MSIMU wa 19 wa mbio maarufu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2021 umezinduliwa Kimkoa Mjini Moshi huku Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira akiahidi kuendelea kushirikiana na waandaaji na wadhamini wa mbio hizo ili kuzifanya kubwa zaidi na zenye manufaa makubwa kwa mkoa wake na nchi nzima kwa ujumla.
Akiwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaj Rajabu Kundya katika uzinduzi uliofanyika Kibo Palace Homes, alisema mbio hizo zimesaidia katika kukuza utalii na biashara katika mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania nzima kwa ujumla na yuko tayari kushirikiana na waandaaji kushugulikia changamoto mbalimbali zilizopo ili mbio hizo ziweze kuandikisha idadi kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Mghwira mbio hizo zinasajili takriban washiriki 12,000 na waandaaji wanashindwa kuongeza idadi hiyo kutokana na changamoto na barabara kuwa nyembamba.
“Tulishaanza mazungumzo ya namna gani tunaweza kutanua barabara zetu ili mbio hizi ziweze kusajili washiriki wengi zaidi kwani kwa sasa ikifikiwa idadi maalumu waandaaji wanalazimika kufunga usajili ili kuhakikisha wanaendana na matakwa na miongozo ya Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) na pia kijiridhisha kuwa wanaweza kutoa huduma muhimu kama maji, huduma ya kwanza na pia mbio zote zinaanza bila washiriki kusukumana na kukanyagana.'' Amesema.
Pia alitoa pongezi kwa mbio hizo kwa namna zimeendelea kuwaongezea kipato wafanya biashara wa Moshi na Kilimanjaro kwa ujumla kutokana na biashara kuongezeka wakati wa Kii Marathon ikiwemo suala la utalii wa michezo (sports tourism).Tukio ambalo huvutia zaidi ya wageni 25,000 katika mji wa Moshi ambao baadhi yao ni washiriki na watazamaji ambao pia hufurahia vivutio mbalimbali za kitalii na kupromoti shughuli nyingine za kiuchumi katika mji huo.
Kwa upande wake Meneja wa bia ya Kilimanjaro, Irene Mutiganzi ambaye pia ni meneja wa kinywaji cha Grand Malt , alisema wanajivunia kuwa wadhamini wakuu wa mbio hizo kwa mwaka wa 19 na kusisitiza kuwa kwao ni jambo la kizalendo kwani ni shughuli ambayo inautangaza Mkoa wa Kilimanjaro, utalii na kuongeza kipato kwa nchi kwa ujumla.
Aidha alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mbio za mwezi ujao ambapo wametenga shilingi milioni 25 kwa ajili ya zawadi za washindi wa kwanza kwa mbio hizo kwa upande wa wanaume na wanawake ambapo washindi watajinyakulia shs milioni 4 kila mmoja na watanzania wa kwanza upande wa wanaume na wanawake watapata shs milioni 1.5 kama motisha .
Aidha Irene pia amewataka wale ambao watapenda kushiriki kwenye mbio za kilometa 5 nao wajisajili mapema kwani nafasi za ushiriki zitakuwa chache kwa mara nyingine tena.
Naye Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini Henry Kinabo, ambaye kampuni yake inadhamini mbio za Km 21 alisema mwaka huu wanatarajia Tigo Kili Half Marathon yenye msisimko wa aina yake na burudani . “Usajili kwa njia ya Tigo Pesa umepokewa vizuri kwani hadi sasa wamejisajii washiriki 3, 917 katika mbio za KM 42, 21 na 5.
Alisema huu ni mwaka wa sita kwao kudhamini Tigo Kili Half Marathon na kama wadhamini wanatoa wito kwa washiriki wendelee kujisajili kwa njia ya Tigo Pesa kwa kuwa ni rahisi na haraka.
Wadhamini wengine ni pamoja na Kilimanjaro Drinking Water, TPC Limited, Unilever Tanzania, Simba Cement, Absa Bank Tanzania na watoa huduma rasmi Keys Hotel, Garda World Security na CMC Automobiles na bila kuwasahau waandaaji Kilimanjaro Marathon Company na Executive Solutions mbao ni waratibu kitaifa.
Katika kuongezea juhudi za Serikali za kuzuia Covid 19 kupitia hatua mbalimbali katika maeneo yote ya kuingilia nchini , waandaaji wa mbio za Kilimanjaro Marathoni watahakikisha wanafuata miongozo ya serikali.
Hafla ya uzinduzi huo ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kilimanjaroaa, Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo, Cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro (KAAA), vilabu mbalimbali, wawakilishi wa wanariadha, wafanyabiashara na vyombo vya habari.
Usajili wa mbio hizo zitakazofanyika Jumapili Februari 28, 2021 katika Chuo Kikuu cha Ushirika cha Moshi (MoCU), unaendelea kwa njia ya mtandao (www.kilimanjaromarathon.com) na Tigopesa *149*20#
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...