Naibu Waziri wa Ujenzi
na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na uongozi wa Mamlaka ya
Usafiri wa Anga (TCAA), wakati alipotembelea Mamlaka hiyo, jijini Dar es
Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Bw. Hamza Johari, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (hayupo pichani), wakati alipotembelea Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Dkt. Agness Kijazi, akitoa taarifa kwa Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (katikati), namna
mamlaka hiyo inavyofanya kazi.
Naibu Waziri wa Ujenzi
na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa nne kutoka kulia), akiwa katika
picha ya pamoja na uongozi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), wakati
alipotembelea Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.
MAMLAKA ya Hali ya Hewa
nchini (TMA), imetakiwa kutangaza taarifa zake kwa vyombo vya habari vingi
kadri iwezekanavyo ili zisaidie wananchi kupanga mipango yao ya kimaendeleo na
kujiepusha na majanga yanayoweza kuepukika.
Hayo yamesemwa na Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alipokagua shughuli
zinazofanywa na Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
“Tafuteni vyombo vingi
vya habari ili vitangaze taarifa zenu kwa kuwa ni taarifa muhimu kwa mustakabali
wa Taifa na watu wake”, amesema Naibu Waziri huyo.
Amesisitiza umuhimu wa
TMA kuweka taarifa zake zote katika mifumo ya kieletroniki ili ziweze
kupatikana kwa urahisi kwa watu wengi na mahali popote.
Awali akitoa taarifa ya
kiutendaji, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agness Kijazi, amesema Mamlaka yake
imejipanga kushirikiana na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kutangaza
taarifa za utabiri kwa wakati.
Amesema usahihi wa
utabiri unaotolewa na TMA kwa sasa ni kati ya asilimia 84 hadi 86 hivyo
kuifanya Tanzania kupata fursa mbalimbali za wataalamu wake kushiriki katika
masuala muhimu ya Shirika la Kimataifa la Hali ya Hewa (WMO.)
Katika hatua nyingine,
Naibu Waziri Kasekenya ametembelea na kuzungumza na Mamlaka ya Usafiri wa Anga
(TCAA), na kuwapongeza kwa uwekezaji mkubwa wa vifaa na utalaamu walioufanya na kuwezesha mamlaka hiyo kupiga hatua katika
kuboresha huduma zake toka asilimia 37 mwaka 2013 hadi asilimia 69.5 mwaka
2020.
Mhandisi Kasekenya,
amewataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa uzalendo na bidii na
kuhakikisha usalama wa anga la Tanzania kuwa ndio kipaumbele chao namba moja.
Aidha, amemtaka
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA kutoa motisha kwa wafanyakazi ili kuwajengea ari ya
kufanya kazi na kukuza uzalendo miongoni mwao.
Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Dar es Salaam katika ziara ya kukagua taasisi zilizo chini ya Wizara yake ambapo ametembelea na kuzungumza na uongozi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA.)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...