingi bilioni 72 ambazo ni msaada uliotolewa na Umoja wa
Ulaya kupitia Shirika letu” alisema Bi. Stephanie
Alisema Mradi
wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia ni sehemu ya mwisho ya
utekelezaji wa mradi wa ushoroba (corridor) kutoka Ethiopia, Kenya,
Tanzania na Zambia unaolenga kupunguza gharama za matumizi ya nishati
hiyo pamoja na kukuza uchumi wa nchi husika.
Alisema kuwa hivi
karibuni, Shirika lake litatoa kiasi kingine cha Euro milioni 130 kwa
ajili ya kutekeleza mradi mwingine mkubwa wa nishati jua (solar PV
Power) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50, utakaojengwa mkoani
Shinyanga.
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania
Mhe. Frederic Clavier, alisema uhusiano wa Tanzania, Ufaransa na Umoja
wa Ulaya uko imara na kwamba nchi hizo zitaendelea kuchangia maendeleo
ya nchi kwa juhudi zote.
Alifafanua kuwa nchi yake kupitia
Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) itaendelea kuwekeza katika
masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambapo katika kipindi cha
miaka 10 Bodi ya wakurugenzi ya AFD imeidhinisha matumizi ya kiasi cha
Euro milioni 430 kwa ajili ya sekta ya nishati.
Naye Kaimu Balozi
wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Mhe. Emilio Rossetti, alisema kuwa
mbali na msaada wa kiasi hicho cha Euro milioni 26 zilizosainiwa, Umoja
wake utatoa kiasi kingine cha msaada wa Euro milioni 4 kwa ajili ya
kulijengea uwezo Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) na kufanya
kiasi kilichotolewa na EU kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa
(AFD) kufikia Euro milioni 30 sawa na shilingi bilioni 84.
Alisisitiza
kuwa Umoja wa Ulaya unatambua jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali
ya Awamu ya Tano ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kwamba Umoja
wa Ulaya utaendelea kuunga mkono juhudi zake za kuwaletea wananchi
maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Frederic Clavier wakibadilishana hati za mkataba wa msaada wa Euro milioni 26 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 72 ikiwa ni sehemu ya msaada wa Euro milioni 30 sawa na shilingi bilioni 84 uliotolewa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), kwa ajili ya mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia, hafla hiyo imefanyika Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Frederic Clavier wakionesha wanahabari (hawapo pichani) hati za mkataba wa msaada wa Euro milioni 26 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 72 ikiwa ni sehemu ya msaada wa Euro milioni 30 sawa na shilingi bilioni 84 uliotolewa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), kwa ajili ya mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia, hafla hiyo imefanyika Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bi. Stephanie Mouen Essombe akisaini mkataba wa msaada wa Euro milioni 26 uliotolewa na Umoja wa Ulaya kupitia Shirika lake kwa ajili ya kusaidia kujenga miundombinu ya mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.Doto James na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bi. Stephanie Mouen Essombe wakibadilishana hati za mkataba wa msaada kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wenye thamani ya Euro milioni 26 kati ya Euro milioni 30 (sh. bil. 84) zilizotolewa na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia.Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James akionyesha kwa waandishi wa habari zawadi ya kitabu alichopewa na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Frederic Clavier mara baada ya hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa msaada kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wenye thamani ya Euro milioni 26 kati ya Euro milioni 30 zilizotolewa na Umoja wa Ulaya kupitia Shirika lake kwa ajili ya mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia, Hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam.Meza kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw, Doto James (katikati), kulia kwake ni Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Frederic Clavier na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa, Tanzania Bi. Stephanie Mouen Essombe na kushoto kwake ni Kaimu Balozi wa Umoja wa Ulaya Emilio Rossetti na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shaabani wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Nishati, mara baada ya hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa msaada kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wenye thamani ya shilingi bilioni 72 kati ya shilkingi bilioni 84 zilizotolewa na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia. (Picha na Ramadhani Kissimba, WFM, Dar es Salaam)Meza kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw, Doto James (katikati), kulia kwake ni Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Frederic Clavier na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa, Tanzania Bi. Stephanie Mouen Essombe na kushoto kwake ni Kaimu Balozi wa Umoja wa Ulaya Emilio Rossetti na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shaabani wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa waandamizi kutoka Umoja wa Ulaya na Ubalozi wa Ufaranza nchini Tanzania, mara baada ya hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa msaada kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wa shilingi bilioni 72 kwa ajili ya mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...