Katambi alianza ziara yake Desemba 31 mwaka 2020, na leo Januari 2, 2021 amehitimisha ziara hiyo ya kushiriki na kuhamasisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari halmashauri ya manispaa ya Shinyanga na kutoa kiasi cha fedha Shilingi Milioni 34, ili kuunga mkono ujenzi wa vyumba hivyo.
Amesema katika ziara hiyo ameridhishwa na ujenzi wa maboma ya vyumba hivyo vya madarasa ambayo yanajengwa kwa kiwango kinachotakiwa, pamoja na kasi ya kumalizia haraka wa jenzi hizo, ili wanafunzi watakapofungua shule waanze kuyatumia kusoma na kufanya vizuri kwenye masomo yao.
“Nashukuru sana wananchi kwa kujitoa nguvu kazi na michango yenu kushiriki kuchangia shughuli za maendeleo kwenye ujenzi huu wa vyumba vya madarasa, na mimi kama mbunge wenu nimeamua kushiriki na ninyi kwenye ujenzi huu wa vyumba vya madarasa, pamoja na kutoa fedha ili tukamilishe zoezi hili haraka na wanafunzi wasome katika mazingira mazuri,” amesema Katambi.
“Natoa wito pia kwa wadau wa elimu, zikiwemo taasisi za kifedha, makampuni, wajitokeze kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwamo vifaa vya maabara na madawati, ili majengo haya yatakapokamilika na vifaa hivyo viwepo na siyo wanafunzi kuanza kukaa chini sababu ya upungufu wa madawati,” ameongeza.
Pia ameiomba halmashauri iwe inagawa idadi sawa ya walimu hasa katika shule za pembezoni mwa mji ambazo zinakabiliwa na upungufu wa walimu ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi.
“Mfano katika shule ya msingi Twendepamoja iliyopo Mwamalili, ina jumla ya Wanafunzi 984, lakini kuna walimu Watano tu, na mmoja nimepewa taarifa anataka kuondoka hivyo itabakiwa na walimu Wanne kwa shule nzima, hili si sawa naomba uwiano uwepo kwa shule za mjini na pembezoni mwa mji, ili watoto wetu wafundishike na kufaulu,”ameeleza Katambi.
Katika hatua nyingine ameipongeza halmashauri ya manispaa ya Shinyanga kwa kuanzisha kiwanda chao cha ufyatuaji wa matofali, ambayo wanayatumia kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali na kuokoa gharama pamoja na kujenga majengo kwa kiwango kinachotakiwa sababu ya uimara wa matofari hayo.
Naye Mstahiki Meya wa manispaa ya Shinyanga David Nkulila, amesema kasi ambayo imeonekana kwenye ujenzi huo wa vyumba vya madarasa, ndiyo kasi ambayo wataendelea nayo kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi, ili kuendana na kasi ya Rais John Magufuli.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi amesema Serikali inashirikiana kikamilifu na wananchi kwenye ujenzi huo wa vyumba vya madarasa, na kubainisha katika Halmshauri hiyo inaupungufu wa vyumba 100, kwa shule za Msingi upungufu wa vyumba 64 na Sekondari vyumba 34.
Nao baadhi ya wanafunzi David Sharif anayesoma darasa la nne katika shule ya Msingi Ng’wihando, amemshukuru Mbunge Katambi kwa kushiriki kujenga vyumba hivyo vya madarasa, pamoja na Rais John Magufuli kwa kutoa elimu bila malipo ambayo imewafanya wasome ili kutumiza ndoto zao, huku akisema ndoto zake ni kuja kuwa Mbunge.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...