Habari hizo zimetakiwa kuzingatia kipindi kabla, baada na wakati wageni wakiwa nchini ili kujenga taswira chanya ulimwenguni kote.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki wakati wakati akifungua warsha ya siku mbili kati ya Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Wahariri na Waandishi waandamizi wa Vyombo mbalimbali vya Habari jijini Arusha.
Maelezo yake aliyafafanua zaidi wakati wa kujadili masuala mbalimbali kuhusu Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jami, ambapo warsha hiyo imelenga kujadiliana, kubadilishana uzoefu na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Wizara hiyo ikiwemo hifadhi ya Ngorongoro katika kuendeleza sekta hiyo.
“Wanahabari mnalo jukumu kubwa katika jamii hasa kwa kuandika habari za kujenga taswira chanya itakayosambaa duniani kote na kuvutia watalii kote duniani,” alisema Dkt. Nzuki.
Pia amewataka kuwa wazalendo katika tasnia ya habari ambayo ni chanzo kikubwa cha kuaminika."Katika Warsha hii tutakumbushana zaidi kuwa wazalendo ili kujenga jamii imara yenye kujivunia Taifa la Tanzania."
Aidha, amevipongeza vyombo vya habari kwa kuwa mstari wa mbele katika kupeleka habari njema zikiwemo za Utalii nje ya nchi kupitia programu mbalimbali za vipindi vya Redio, Televisheni na mitandao ya kijamii.
Ameeleza, asilimia 70 ya watalii wanaokuja nchini huja kutalii kutokana na kusikia kutoka kwa watu na vyanzo mbalimbali vya habari.
" Asilimia 80 ya wageni wanaokuja ni wapya, Asilimia 20 pekee ndio wanarudi baada ya kutembelea vivutio vyetu.. ndani ya siku mbili hizi tujadili na tusaidie Wizara namna ya kuwarudisha watalii hao ili kuweza kufikia malengo ya kuwafikia watalii milioni tano ifikapo 2025 na mapato yanayotokana na utalii kufikia Dola za Kimarekani Bilioni 6... tukaze kamba kufikia malengo haya kwa ushirikiano wa Wanahabari na Hifadhi zetu," amesema.
Pia ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kwa ubunifu wa kuwakutanisha wanahabari na kueleza kuwa wanategemea mabadiliko makubwa hadi kufikia mwaka 2025.
Kwa upande wake Kamishina wa Uhifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Freddy Manongi amesema eneo hilo lilianza mwaka 1959 na tangu kuanzishwa kwake miaka 60 iliyopita TANAPA imeendelea kutimiza majukumu yake ikiwemo kulinda hifadhi na malekale, kuendeleza jamii zinaoishi ndani ya ya hifadhi na kuendeleza Utalii.
Amesema, tangu eneo hilo ligawanywe mwaka 1959 kutoka hifadhi ya Serengeti kwa mujibu wa Serikali ya Kikoloni, TANAPA imekuwa ikisimamia majukumu yake katika kuhakikisha Utalii wa Tanzania unapepea ulimwenguni kote.
Warsha hiyo itaenda sambamba na wanahabari kutembelea vivutio mbalimbali na kuvifahamu ili waweze kutangaza bidhaa za Utalii zinazopatikana katika hifadhi hiyo ikiwemo Utalii wa wanyama pori, malikale ya Olduvai gorge na Utalii mpya wa jiolojia ulioanza mwaka 2018.
Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya NCAA, jukwaa la Wahariri pamoja na Waandishi wandamizi katika kikao kazi kati ya NCAA na jukwaa la hilo kinachoendelea katika ofisi za makao Makuu ya NCAA Ngorongoro Crater Arusha.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki akizungumza na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Wahariri na Waandishi waandamizi wa Vyombo mbalimbali vya Habari wakati wa kufungua kikao kazi kati ya NCAA na jukwaa la Wahariri kujadili masuala mbalimbali kuhusu Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt Freddy Manongi akizungumza na Wahariri na Waandishi waandamizi wa Vyombo mbalimbali vya Habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kiuhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii kwa Wahariri kama sehemu ya wadau muhimu katika Sekta ya Uhifadhi na Utalii.
Mkuu wa Idara ya Mambo ya kale, Mhandisi Joshua Mwankunda akiwasilisha mada katika semina hiyo iliyofanyika leo Makao Mkuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro NCAA Karatu Mkoani Arusha
Mtafiti kutoka TAWIRI,Dkt Victor Kakenke akiwasilisha mada katika semina hiyo iliyofanyika leo kwenye makao makuu ya mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Karatu Mkoani Arusha.
Baadhi ya Makamishna wa Uhifadhi wakishiriki katika semina hiyo iliyowakutanisha Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na waandishi waandamizi kutoka vyombo vya habari.
Wahariri na Waandishi waandamizi wa Vyombo mbalimbali vya Habari wakifuatilia Mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na Wataalamu wa mambo ya Uhifadhi wakati wa semina iliohusu masuala mbalimbali ya kiuhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii kwa Wanahabari hao kama sehemu ya wadau muhimu katika Sekta ya Uhifadhi na Utalii.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...