Na Muhidin Amri,Mbinga
KAMPUNI ya Chico inayojenga barabara kwa kiwango cha lami kilomita 66
kutoka Mbinga hadi Mbambabay wilaya ya Nyasa imesema kazi ya ujenzi wa
barabara hiyo umekamilika kwa wakati kama ilivyoahidi kwa Rais Dkt John
Magufuri wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo mwezi
April 2019.
Meneja msaidizi wa mradi huo Sam Han alisema, barabara hiyo kwa sasa
imekamilika kwa asilimia 100 ambapo kazi kubwa ilikuwa kukata
milima,kuondoa kifusi kisicho hitajika barabarani pamoja na kujenga
makalavati kazi ambayo imeshafanyika kwa ufanisi mkubwa.
“ Kazi kubwa katika ujenzi wa barabara ilikuwa kukata milima,kutoa
udongo wa juu usiohitajika na kujaza kifusi kipya na kujenga
makalavati,hivyo matumaini yetu kwamba ifikapo Disemba mwaka huu mradi
utakamilika kama tulivyohaidi kwa Mheshimiwa Rais Dkt John
Magufuri”alisema Sam.
Hata hivyo Sam alisema, changamoto kubwa waliyokutana nayo katika ujenzi
wa mradi huo ni kuwepo kwa milima mikubwa,kona nyingi na mawe mengi
hasa eneo la Chunya, lakini kutokana na uwezo na umahiri mkubwa wa
Chico katika ujenzi wa miundombinu hasa ya barabara kazi inaendelea na
itakamilika kwa muda muafaka.
Sam alisema, ni matumaini ya Chico kuwa, baada ya kukamilika barabara
hiyo itachochea kukua kwa uchumi na kuharakisha maendeleo ya wakazi wa
Nyasa na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla na ameiomba Serikali ya Tanzania
kupitia wizara ya ujenzi kushirikiana na Chico katika ujenzi wa
barabara na miradi mingine hapa nchini.
Alisema, baada ya kukamilika wananchi wameanza kunufaika kwa
kubadilisha maisha yao ikiwemo kupunguza gharama ya usafiri na
kusafirisha mazao,bidhaa mbalimbali na samaki wanaopatikana kwa
wingi katika ziwa nyasa kwenda katika masoko mbalimbali ya ndani na nje
ya mkoa wa Ruvuma.
Kwa mujibu wa Sam, kujengwa kwa barabara hiyo kumehamasisha watu wengi
kutoka ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma kwenda kuwekeza wilayani humo
katika miradi mbalimbali ikiwemo nyumba za kulala wageni,biashara ya
usafirishaji,kilimo na uvuvi hivyo kuchangia sana kukua kwa uchumi wa
wananchi wa kawaida na wilaya ya Nyasa.
Alisema, Chico imefanya kazi usiku na mchana, ili kuhakikisha barabara
hiyo inakamilika kwa muda uliopangwa na imejengwa kwa ubora mkubwa na
kuwa mfano kwa barabara nyingine hapa nchini.
“sisi kama kampuni ya Chico tunaamini barabara hii ni mfano, kwani
tumitumia uzoefu wetu na weledi wa hali ya juu katika ujenzi
wake,tunataka watanzania watukumbuke na watumie barabara hii kujiletea
maendeleo na kukuza uchumi wao”alisema Sam.
Baadhi ya wananchi wameishukuru Serikali ya awamu ya tano kupitia wizara
ya ujenzi kwa jitihada zake za kuwaondolea kero ya usafiri
iliyowasumbua kwa muda mrefu.
Wameipongeza kampuni ya Chico kutokana na uwezo mkubwa kwa kujenga
barabara hiyo na matumaini yao, mara itakapo kamilika itakuwa mkombozi
na kuharakisha maendeleo ya Nyasa na wilaya mama ya Mbinga.
Boniface Ndunguru mkazi wa kijiji cha Nyoni wilayani Mbinga alisema,
kampuni ya Chico imeonesha weledi wa hali ya juu katika utekelezaji wa
mradi huo na kuiomba Serikali kuendelea kuitumia kampuni hiyo katika
miradi mbalimbali ya ujenzi.
Nyoni alisema, kujengwa kwa barabara hiyo ni faraja kubwa kwa wananchi
wa wilaya hizo mbili na mkoa wa Ruvuma kwa jumla, kwani imeanza kufungua
mawasiliano ya barabara kati ya wilaya ya Nyasa na maeneo mengine.
Mkazi mwingine Alex Massimba amesema, kuimarishwa kwa miundombinu ya
barabara kuna faida kubwa kwa wananchi wa kipato cha chini kwa sababu
gharama za usafi zimeanza kupungua na kufika kwa wakati katika shughuli
zao za kila siku.
Alisema, kabla ya kujengwa kwa barabara hiyo wananchi waliteseka sana
na wapo waliopoteza maisha kwa kushindwa kufikia katika vituo vya
kutolea huduma kwa muda sahihi kutokana na miundombinu duni ya barabara.
“kwa kweli tunaipongeza sana kampuni ya Chico kujenga barabara hii kwa
ubora na weledi wa hali ya juu ikilinganishwa na baadhi ya barabara za
lami zinazojengwa katika mikoa mingine hapa nchini,tunamuomba Rais Dkt
John Magufuri na Serikali yake iwape upendeleo mkubwa ndugu zetu wa
CHICO kwenye miradi mbaimbali,hii kampuni imeonesha uwezo
mkubwa”alisema.
Alisema, ni faraja kwa wananchi wa Nyasa kuona wanaondoka katika
mateso makubwa yaliyotokana na ukosefu wa miundombinu ya uhakika kwa
kuwa wapo baadhi ya wananchi wakiwemo wanawake wajawazito waliopoteza
maisha kwa kuchelewa kufika zahanati,vituo vya afya na Hospitali
kutokana na tatizo la miundombinu duni ya barabara, hivyo kukamilika kwa
barabara hiyo kutaokoa maisha ya watanzania wengi hasa wale wenye
kipato cha chini.
,Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya akipiga magoti
katikati ya barabara ya lami inayojengwa na kampuni ya Chico, kama
ishara ya kuishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kujenga barabara
hiyo kutoka Mbinga hadi Mbambabay yenye urefu wa km 66 ambayo ujenzi wake
umekamilika kwa asilimia 99.
Mwanasheria wa kampuni ya Chico inayojenga barabara ya lami kutoka
Mbinga hadi Mbambabay wilaya y,a Nyasa mkoani Ruvuma Gaudence Ndomba
kulia, akitoa ufafanuzi wa baadhi ya changamoto walizokutana wakati wa
ujenzi wa barabara hiyo ambayo inatajwa itachochea kukua kwa uchumi wa
wananchi wa wilaya hizo mbili,wa kwanza kushoto meneja msaidizi wa mradi
wa ujenzi kutoka kampuni ya Chico Sam Han,wa pili kushoto mkuu wa
wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba.
Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Isabela Chilumba wa pili kushoto
akimsikiliza meneja msaidizi wa mradi wa ujenzi wa Barabara ya lami
Mbambabay hadi Mbinga yenye urefu wa km 66 ya Chico Sam Han,baada ya
mkuu wa wilaya kutembelea ujenzi wa barabara hiyo eneo la Mbambabay
wilayani humo,kulia mwanasheria wa Chico Gaudence Ndomba. Picha zote na Muhidin Amri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...