MKUU wa Mkoa wa Ruvuma
Christina Mndeme amesema kukamilika kwa ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara
ya Mbinga hadi Mbambabay yenye urefu wa kilometa
66 kunafungua fursa mpya za kiuchumi.
Mndeme alikuwa
anazungumza wakati anafungua kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Ruvuma
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini Songea.
“Niwahakikishie
wananchi kuwa serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe.Dkt John Magufuli
imedhamiria kukamilisha na kuunganisha maeneo mbalimbali ya Mkoa wetu kwa
barabara za lami’’,alisema Mndeme.
Amesema barabara hiyo
inafungua sekta ya usafiri na usafirishaji ukanda wa ziwa Nyasa hivyo
kuhitimisha malengo ya serikali ya kufungua ushoroba wa Mtwara(Mtwara Corridor)
na kuunganisha kwa urahisi na usafiri wa ndege kupitia kiwanja cha Ndege Songea
na meli kupitia bandari ya Mbambabay ziwa Nyasa.
Mndeme amesisitiza kuwa
kukamilika kwa mtandao wa barabara ya Mbambabay kumewezesha Mkoa wa Ruvuma
kufunguka ambapo hivi sasa ajira na biashara zitaongezeka na kwamba hadi
kufikia Desemba 2020,Mkoa ulikuwa na kilometa 9,321.38 za mtandao wa barabara.
Hata hivyo amesema kati
ya kilometa hizo,Wakala wa Barabara Mkoa(TANROASDS) anahudumia na kutunza barabara zenye urefu wa kilometa 2,175.18.
Kwa upande wake Meneja
wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Lazack Alinanuswe amezitaja barabara za
Mkoa kuwa zina urefu wa kilometa 1,270.78 na
barabara kuu zina urefu wa kilometa 925.10.
“Wakala wa barabara za
vijijini na mijini TARURA wanahudumia barabara zenye urefu wa kilometa
7,146.2,hadi sasa Mkoa umefanikiwa kuongeza mtandao wa kilometa 800.48 sawa na
asilimia 8.6 ya barabara zote za TANROADS na TARURA’’,alisema.
Mkoa wa Ruvuma ni
miongoni mwa mikoa nchini ambayo makao makuu ya wilaya zote yameunganishwa kwa
mtandao wa barabara ya lami.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...