Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imesema imejipanga kuhakikisha inatoa mchango wake kwa wakulima wa mazao ya mafuta nchini huku ikiwataka wakulima wenyewe kutumia fursa hii ya upungufu wa mafuta katika kuandaa mashamba yao ili waweze kuzalisha mazao hayo kwa wingi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda leo jijini Dodoma wakati alipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha kutengeneza mafuta cha Pyxus.

Waziri Prof Mkenda amesema serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya kiuwekezaji kwa wawekezaji wote ambao wamekua wakiwekeza kwenye kilimo ikiwemo cha mazao ya mafuta huku akiwataka wakulima kuzingatia mikataba ambayo wamekua wakiingia na wawekezaji hao.

Prof Mkenda amesema suala la uhaba wa mafuta hivi sasa nchini limesababishwa na hali ya hewa ambapo kwa mwaka jana hali ya unyevunyevu ilikua nyingi kiasi cha kuchangia uzalishaji mdogo huku ugonjwa wa Corona ukisababisha uzalishaji kushindwa kufanyika kwa kasi kwenye Nchi ya Malaysia inayolima Mawese na Nchi za Latini Amerika ambazo zinalima mazao ya Soya.

" Kumekua na uhaba wa mafuta kwa sasa lakini hali hii tuitumie kama fursa katika kuyaandaa mashamba yetu ili kuongeza uzalishaji mkubwa ambao utakidhi mahitaji ya Tani Laki Tano kwa mwaka na kuepuka gharama za uagizaji nje ya nchi ambazo huigharimu nchi fedha nyingi za kigeni," Amesema Prof Mkenda.

Amesema mpango wa serikali ni kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya mafuta kutoka mikoa minne kwa sasa na kuwa na idadi kubwa ya mikoa inayozalisha ili kuwa na akiba kubwa ya mafuta ambayo watauza ndani ya Nchi na nchi nyingine za nje ambazo zimekua na uhitaji mkubwa.

Kwa upande wake Meneja wa Wakulima Wadogowadogo wa Kampuni hiyo ya Pyxus, Edwin Shiyo amemshukuru Waziri Prof Mkenda kwa kufika kwenye kiwanda hicho kujionea shughuli za uendeshaji ambapo amemuahidi kiwanda hicho kitaendelea kushirikiana na serikali katika kukuza uchumi .

" Tunashukuru Waziri ameahidi kumaliza changamoto iliyokua inatukabili pale Bandarini tunaposafirisha mazao yetu nje ya nchi hasa nchini Uswis, tulikua tunacheleweshwa bandarini hata wiki mbili, hivyo kwa kauli ya Waziri tunaamini sasa tutafanya kazi zetu kwa ufanisi tukiiletea mapato ya fedha za kigeni nchi yetu," Amesema Shiyo.

Waziri wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda akitoa maelekezo kwa viongozi wa wizara hiyo na viongozi wa kiwanda cha Pyxus alipokitembelea leo jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda akipatiwa maelezo ya uzalishaji wa mafuta katika kiwanda cha Pyxus kilichopo jijini Dodoma alipofanya ziara ya kukitembelea.
Waziri wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda akikagua uzalishaji wa mafuta katika kiwanda cha Pyxus kilichopo jijini Dodoma alipokitembelea leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...