Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Shirika
la Nyumba la Taifa litaanza kuwabana wapangaji wake wanaodaiwa takriban
Bilioni 27 ikiwa ni malimbikizo ya upangishaji nyumba zake kwa
kuwatangaza na kunadi mali zao kufidia deni kufikia mwisho wa mwezi
Januari 2021.
Shirika hilo la nyumba la NHC lina takriban
wapangaji 17,000 katika mikoa mbalimbali nchini zikiwemo taasisi za umma
na binafsi wanaodaiwa kodi nyumba kama malimbikizo ya kodi hiyo baada
ya kushindwa kulipa kwa wakati.
Akizungumza wakati wa kikao cha
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
na watendaji wa Sekta ya ardhi jijini Arusha tarehe 9 Januari 2021
Meneja Huduma za Jamii na Uhusiano wa NHC Muungano Saguya alisema, kwa
jiji la Arusha pekee shirika lake linadai wapangaji zaidi ya milioni
370 na kusisitiza kuwa zoezi hilo ni la nchi nzima.
Alisema, njia
pekee kwa wadaiwa wa kodi ya pango la nyumba wa Shirika hilo kuepuka
kuchukuliwa hatua ikiwemo kuwatangaza katika vyombo vya habari ni
kuhakikisha wanalipa malimbikizo na kodi wanazodaiwa kabla ya januari
31, 2021.
Kwa mujibu wa Saguya, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
linategemea fedha za wapangaji wake na miradi mbalimbali inayofanya
kujiendesha hivyo kutolipwa fedha za upangishaji ni kufifisha juhudi za
Shirika katika kujiendesha kibiashara.
"Shirika letu la NHC
linategemea fedha za upangishaji nyumba zake na miradi kujiendesha
kibiashara hivyo kutolipa kodi kunalifanya Shirika kushindwa kujiendesha
kwa ufanisi" alisema Saguya.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema zoezi
linaloendelea la kuwafikisha wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi
katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya liende sambamba na
kuwachukulia hatua wapangaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
wanaodaiwa kodi ya nyumba.
Alisema, Shirika la Nyumba la Taifa
linategemea kwa asilimia mia moja kujiendesha hivyo wapangaji wake
kushindwa kulipa kodi kwa wakati kunalifanya kushindwa kufanya kazi kwa
ufanisi.
"Msako wa kodi ya ardhi pango la ardhi uende sambamba
pia na wale wadaiwa wa Shirika la Nyumba la Taifa maana Shirika
hujitegemea kwa asilimia mia moja, tusipolipa tutalikwamisha kufanya
kazi" alisema Dkt Mabula.
Shirika la Nyumba la Taifa ni moja ya
taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na
mbali na upangishaji wa nyumba zake hujishughulisha pia na kazi
mbalimbali kama vile ukandarasi wa miradi na upangaji miji ambapo kwa
sasa linaendesha miradi ya ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mtwara na
Kwangwa Mara, Ofisi za wilaya za Hai Kilimanjaro na Wanging'ombe Njombe
pamoja na ujenzi wa Ofisi na nyumba 17 za Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS).
Meneja Huduma za Jamii na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa
Muungano Saguya akizungumzia wadaiwa wa kodi wa nyumba za Shirika lake
wakati wa kikao cha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
na Watendaji wa Sekta ya Ardhi mkoani Arusha tarehe 9 Januari 2021.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa mkoa wa Arusha waliojitokeza kuwasilisha malalamiko wakati wa ziara ya kikazi katika mkoa wa Arusha tarehe 9 Januari 2021
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...