Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Dkt. Agness Kijazi, akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (katikati), namna mamlaka hiyo inavyofanya kazi.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na uongozi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Dkt. Agness Kijazi, wakati alipotembelea Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa nne kutoka kulia), akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), wakati alipotembelea Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na uongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), wakati alipotembelea Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Bw. Hamza Johari, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (hayupo pichani), wakati alipotembelea Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), wakati alipotembelea Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.

***********************************

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imetakiwa kutangaza taarifa zake kwa vyombo vya habari vingi kadri iwezekanavyo ili zisaidie wananchi kupanga mipango yao ya kimaendeleo na kujiepusha na majanga yanayoweza kuepukika.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alipokagua shughuli zinazofanywa na Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.

“Tafuteni vyombo vingi vya habari ili vitangaze taarifa zenu kwa kuwa ni taarifa muhimu kwa mustakabali wa Taifa na watu wake”, amesema Naibu Waziri huyo.

Amesisitiza umuhimu wa TMA kuweka taarifa zake zote katika mifumo ya kieletroniki ili ziweze kupatikana kwa urahisi kwa watu wengi na mahali popote.

Awali akitoa taarifa ya kiutendaji, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agness Kijazi, amesema Mamlaka yake imejipanga kushirikiana na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kutangaza taarifa za utabiri kwa wakati.

Amesema usahihi wa utabiri unaotolewa na TMA kwa sasa ni kati ya asilimia 84 hadi 96 hivyo kuifanya Tanzania kupata fursa mbalimbali za wataalamu wake kushiriki katika masuala muhimu ya Shirika la Kimataifa la Hali ya Hewa (WMO).

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya ametembelea na kuzungumza na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), na kuwapongeza kwa uwekezaji mkubwa wa vifaa na utalaamu walioufanya  na kuwezesha mamlaka hiyo kupiga hatua katika kuboresha huduma zake toka asilimia 37 mwaka 2013 hadi asilimia 69.5 mwaka 2020.

Mhandisi Kasekenya, amewataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa uzalendo na bidii na kuhakikisha usalama wa anga la Tanzania kuwa ndio kipaumbele chao namba moja.

Aidha, amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa TCAA kutoa motisha kwa wafanyakazi ili kuwajengea ari ya kufanya kazi na kukuza uzalendo miongoni mwao.

Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Dar es Salaam katika ziara ya kukagua taasisi zilizo chini ya Wizara yake ambapo ametembelea na kuzungumza na uongozi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...